• HABARI MPYA

  Monday, January 12, 2015

  PLUIJM AANZA ‘KUZIBA VIRAKA’ YANGA SC

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm amesema kwamba leo wanaanza mazoezi  na kikubwa anachotarajia kukifanyia kazi ni mapungufu aliyoyaona katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini hapa jana, Pluijm amesema kwamba Yanga imebadilika mno kwa kipindi kifupi tu tangu arejee kazini na ataendelea kufanya kazi nzuri kuimarisha zaidi timu.
  Yanga SC ilitolewa katika Robo Fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa kufungwa 1-0 na JKU, ikitoka kushinda mechi zote za kundi lake, A 4-0 mara mbili dhidi ya Taifa Jang’ombe na Polisi na 1-0 dhidi ya Shaba.
  Kocha wa Yanga SC, Hans van der Pluijm kulia amesema atafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika Kombe la Mapinduzi

  Pluijm amesema kwamba timu ilicheza vizuri katika mashindano hayo na hata siku wanatolewa na JKU walicheza vizuri pia na kupata bao lililofungwa na Mliberia Kpah Sherman, lakini refa akakataa huku washambuliaji wake wakipoteza nafasi nyingi nzuri walizotengeneza.
  “Bado picha ya ile mechi inaniijia kila ninapokaa, nakumbuka refa alivyokataa lile bao halali, nakumbuka nafasi nyingi tulizopteza, nakumbuka kosa moja tu, lilivyowapa ushindi wapinzani,”amesema.
  Lakini Pluijm amesema anakutana tena na vijana wake leo, kuanza maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting mwishoni mwa wiki na atafanyia kazi mapungufu.
  “Nilizungumza na washambuliaji wangu wote, nikawaambia umuhimu wa kutumia nafasi na kushirikiana. Wamenielewa, natarajia mabadiliko kutoka kwao. Lakini pia, kama timu kuna mapungufu nimeyaona, nitayafanyia kazi,”amesema.
  Pluijm amesema anataka kufanya kazi nzuri Yanga SC baada ya uongozi wa klabu hiyo kuonyesha heshima kubwa kwake, ikiwemo kumpatia makazi bora.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PLUIJM AANZA ‘KUZIBA VIRAKA’ YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top