• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 28, 2019

  SIMBA SC KUTOLEWA MAPEMA LIGI YA MABINGWA KUNA FUNDISHO

  Na Dominick Salamba, DAR ES SALAAM
  Imekuwa ni jambo la kushangaza huku wengi wakiwa hawaamini kilichotokea Kwani katika hali ya kawaida wadau wengi waliamini Simba ni lazima ipite hatua hii ya kwanza wakilinganisha na mafanikio ya msimu uliopita.
  Yapo mengi sana yatasemwa kama ilivyo ada ila kwa upande wangu nimeona mambo yafuatayo na mengine nilishaandika katika makala zangu za siku za nyuma!
  1. Usajili uliofanywa
  Niliwahi kuandika nikishangaa na kuhoji kwanini klabu ya Simba inasajili wachezaji wengi zaidi ya 10 wakati tayari gari lilikuwa limewaka na kuhitaji kutia gia ya mwendo kasi..Kwani msimu uliopita walikuwa na kikosi bora ambacho kilikuwa na maelewano makubwa na kuwa na kasoro ndogondogo tu na pengine kuhitaji marekebisho madogo sana ili kuongeza uimara wao lakini cha ajabu ni sawa na kulizima gari ambalo tayari lilisha waka na kuanza kulisukuma tena.
  Simba SC ya msimu uliopita ilikuwa na mapungufu yasiyozidi manne kwa maana beki wa kati mzoefu,kiungo mkabaji,winga mmoja wenye kasi na mshambuliaji mmoja wa kati aliyekamilika basi.Lakini cha kushangaza umefanyika usajili ambao hauendani na kile ambacho tulikisikia kikisemekana mitandaoni na kwenye vyombo vya habari,unaposajili wachezaji zaidi ya 10 ni sawa na kuanza upya na kufanya kazi iwe ngumu kwa benchi la ufundi katika kutafuta muunganiko ukizingatia na mda wa maandalizi haukuwa wa kutosha hivyo kilichofanyika ni kurudi nyuma hatua tano huku ulishapiga hatua mbili mbele,na hapa ndipo ninapotamani kujua kama zile ripoti za mabenchi ya ufundi kila mwisho wa msimu huwa zinafanyiwa kazi kwa kiwango kinachostahili au ndio kufungana midomo kunachukua nafasi na walimu kubaki na siri nzito vifuani mwao?
  2. Pengo la James Kotei na Emanuel Okwi bado linaonekana.
  Siku niliyosikia James Kotei akijiunga na klabu ya Kaiza Chiefs ya huko Afrika Kusini nilishtuka sana ila nikajiuliza kwani tarehe za kufungwa dirisha la usajili bado?nikakuta muda bado upo nikasema kama Kotei kaachwa basi huenda Simba wamepanga kuleta kiungo wa kiwango cha juu katika ukabaji barani Afrika,siku zikapita mwisho nakuja kuona kuna kiungo kutoka nchini Brazil. Daah nilichoka nikawaza inawezekana vipi kwa timu ambayo imefikia katika hatua nzuri kuwa na kiwango bora kucheza kamali na wachezaji kutoka Bara lingine tena ambao sidhani kama walikuwa katika viwango bora huko walikotoka zaidi ya rekodi za kwenye Wikipedia? 
  Nikajiuliza Simba imecheza na Nkana,AS Vita,Mazembe Kweli imeshindwa kuona kiungo wa haja ambaye ana kitu na kuleta tija ndani ya Simba SC? nikaenda mbali na kuwaza ni kweli Mkude anaweza kutimiza majukumu ya ukabaji?
  Nani anaendelea kuwaaminisha kuwa Mkude ni kiungo mkabaji? ipo siku nitamchambua kwa kina  Mkude kwa nia njema kuonesha ubora na madhaifu yake ila kifupi ni kiungo mzuri kwenye kushambulia ila si mzuri kwenye ukabaji ndio mana uwepo wa Kotei ulileta muunganiko mzuri kwani Kotei alikuwa anakaba kwa kuzunguka eneo lote la kati huku mkude akikaba kwa kujimegea eneo jambo ambalo limewagharimu katika mechi ya UD Songo.
  Pia usajili wa Kahata,na Deo Kanda bado hujaziba pengo la Okwi ingawa Deo Kanda anakasi na vitu vingi ila swala la kufunga na kutengeneza nafasi bado yupo nyuma kumlinganisha na Okwi labda tumpe muda ila kwa sasa bado.
  3. Mtazamo wa mechi ya ugenini dhidi ya UD Songo uliwamaliza Simba SC.
  Pamoja na kutolewa na UD Songo bado Simba SC wanakikosi kizuri kulinganisha na UD Songo na hata mafanikio na uzoefu bado Simba sc wapo juu,hivyo mtazamo wa kwenda kutafuta sare ugenini kwa timu kama UD Songo haukuwa sahihi kwani walikuwa na uwezo wa kushambulia na kupata matokeo ugenini ila mtazamo kuwa wapate hata sare ili waje kumaliza mechi Dar-es -salaam uliwamaliza na kujikuta wakiwa kwenye presha kubwa kwenye mechi ya marudiano lakini pia mwalimu aliendelea kufanya makosa kwa kutodhani kama UD Songo wanaweza kupata bao ugenini huku akijikita zaidi kushambulia lakini akisahau kuweka mbinu bora za ulinzi.
