• HABARI MPYA

  Saturday, January 10, 2015

  MESSI AIPELEKA SIMBA SC FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI, ITAKUTANA NA MTIBWA SUGAR

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  SIMBA SC imetinga Fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa mwaka wa pili mfululizo, baada ya usiku huu kuifunga Polisi ya hapa, bao 1-0 Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Simba SC sasa itamenyana na Mtibwa Sugar katika Fainali ya timu za Bara tupu Jumanne Uwanja wa Amaan. Mtibwa imeitoa JKU pia ya Zanzibar kwa penalti 4-3 baada ya sare ya 0-0 jioni ya leo.
  Shujaa wa Wekundu wa Msimbazi leo alikuwa ni winga Ramadhani Yahya Singano ‘Messi’ aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 26 kwa shuti la mpira wa adhabu, baada ya Simon Sserunkuma kuchezewa rafu pembezoni mwa Uwanja.
  Pamoja na Simba SC kutoka inaongoza 1-0 hadi mapumziko, lakini timu hizo zilishambuliana kwa zamu kipindi cha kwanza.
  Nahodha wa Simba SC, Hassan Isihaka (juu) akimpongeza winga Ramadhani Singano 'Messi' baada ya kuifungia timu hiyo bao pekee usiku huu Uwanja wa Amaan
  Mshambuliaji wa Simba SC, Simon Sserunkuma akimruka beki wa Polisi nje kidogo ya boksi  

  Kipindi cha pili, Simba SC walirudi kwa kasi na dakika ya 46 Dan Sserunkuma alikosa bao la wazi akiwa amebaki yeye na kipa baada ya kutanguliziwa pasi nzuri na Said Ndemla aliyeibuka nyota wa mchezo.
  Ibrahim Hajibu naye aliyetokea benchi kipindi cha pili kumbadili Elias Maguri alikosa bao la wazi dakika ya 48 baada ya pasi nzuri ya Jonas Mkude, alipotaka kumlamba chenga Nasir Abdallah, lakini kipa huyo akafanikiwa kuudaka mpira.
  Simba SC iliendelea kung’ara mchezoni na kupoteza nafasi zaidi za kufunga mabao, kutokana na umakini haba wa washambuliaji wake- sifa ziwaendee viungo Mkude na Ndemla kwa kazi nzuri leo.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’Shaaban Kisiga ‘Malone’ dk64, Said Ndemla, Elias Maguri/Ibrahim Hajibu dk46, Dan Sserunkuma na Simon Sserunkuma/Awadh Juma dk79.
  Polisi; Nasir Suleiman, Juma Ally, Suleiman Ali, Mohammed Hajji, Abdallah Mwalimu, Mohammed Ally, Adam Juma, Daniel Justin, Ali Khalid/Amir Hamad dk84, Frank Hamisi, Abdallah Omar/Mohammed Seif dk57 na Samir Vincent/Steven Emanuel dk58.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MESSI AIPELEKA SIMBA SC FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI, ITAKUTANA NA MTIBWA SUGAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top