• HABARI MPYA

  Thursday, January 08, 2015

  MANYIKA MDOGO AJIWEKEA REKODI BABU KUBWA, MECHI TATU MFULULIZO BILA KUFUNGWA

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  KIPA kinda wa Simba SC, kwa mara ya kwanza jana ametimiza mechi tatu mfululizo za kudaka bila kufungwa hata bao moja.
  Mtoto huyo wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Yanga, Manyika Peter alikuwepo langoni usiku wa jana Uwanja wa Amaan, Zanzibar wakati Simba SC ikiilaza 4-0 Taifa ya Jang’ombe.
  Huo ulikuwa mchezo wa tatu mfululizo Manyika Jr. anadaka bila kufungwa katika mashindano haya, baada ya awali kuwakatalia Mafunzo na JKU mechi za Kundi C, Simba ikishinda 1-0 kila mchezo.

  Peter Manyika wa tatu kutoka kushoto katika kikosi cha Simba SC jana kilichoibuka na ushindi wa 4-0 dhidi ya Taifa Jang'ombe

  REKODI YA MANYIKA MDOGO SIMBA SC 

  Simba SC 0-0 Orlando Pirates (kirafiki aliingia dk43 hakufungwa, Afrika Kusini) 
  Simba SC 2-4 Orlando Pirates (Kirafiki, alifungwa nne Afrika Kusini) 
  Simba SC 0-2 Bidvest Wits (Kirafiki, alifungwa mbili Afrika Kusini) 
  Simba SC 0-0 Yanga SC (Ligi Kuu, hakufungwa)
  Simba SC 1-1 Prisons (Ligi Kuu, alifungwa moja)
  Simba SC 1-1 Mtibwa Sugar (Ligi Kuu, aliokoa penalti, akafungwa moja)
  Simba SC 0-0 Express (Kirafiki Dar es Salaam, hakufungwa) 
  Simba SC 0-1 Mtibwa Sugar (Kombe la Mapinduzi, Zanzibar alifungwa moja)
  Simba SC 1-0 Mafunzo (Kombe la Mapinduzi, Zanzibar hakufungwa)
  Simba SC 1-0 JKU (Kombe la Mapinduzi, hakufungwa)
  Simba SC 4-0 Taifa Jang’ombe (Robo Fainali Kombe la Mapinduzi, hakufungwa)
  Simba SC iliyaanza vibaya mashindano ya mwaka huu, baada ya kufungwa 1-0 na Mtibwa Sugar katika mchezo wa ufunguzi, kabla ya kuzinduka na kushinda mara mbili mfululizo hivyo kutinga Robo Fainali.
  Kwa ujumla, Manyika aliyesajiliwa msimu huu kwa ajili ya timu ya vijana ya klabu hiyo na kupandishwa timu ya wakubwa kukomazwa, amekwishaidakia Simba SC katika mechi 11 na kufungwa mabao tisa.
  Kipa huyo wa tatu, alianza kudaka nchini Afrika Kusini Oktoba mwaka jana kufuatia makipa wote wa klabu hiyo, Ivo Mapunda na Msaidizi wake, Hussein Sharrif ‘Casillas’ kuumia. 
  Alidaka wakati Simba SC ikitoka sare ya 0-0 na Orlando Pirates akiingia dakika ya 43 kumpokea Casillas aliyeumia na akadaka tena Simba SC ikifungwa 4-2 na Bidvest Wits na dhidi ya Jomo Cossmos wakifungwa 2-0 ziara ya Afrika Kusini.
  Kutoka hapo akaidakia Simba SC ikitoa sare ya 0-0 na mahasimu Yanga SC katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Akadaka mechi mbili mfululizo Simba SC ikitoa sare ya 1-1 zote na Prisons mjini Mbeya na
  Mtibwa Sugar mjini Morogoro zote za Ligi Kuu.
  Akadaka mchezo wa kirafiki Simba SC ikitoka sare ya 0-0 na Express, kabla ya kuingia kwenye Kombe la Mapinduzi na kufungwa bao moja katika mechi nne hadi sasa.
  Baada ya Simba SC kwenda Robo Fainali, sasa inasuburi mshindi kati ya mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi, KCCA ya Uganda na Polisi ya Zanzibar ikutane naye katika Nusu Fainali Jumamosi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MANYIKA MDOGO AJIWEKEA REKODI BABU KUBWA, MECHI TATU MFULULIZO BILA KUFUNGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top