  4. Benchi la ufundi lilitumia muda mwingi kuiandaa Simba bila kuwaza pia ubora wa UD Songo.
  Kuna msemo unasema siku zote timu kubwa hujiandaa wao wenyewe bila kushughulika na timu ndogo wanazokutana nazo inaweza ikawa sawa ila pia lazima uangalie na aina ya michuano, Simba sc walikuwa kwenye mechi za mtoano ambapo kosa moja unatolewa lakini pia makosa ambayo waliyafanya kwenye mechi ya awali nilitegemea wangeyafanyia kazi kwani walifanya makosa zaidi ya matano ambayo kama UD Songo wangekuwa makini mambo yangekuwa tofauti lakini wakabaki na dhana ya wao ni timu kubwa na kujiandaa wakizingatia ubora wao na wakiamini wao ndio wenye haki ya kushambulia na kupata matokeo na pengine UD Songo hawatakiwi kupata bao bila kuwa na namna nzuri ya kuweka ulinzi.
  Wakati Simba sc wakijivunia na ubora walio nao kwa upande wa UD Songo wao walijikita kuangalia ubora na udhaifu wa Simba sc na kweli waligundua mambo yafuatayo na kuyafanyia kazi.
  ●Simba wazuri kwenye kumiliki mpira ila hawana  kasi kwenye kushambulia hivyo njia nzuri ya kuwakabili ni kuwashambulia kwa kushtukiza na wakifanikiwa kupata mpira jambo la kwanza ni kurudi nyuma kwa haraka na kuziba mianya huku wao wakibaki kupiga pasi nyingi eneo la kati na kufanikiwa kuwadhibiti.
  ●Mipira ya krosi inapigwa na walinzi wa pembeni wakati mawinga wao wakiwa kati kuongeza idadi ya washambuliaji hivyo endapo utafanikiwa kuokoa mipira ya krosi ni vyema kuicheza pembeni na kuleta madhara makubwa kwa simba sc kwani pembeni kunakuwa kweupe sana uku mawinga wao wakiwa hawana nguvu katika ukabaji na kupelekea ukuta wao kutawanyika na kuwa na idadi ndogo ya walinzi uku wakiwa kwenye umbali mkubwa kati ya mlinzi mmoja kwenda kwa mlinzi mwingine
  ●Safu ya kiungo ya Simba sio wazuri kwenye kukaba wanapenda kuchezea mipira sana hivyo njia bora ni kuwa na wachezaji wengi eneo la kati na kutumia mipira mirefu kuwachosha viungo wa simba ambao hawapendi kukimbia kuutafuta mpira.
  ●Safu ya ulinzi ya Simba ina walinzi bora wenye uzoefu na umiliki mzuri wa mpira ila sio wepesi kwenye kugeuka na kufanya maamuzi ya haraka hivyo ukiwashambulia kwa kasi kwa kuwafuata ni rahisi kufanya makosa na kusababisha penalty au adhabu karibu na eneo la hatari kitu ambacho kilifanikiwa na kuwapatia bao UD songo kupitia kwa mpira wa adhabu uliopigwa na nahodha wao Luis Jose Miquissone ambaye ndio alibeba mpango mkakati wa kuichachafya safu ya ulinzi ya Simba sc uku akipokea mipira kutoka pembeni na kuingia kwa kasi kwa kuwafuata walinzi wa kati.
  ●Ni vigumu kumiliki mpira mbele ya Simba hivyo jambo la kufanya ni kuwaacha wachezee mpira kwenye eneo lao hadi sehemu ya kati na kuanza kukaba kwa nguvu wakianza kusogea kwenye eneo la tatu la kiwanja  jambo litakalo pelekea kupoteza pasi zao na kupora mipira kwa urahisi.
  ● Kwa ujumla njia bora ya kuwadhibiti Simba ni kucheza mpira wa nguvu na kasi muda wote huku ukiwafikia kwenye miili yao kitu ambacho kitawachanganya na kuwatoa mchezoni na kuathiri  namna  ya uchezaji wao wa nipe nikupe.
  Hayo ni baadhi ya mambo ambayo UD songo waliyagundua na kuyafanyia kazi ndio mana hata kwenye mahojiano mwalimu wao Chiquinho Conde aliweka bayana kwani waliingia wakijua nini  wanatakiwa kukifanya katika mchezo huo mgumu.
  Hayo ni baadhi ya mambo ambayo yameiangusha Simba katika hatua za awali hivyo kuna haja ya kuwa makini kwenye usajili,chaguo la kikosi,jopo zuri la kusoma ubora na udhaifu wa timu pinzani na kutoa uzito sawa kwenye kila mchezo ulio mbele ili kujiwekea mazingira mazuri ya ushindi.Kwa sasa si wakati wa kumtafuta mchawi yameshapita ni wakati wa kujipanga upya ili kurudi tena msimu ujao kwa nguvu na kasi.
  (Dominick Salamba ni mchambuzi wa soka anapatikana kupitia Akaunti yake ya instagram @dominicksalamba au namba +255713942770)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUTOLEWA MAPEMA LIGI YA MABINGWA KUNA FUNDISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top