• HABARI MPYA

  Saturday, August 17, 2019

  SIMBA SC YAIPIGA AZAM FC 4-2 NA KUBEBA NGAO YA JAMII KWA MARA YA TATU MFULULIZO

  Na Asha Said, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imefanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii baada ya ushindi wa 4-2 dhidi ya Azam FC kwenye mchezo mzuri uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam usiku wa leo kuashiria ufenguzi wa msimu mpya nchini.
  Shujaa wa Simba SC leo alikuwa ni mchezaji mpya kutoka Sudan, Sharaf Eldin Shiboub aliyefunga mabao mawili kipindi cha kwanza kabla ya viungo wenzake, Mzambia Clatous Chama na Mkenya Francis Kahata kuongeza mawili kipindi cha pili.
  Hiyo inakuwa mara ya tano kwa Simba SC kutwaa Ngao ya Jamii, baada ya mwaka jana wakiichapa Mtibwa Sugar 2-1, mwaka 2011 wakiifunga Yanga 2-0, mwaka 2012 wakiifunga Azam FC 3-2 na mwaka 2017 wakiwafunga tena mahasimu wao wa jadi, Yanga kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0.

  Azam FC iliyotwaa Ngao ya Jamii mara moja tu mwaka 2016 walipoifunga Yanga kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 2-2, leo imepoteza mechi ya tano ya Ngao baada ya mwaka 2012 walipofungwa 3-2 na Simba SC, 2013 walipofungwa 1-0 na Yanga SC, 2014 walipofungwa 3-0 na Yanga SC na 2015 walipofungwa na Yanga SC kwa penalti 8-7 baada ya sare ya 0-0.
  Azam FC waliuanza vizuri mchezo wa leo na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 13 tu, mfungaji mshambuliaji wake Shaaban Iddi Chilunda aliyefanikiwa kuwatoka walinzi wa Simba baada ya pasi ya mshambuliaji mpya, Muivory Coast, Richard Djodi.
  Shiboub akaisawazishia Simba SC dakika ya 16 Simba akimalizia kwa kichwa mpira uliotemwa na kipa Mghana, Razack Abalora kufuatia shuti la kiungo Hassan Dilunga.
  Shiboub tena akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 22 kwa kichwa pia akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Mohammed Hussein Tshabalala.
  Kipindi cha pili Simba SC ikaendelea kutawala mchezo na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 56 lililofungwa na Chama aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Nahodha, John Bocco aliyeumia katikati ya kipindi cha kwanza.
  Kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Frank Raymond Domayo akaifungia Azam FC bao la pili dakika ya 78 kwa shuti la mbali kabla ya Kahata aliyetokea benchi pia kuifungia Simba bao la nne dakika ya 83.
  Mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere hakuwa mwenye bahati leo, baada ya kupiga nje kidogo ya lango mara mbili na mara moja Abalora akiokoa.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razak Abalora, Nico Wadada/Obrey Chirwa dk63, Bruce Kangwa/Salmin Hoza dk58, Oscar Maasai, Yakubu Mohammed, Frank Domayo, Emmanuel Mvuyekure/Abdulhaj Omar ‘Hama Hama’ dk74, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Shaaban Iddi Chilunda/Iddi Kipagwile dk69, Richard Djodi na Joseph Mahundi/Masoud Abdallah ‘Cabaye’ dk51.
  Simba SC: Benno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Deo Kanda/Miraj Athumani dk74, Sharif Shiboub/Gerson Fraga Vieira dk83, John Bocco/Clatous Chama dk27, Meddie Kagere na Hassan Dilunga/Francis Kahata dk59.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAIPIGA AZAM FC 4-2 NA KUBEBA NGAO YA JAMII KWA MARA YA TATU MFULULIZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top