• HABARI MPYA

  Ijumaa, Agosti 16, 2019

  YANGA SC YACHAPWA 2-0 NA POLISI TANZANIA LEO MOSHI, KESHO NA AFC LEOPARDS ARUSHA

  Na Saada Akida, KILIMANJARO
  YANGA SC imepoteza mechi ya kwanza ya msimu mpya baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Polisi Tanzania katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
  Kipa wa tatu, Ramadhani alianza kipindi cha kwanza na akatunguliwa bao moja kabla ya kipa anayewani kuwa wa kwanza, Mkenya Farouk Shikalo anayechuana na Metacha Mnata kuruhusu bao la pili baada ya kuingia kipindi cha pili.
  Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Marcel Kaheza alifunga kwa penalti Polisi Tanzania dakika ya sita baada ya beki Mrundi, Mustafa Suleiman kunawa mpira uliopigwa na Ditram Nchimbi, anayecheza kwa mkopo kutoka Azam FC.
  Yanga SC ilijitahidi kusaka bao la kusawazisha, lakini washambuliaji wake Mzambia Maybin Kalengo na David Molinga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wakashindwa kuupenya ukuta wa Polisi ulioongozwa na beki Iddy Mobby. 
  Kipindi cha pili pamoja na mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mkongo wa Yanga, Mwinyi Zahera akiwaingiza beki Juma Abdul na kiungo mshambuliaji Issa Bigirimana kwenda kuchukua nafasi za Kelvin Yondan na Deus Kaseke, lakini mambo hayakubadilika.
  Mshambuliaji mpya, Ditram Nchimbi aliyesajiliwa kutoka Azam FC akaifungia Polisi Tanzania bao la pili dakika ya 74 akitumia makosa ya walinzi wa Yanga kumtungua ‘Kipa Asiyefungika’, Shikalo kwa kumbisha kanzu.
  Molinga alikaribia kufunga kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka nje kidogo ya boksi dakika ya 87, lakini kipa Yussuf Mohammed aliyesajiliwa kutoka Lipuli FC ya Iringa akapangua.
  Huu unakuwa mchezo wa kwanza Yanga SC inapoteza msimu huu mpya, baada ya awali kushinda mechi mechi tano, 4-1 dhidi ya Mlandege ya Zanzibar, 2-0 dhidi ya Friends Rangers, 7-0 dhidi ya ATN, 2-0 dhidi ya Moro Kids na 1-0 dhidi ya Mawenzi Market zote mjini Morogoro na sare tatu zote 1-1 na Township Rollers ya Botswana, Malindi SC ya Zanzibar na Kariobangi Sharks ya Kenya.
  Baada ya mchezo wa leo, Yanga itasafiri kwenda mkoa jirani, Arusha kwa ajili ya mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya AFC Leopards ya Kenya keshokutwa jioni Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
  Yanga imeweka kambi mjini Moshi kujiandaa na mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Township Rollers utakaofanyika Agosti 24 Uwanja wa Taifa mjini Gaborone kufuatia timu hizo kutoka sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Jumamosi ilitopita.
  Kikosi cha Polisi Tanzania kilikuwa; Mohammed Yussuf, William Lucian ‘Gallas’/Shaaban Stambuli dk48, Yassin Mustafa, Othman Mmanga, Iddi Mobby, Baraka Majogoro, Andrew Chamungu, Nassor Abbal, Ditram Nchimbi, Marcel Kaheza/Erick Msagati dk54 na Sixtus Sabilo/Pato Ngonyani dk62. 
  Yanga SC; Ramadhani Kabwili/Farouk Shikalo dk46, Mustafa Suleiman, Gustafa Simon/Jaffar Mohammed dk56, Ali Ali, Kelvin Yondan/Juma Abdul dk66, Abdulaziz Makame, Maybin Kalengo, Feisal Salum, David Molinga, Raphael Daudi na Deus Kaseke/Issa Bigirimana dk56.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YACHAPWA 2-0 NA POLISI TANZANIA LEO MOSHI, KESHO NA AFC LEOPARDS ARUSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top