• HABARI MPYA

    Saturday, May 02, 2015

    WARAKA WA HANS POPPE KWA WAPOTOSHAJI MAMBO KUHUSU SIMBA SC…

    Zacharia Hans Poppe ameandika waraka kutolea ufafanuzi masuala mbalimbali Simba SC, ambayo anaamini yanapotoshwa kwenye vyombo vya Habari.
    “Nimesoma makala moja katika tovuti fulani (siyo BIN ZUBEIRY) na kwa mara nyingine nikasikitishwa na upungufu wa weledi wa mwandishi makala hiyo. 
    Mara nyingi nimekuwa nasema pale unapotaka kusemea jambo haswa lisilo lako, bali la mwingine basi jitahidi angalau kulifanyia utafiti wa kiasi Fulani kabla hujaaandika tu mawazo yako ambayo kwa kiwango kikubwa yanaweza kupotosha ukweli wa mambo yalivyo. 
    Ni kitu rahisi sana kuwauliza wahusika wakakupa majibu yao, ambayo hata kama hutayapenda utawajibika kuyaandika ili wasomaji wakapata maelezo ya upande wa pili. 
    Ni tovuti hiyo tu imekuwa ina mazoea ya kuandika maelezo ya upande mmoja na iko siku watapitiliza, halafu ikawabidi wajibu mbele ya sheria.
    Nitajaribu kutoa maelezo ambayo yanaweza yakatoa mwanga wa upande wa pili. Sijui wametoa wapi dhana kwamba Rage (Ismail, Mwenyekiti wa zamani wa Simba) aliinua kikosi cha pili, au cha vijana. Maana katika kipindi chake chote hakuwahi kukitengea bajeti yoyote (kikosi cha vijana) mpaka alipotoka. Kama kuna mtu anastahili sifa kwa kikundi cha vijana basi ni Kaburu (Geoffrey Nyange, Makamu wa Rais wa sasa na tangu wakati wa Rage) ambaye alisisitiza katika kila gate collection, million 3 zitengwe kwa ajili ya vijana na haya yalianzia kwenye utawala wa Dalali (Hassan, Mwenyekiti wa klabu ya Rage) na alipoingia Rage utaratibu huu ulisitishwa na ndio mwanzo wa kuporomoka kwa timu hiyo, ambayo hata hivyo Kaburu aliendelea kuisimamia kwa pesa zake binafsi akisaidiwa na wapenzi wengine kadhaa. 
    Alipojiuzulu (Kaburu) wadhifa wake (katika uongozi wa Rage) hiyo timu ikafa kabisa mpaka utawala huu mpya (chini ya Rais Evans Aveva) ambao umeianzisha tena. Kwamba Rage alikuwa na usimamizi mzuri wa pesa, sijui wanayatoa wapi hayo, maana hakuna uongozi umeacha madeni kama huo na mpaka leo uongozi huu wa sasa haujamaliza kuyalipa.
    Ubabe wa viongozi na usajili. Hii ni mara ya nne nadhani wanaandika bila ya kumtaja huyo kiongozi anayesajili kwa fikra zake binafsi. Hivi kama kuna ukweli wowote juu ya jambo hilo, wanashindwa nini kumtaja huyo kiongozi, wakisema wazi kuwa kiongozi huyo Fulani alimsajili mchezaji Fulani bila ya kufuata utaratibu uliowekwa na club. 
    Ni wazi wanashindwa kufanya hivyo kwa sababu huo ni uongo ambao hawawezi kuuthibitisha na sijui wana nia gani ya kuuendeleza na wakiurudia tena, wasilalamike na hatua zitakazofuata.
    Aveva kafukuza wanachama. Kwa mara nyingine wanadhihirisha uelewa wao mdogo na katiba za TFF na za vilabu ambazo lazima ziendane na katiba ya FIFA. Katiba zote hizo zinatamka wazi kuwa mwanachama yeyote atakayepaleka masuala ya mpira mahakamani basi ataondolewa kujishughulisha na mambo ya mpira mpaka ama kesi iishe au ifutwe. 
    Aveva hawezi akaamua kuwafukuza wanachama kwa utashi wake tu bila sababu. Baada ya wale wanachama kwenda mahakamani, kamati ya utendaji iliwasimamisha na suala lao likapelekwa kwenye mkutano mkuu ambao kwa kauli moja ukawafukuza kwa mujibu wa katiba. 
    Kumshutumu Aveva kuwa kawafukuza hao ni kukosa weledi.
    Mara nyingi pia inaandikwa sana kuhusu vyanzo vya mapato vya club hususan Simba ambayo angalau licha ya viingilio wana majengo ambayo huwaingizia kiasi cha tshs 181m kwa mwaka. Sijawahi kuona ikizungumziwa Yanga ambayo ukiondoa gate collection hawana kabisa chanzo kingine zaidi ya kuomba kwa mtu mmoja ambaye siku akiacha itakuwa tabu sana kama alivyosema kiongozi wao wa zamani Abbas Tarimba hivi karibuni. 
    Hapa karibuni tumesema kuwa kipato cha viwanjani kimepungua sana kwa sababu ya TV kuonesha michezo yetu live, lakini kwa sababu zao wenyewe wamerukia hili kwa kusema sio hivyo, ila mgawanyiko ndio umepelekea wengi wasiende mpirani. 
    Walioenda mahakamani ni 64 tu na hata kama wana wanaowaunga mkono hawawezi kuzidi elfu moja ambao hata wasipokuja wasingeathiri kipato kwa kiwango hicho. Kwa taarifa yao, waendaji mpirani sio wanachama pekee ila zaidi ni washabiki na hao huwa hawajihusishi na migogoro. 
    Mara nyingi wanachama ndio wale wenye vikundi vya ushangiliaji na hulipiwa tiketi na club kwa hiyo kipato cha milangoni kutoka kwa wanachama ni kidogo sana. Ukifuatilia wenzetu huko majuu siku zote TV hazirushi matangazo live kwenye ule mji unapochezewa mpira huo na hurushwa baadaye baada ya mechi kumalizika. Ni rahisi kufuatilia hili.
    Mwisho ni hoja yao kuwa wachezaji kulipwa tofauti. Hii imeniacha hoi kabisa na sidhani kama nitalisemea sana, ila tu siku Rooney, Messi na Ronaldo watakavyolipwa sawa na wengine na sisi tutajitahidi kufanya hivyo. Mambo mengine hayaitaji utaalamu ni akili za kuzaliwa tu. Wakatabahu,”.

    (Makala hii imeandikwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe kutolea ufafanuzi masuala mbalimbali ya klabu hiyo) 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WARAKA WA HANS POPPE KWA WAPOTOSHAJI MAMBO KUHUSU SIMBA SC… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top