• HABARI MPYA

    Saturday, May 02, 2015

    PLUIJM: HAKUNA KINACHOSHINDIKANA, YANGA TUMEFUATA USHINDI TUNISIA NA TUTAPAMBANA

    Na Prince Akbar, SOUSSE
    KOCHA wa Yanga SC, Han van der Pluijm amesema kwamba hakuna kinachoshindikana na leo ataingiza kikosi chake Uwanja wa Olimpiki mjini Sousse kutafuta nafasi ya kusonga mbele Kombe la Shirikisho Afrika.
    Yanga watakuwa wageni wa Etoile du Sahel Uwanja wa Olimpiki, Sousse katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika.
    Na Yanga SC wanahitaji ushindi wa ugenini au sare ya zaidi ya mabao 2-2 ili kusonga mbele, baada ya awali kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani Dar es Salaam.
    Sare nyingine ya 1-1 itaurefusha mchezo huo hadi kwenye dakika 120 ambako pia mshindi asipopatikana mikwaju ya penalti itatumika.
    Kocha wa zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana, Pluijm amesema kwamba matokeo ya Dar es Salaam hayakuwa mazuri, lakini watapambana kutafuta nafasi ya kusonga mbele wakiwa ugenini.
    “Matokeo ya nyumbani hayakuwa mazuri. Lakini hakuna kinachoshindikana. Tumekuja hapa kupambana kutafuta nafasi ya kusonga mbele. Na tumekuja na mbinu tofauti. Tumejifunza kutokana na makosa ya mchezo wa kwanza,”amesema Pluijm.
    Hakuna kinachondikana; Kocha wa Yanga SC, Hans van der Pluijm amesema watapigania ushindi wa ugenini leo wasonge mbele

    Mholanzi huyo anafurahi vijana wake wako vizuri kuelekea mchezo huo na timu imeandaliwa vizuri kwa ujumla.
    “Wachezaji wamepatiwa vifaa madhubuti kwa ajili ya baridi. Kuna baridi hapa, lakini hatuna wasiwasi watacheza vizuri kwa sababu kila kitu kipo vizuri,”amesema Pluijm.
    Mshambuliaji Mliberia wa Yanga SC, Kpah Sherman ambaye ataanza leo anaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, ambayo ilikosa mtu wa kuwapa misukosuko mabeki wa Etoile katika mchezo wa kwanza Dar ves Salaam.
    Kiungo hodari mchezeshaji, Haruna Niyonzima atakosekana kwa sababu ameachwa nyumbani kutokana na kuwa mgonjwa, lakini habari njema ni kwamba kiungo mwingine tegemeo, Salum Telela yuko vizuri na anaanza leo. 
    Hali ya Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ si ya kuridhisha bado na anaweza kuanzia benchi leo, katikati wakicheza pamoja Mbuyu Twite na Kevin Yondan.
    Langoni ataanza Ally Mustafa ‘Barthez’, kulia Juma Abdul, kushoto Oscar Joshua, wakati Salum Telela na Said Juma ‘Makapu’ wote watakuwa viungo wa ulinzi.
    Mrisho Ngassa leo atatumika kama kiungo mchezeshaji, wakati safu ya ushambuliaji itaundwa na Sherman, Simon Msuva na Amissi Tambwe.
    Injini ya timu; Mrisho Ngassa kushoto anatarajiwa kuiongoza timu leo, wakati Juma Abdul kulia ataanza beki ya kushoto

    Kwenye benchi watakuwepo Deo Munishi ‘Dida’, Edward Charles, Rajab Zahir, Cannavaro, Pato Ngonyani, Andrey Coutinho, Nizar Kalfan, Hussein Javu na Jerry Tegete.
    Etoile wamekuwa wakiendelea na maandalizi yao nyumbani wiki yote hii kwa matumaini makubwa ya kushinda mechi hiyo.
    Kikosi cha Yanga SC kinatarajiwa kuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondan, Mbuyu Twite, Saidi Makapu, Simon Msuva, Salum Telela, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa na Kpah Sherman.
    Etoile su Sahel; Aymen Mathlouthi, Hamdi Nagguez, Ammar Jemal, Rami Bedoui, Zied Boughattas, Franck Kom, Mohamed Amine Ben Amor, Alkhali Bangoura, Marouene Tej, Youssef Mouihbi, Baghdad Bounedjah.
    Katika benchi watakuwepo; Aymen Ben Ayoub
    Ghazi Abderrazzak, Saddam Ben Aziza, Mohamed Nidhal Saied, Mehdi Saada, Alaya Brigui, Hamza Lahmar na Sofiane Moussa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PLUIJM: HAKUNA KINACHOSHINDIKANA, YANGA TUMEFUATA USHINDI TUNISIA NA TUTAPAMBANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top