• HABARI MPYA

  Saturday, January 17, 2015

  MASTRAIKA YANGA BUTU, SARE 0-0 NA RUVU SHOOTING

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  UBUTU wa safu ya ushambuliaji ya Yanga SC kwa mara nyingine umeendelea kuitesa timu hiyo, baada ya jioni ya leo kulazimishwa sare ya bila kufungana na Ruvu Shooting ya Pwani katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
  Washambuliaji wa Yanga SC, Kpah Sherman, Amisi Tambwe, Simon Msuva na Andrey Coutinho wote walikosa mabao ya wazi leo. 
  Refa Mohammed Theofil wa Morogoro aliyesaidiwa na Michael Mkongwa wa Njombe na Yussuf Sekile wa Ruvuma, alilazimika mara kadhaa kuamulia ugomvi baina ya wachezaji wa timu zote mbili.
  Mpira ukigonga mwamba kwenye lango la Ruvu Shooting, kufuatia kona ya Andrey Coitinho (hayupo pichani)  kuunganishwa kwa kichwa na Simon Msuva 

  Winga wa Yanga SC, Simon Msuva akijaribu kumtoka beki wa Ruvu Hamisi Maulid
  Ilikuwa ni vita iliyoanza mapema baina ya Tambwe na beki George Michael wa Ruvu- na badaye ikawa vita ya washambuliaji wote wa Yanga dhidi ya mabeki wote wa timu hiyo ya jeshi.
  Winga Simon Msuva ndiye aliyewasikitisha zaidi wana Yanga kwa kupoteza nafasi tatu za wazi za kufunga dakika za 10, 13 na 38 na Mbrazil Andrey Coutinho alipoteza nafasi mbili, huku nyingine ikipotezwa na Amisi Tambwe. 
  Kipindi cha pili, pamoja na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm kubadilisha washambuliaji, akiwatoa Coutinho, Msuva na Tambwe ambao nafasi zao zilichukuliwa na Hussein Javu, Dan Mrwanda na Mrisho Ngassa, lakini bado haikuwa siku ya Yanga SC.
  Na ilibaki kidogo Yanga wapoteze mchezo kama si jitihada za beki Rajab Zahir kuokoa mpira uliokuwa unaelekea nyavuni kufuatia kipa wake, Ally Mustafa ‘Barthez’ kulambwa chenga na Abdulrahman Mussa dakika ya 81.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Edward Charles, Rajab Zahir, Kevin Yondan, Salum Telela, Simon Msuva/Danny Mrwanda dk65, Haruna Niyonzima, Kpah Sherman, Amisi Tambwe/Mrisho Ngassa dk83 na Andrey Coutinho/Hussein Javu dk72.
  Ruvu Shooting; Abdallah Rashid, Michael Aidan, Said Madega, George Osey, Hamisi Kasanga, Salvatory Ntebe, Juma Nade, Hamisi Maulid, Yahya Tumbo/Baraka Mtuwi dk54, Mwita John/Jerome Lambele dk65 na Ayoub Kitala/Abdulrahman Mussa dk42. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MASTRAIKA YANGA BUTU, SARE 0-0 NA RUVU SHOOTING Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top