• HABARI MPYA

  Thursday, January 08, 2015

  MTIBWA SUGAR YAING’OA AZAM FC KWA MATUTA KOMBE LA MAPINDUZI

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  AZAM FC imeaga mashindano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar kwa penalti 7-6 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Shujaa wa Mtibwa Sugar alikuwa ni kipa Said Mohammed Kasarama aliyecheza penalti mbili za Kipre Herman Tchetche na kipa mwenzake Aishi Manula.
  Penalti za Mtibwa zilifungwa na Shaaban Nditi, Henry Joseph, David Luhende, Vincent Barnabas, Mussa Nampaka, Muzamil Yassin na Said Mkopi, wakati ya Ame Ally ilipanguliwa na kipa Manula.
  Kwa upande wa Azam FC, waliofunga penalti ni Aggrey Morris, Didier Kavumbangu, Erasto Nyoni, Brian Majwega, John Bocco na Serge Wawa. 
  Wachezaji wa Mtibwa Sugar wakiwa wamemuinua juu kipa Said Mohammed baada ya kucheza penalti mbili na kuivusha timu hiyo Nusu Fainali Kombe la Mapinduzi  

  Dakika 45 za kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa hazijafungana na kipindi cha pili, Shomary Ally alianza kuifungia Mtibwa Sugar dakika ya 
  63 akimalizia pasi ya Mussa Hassan Mgosi, kabla ya Kipre Tchetche kuisawazishia Azam FC dakika ya 89 akimalizia krosi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
  Kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu na mchezo ulikuwa wa kukamiana, wachezaji hawakuthubutu kupeana nafasi.
  Hata hivyo, uimara wa fiziki ya wachezaji wa pande zote mbili ulisababisha yasitokee majeruhi katika dakika 45 za kwanza, licha ya wachezaji kugongana kiasi cha kutosha.
  Ibrahim Rajab Jeba aliishia dakika 41 tu kabla ya kocha Mecky Mexime kumuingiza Mussa Nampaka badala yake kuimarisha safu ya kiungo, ambayo awali Azam FC waliitawala.
  Kiungo wa Azam FC, Himid Mao akimlamba chenga kiungo wa Mtibwa Henry Joseph kushoto
  Beki wa Mtibwa Sugar, Said Mkopi akiwa ameruka juu kuondosha mpira katika hatari langoni mwao

  Mtibwa Sugar walikianza vizuri kipindi cha pili na kukosa mabao mawili ya wazi licha ya kupata moja, wakati Azam FC ilichangamka baada ya kuingia kwa Sure Boy na Kipre Tchetche kwenda kuchukua nafasi za Frank Domayo na Himid Mao.
  Katika Robo Fainali ya Kwanza, KCCA ya Uganda ilivuliwa ubingwa na Polisi ya hapa kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 Uwanja wa Amaan, Zanzibar.  
  Polisi sasa itamenyana na Simba SC katika Nusu Fainali keshokutwa Uwanja wa Amaan, ambayo jana iliitoa Taifa ya Jang’ombe kwa mabao 4-0.
  Robo Fainali ya mwisho inawadia hivi sasa kati ya Yanga SC JKU na mshindi wa mchezo huo, ndiye atakutana na Mtibwa Sugar atika Nusu Fainali Jumamosi. 
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Serge Wawa, Mudathir Yahya, Himid Mao/Kipre Tchetche dk62, Frank Domayo/Salum Abubakar dk63, John Bocco, Didier Kavumbangu na Brian Majwega.
  Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Said Mkopo, David Luhende, Salim Mbonde, Andrew Vincent, Henry Joseph, Shomary Ally/Shaaban Nditi dk90, Muzamil Yassin, Ame Ally, Ibrahim Rajab/Mussa Nampaka dk40 na Mussa Hassan Mgosi/Vincent Barnabas dk78.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR YAING’OA AZAM FC KWA MATUTA KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top