• HABARI MPYA

    Tuesday, February 14, 2017

    FARID APANDISHWA KIKOSI CHA KWANZA TENERIFE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Farid Malik Mussa amepandishwa kikosi cha kwanza cha timu ya Deportivo Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Hispania, maarufu kama Segunda.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Farid amesema kwamba tangu wiki iliyopita ameanza kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza, ingawa ameendelea kuchukuliwa timu B kwa ajili ya mechi tu.
    “Namshukuru Mungu hatimaye nimepandishwa kikosi cha kwanza, ila nimeendelea kupelekwa timu B kwa ajili ya mechi tu. Sasa ninapambana nianze kupata nafasi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza hapa,”amesema Farid.
    Farid Mussa akiwa na mchezaji mwenzake wa kikosi cha kwanza cha Tenerife kwenye chumba cha kubadilishia nguo

    Farid alijiunga na klabu hiyo ya Santa Cruz de Tenerife, Tenerife, visiwa vya Canary Desemba mwaka jana kwa mkopo wa muda mrefu wa msimu kutoka Azam FC ya Dar es Salaam. 
    Azam FC ilimtoa kwa mkopo Farid kwenda CD Tenerife kwa makubaliano maalum baada ya winga huyo kufuzu majaribio katika klabu hiyo Aprili mwaka jana alipokwenda na Mkurugenzi wa klabu yake, Yussuf Bakhresa.
    Farid alitua Hispania kwa mara ya kwanza Aprili 21, mwaka jana baada ya kuichezea Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance mjini Tunis, Tunisia ikifungwa 3-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda 2-1 Dar es Salaam.
    Na ilimchukua wiki moja tu Farid kuwakuna kwa kipaji chake makocha wa Tenerife na kutaka kumnunua, lakini Azam ikakataa na kuamua kumtoa kwa mkopo Desemba, 2016.
    Na baada ya kutua Tenerife akapangiwa kuanza kuchezea kikosi cha U-20 ili kupata uzoefu kabla ya wiki iliyopita kupandishwa kikosi cha kwanza kinachocheza Segunda, Ligi ya pili kwa ukubwa Hispania.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FARID APANDISHWA KIKOSI CHA KWANZA TENERIFE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top