• HABARI MPYA

  Sunday, January 11, 2015

  MWISHOWE WASHAMBULIAJI YANGA WATAANZA KUSHIKANA UCHAWI!

  MSIMU wa 2009/2010, safu ya ushambuliaji ya Yanga SC ilikuwa inaundwa na akina Ben Mwalala, Boniphace Ambani wote Wakenya na wazalendo Jerry Tegete na Mrisho Ngassa.
  Hii ilikuwa fowadi kali sana na tishio katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mashabiki wa Yanga SC waliifurahia timu yao.
  Msimu uliofuata ikaanza kubomoka, Ambani na Mwalala waliondoka, Ngassa alihamia Azam akabaki Tegete peke yake, ambaye alibadilishiwa washambuliaji tofauti katika kipindi chote hicho.
  Alipita hadi Mzambia Davies Mwape, lakini Yanga SC haikuwahi tena kuwa na fowadi kali kama ile ya 2009/2010.
  Msimu huu tena, imetokea bahati kubwa Yanga SC imepata washambuliaji bora wa kutosha, Mliberia Kpah Sherman, Mrundi Amisi Tambwe na wazalendo Ngassa, Hussein Javu na Danny Mrwanda.  
  Bado viungo washambuliaji wanaongeza chachu ya makali ya fowadi ya timu hiyo Mbrazil Andrey Coutinho na mzalendo Simon Msuva.
  Tuweke kando mapenzi na ushabiki, Yanga SC hivi sasa ina fowadi kali, ambayo kama makocha wa timu hiyo wataweza kuiunganisha vyema, inaweza kuizidi hata ile ya 2009/2010.
  Tuseme rasmi fowadi hiyo ilianza kucheza pamoja katika Kombe la Mapinduzi ambako katika mechi nne walifunga mabao tisa, Msuva manne, Coutinho matatu na mawili Sherman.
  Yanga SC ilitolewa katika Robo Fainali na JKU kwa kufungwa 1-0, siku ambayo refa alikataa bao moja la Sherman na pia washambuliaji wa timu hiyo wakakosa mabao mengi ya wazi.
  Yanga SC pia walikosa mabao mengi katika mchezo uliotangulia dhidi ya Shaba kabla ya Coutinho kufunga bao pekee la ushindi dakika ya 86.
  Hata katika mechi ambazo Yanga SC walishinda 4-0 mara mbili dhidi ya Polisi na Taifa Jang’ombe, bado walikosa mabao mengi ya wazi.
  Kwa kuwa wana fowadi nzuri, Yanga wanatengeneza mashambulizi mengi, lakini utumiaji wa nafasi limekuwa tatizo katika mechi mbili mfululizo zilizopita.
  Kuna hali ya kila mchezaji kutaka kufunga na Msuva na Coutinho ambao kama mawinga wanategemewa sana kuwa wapishi, nao wanapenda kufunga wenyewe.
  Yaani washambuliaji wa Yanga SC pamoja na ubora wao, wanacheza bila mipango wala malengo, ndiyo maana wanapoteza nguvu zao bure uwanjani.
  Ile fowadi ya mwaka 2009, mfungaji wao namba moja alikuwa Ambani, kwa hivyo wote Ngassa, Mwalala na Tegete walicheza wakifikiria kumlisha mipira Mkenya huyo afunge na akawa mfungaji bora wa Ligi Kuu, Yanga ikiwa bingwa.
  Haiwezekani Yanga kila mchezaji atake kufunga, lazima wacheze kwa uelewano, maarifa na mipango kwa maslahi ya timu yao.
  Vinginevyo kila siku watakuwa wanapamiana pale mbele, mwisho wa siku wapinzani wanashinda mechi. Uchu wa kufunga si mbaya, lakini lazima mchezaji aweke mbele maslahi ya timu kwanza.
  Wote Tambwe, Sherman, Ngassa na Mrwanda wamekwishakuwa wafungaji bora wa mashindano na Ligi mbalimbali walizocheza- hakuna ubishi ni washambuliaji na wafungaji wazuri.
  Lakini, kwa kukutana pamoja Yanga SC, lazima wabadilishe fikra zao na wakubaliane kumfanya mmoja wao ndiye awe mlengwa wa kwanza wa kufunga.
  Wajipange wakati wa kushambulia nani apewe pasi ya mwisho, na akipga mpira ukarudishwa wajipange vipi kumalizia. Naamini, washambuliaji wa Yanga SC wakicheza kwa mipango watafanikiwa sana.   
  Bila ya washambuliaji Yanga SC kukaa chini na kutafakari namna ya kucheza kwa uelewano na ushirikiano kwa maslahi ya timu yao, wataendelea kupamiana kwenye lango la wapinzani wakikosa mabao ya wazi na mwisho wa siku, wataanza kushikana uchawi, wanalogana. Alamsiki.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MWISHOWE WASHAMBULIAJI YANGA WATAANZA KUSHIKANA UCHAWI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top