• HABARI MPYA

  Friday, January 16, 2015

  KOMBE LA TAIFA YAINGIA RAUNDI YA PILI

  Na Boniface Wambura, DAR ES SALAAM
  MICHUANO ya Kombe la Taifa kwa Wanawake inaingia raundi ya pili kesho (Januari 17 mwaka huu) kwa mechi za kwanza za raundi hiyo zitakazochezwa katika miji ya Bukoba, Arusha, Mlandizi, Dar es Salaam na Katavi.
  Jijini Dar es Salaam kutakuwa na mechi mbili ambapo mkoa wa kisoka wa Ilala utacheza na Mtwara kwenye Uwanja wa Karume, wakati Uwanja wa Chuo cha Bandari uliopo Tandika utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Temeke na Dodoma.
  Mechi nyingine za michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Proin zitakuwa kati ya Kagera na Mwanza itakayochezwa mjini Bukoba, Arusha na Tanga (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid), Pwani na Kinondoni (Uwanja Mabatini, Mlandizi), na Katavi na Mbeya zitakazoonesha kazi kwenye Uwanja wa Azimio.

  Nazo Ruvuma na Iringa zitacheza Januari 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Majimaji. Mechi hiyo itachezwa tarehe hiyo ili kusubiri matokeo ya mechi ya marudiano kati ya Shinyanga na Simiyu.
  Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Januari 15 mwaka huu) kupitia ripoti ya mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza kati ya Shinyanga na Simiyu ambayo ilivunjwa na mwamuzi katika daika ya 70.
  Baada ya kupitia ripoti, Kamati imebaini kuwa licha ya vurugu alizofanyiwa mwamuzi, bado mechi hiyo ingeweza kuendelea kwa kuchezeshwa na mwamuzi wa akiba kwa vile usalama ulikuwepo baada ya yeye kupigwa.
  Pia Kamati imeagiza Katiba wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Sologo aliyeripotiwa kumpiga mwamuzi suala lake lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa hatua zaidi, wakati Kocha wa Simiyu, Emmanuel Babu ambaye naye alishiriki kumpiga mwamuzi amesimamishwa wakati akisubiri kuchukua hatua zaidi.
  Kamishna wa mechi hiyo Idd Mbwana, na mwamuzi Joseph Pombe wamefungiwa kwa miaka miwili.
  Mechi kati ya Shinyanga na Simiyu itamaliziwa dakika kumi zilizobaki kesho (Januari 17 mwaka huu) mjini Shinyanga. Kila chama cha mkoa kitabeba gharama zake katika uendeshaji wa mechi hiyo ambayo mwenyeji ni Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA).
  Timu itakayosonga mbele baada ya mechi hiyo itacheza mechi ya kwanza ya raundi ya pili ugenini Januari 19 mwaka huu dhidi ya Kigoma. Mechi za marudiano za raundi ya pili zitachezwa kati ya Januari 21 na 22 mwaka huu.
  Hatua ya robo fainali hadi fainali ambayo mechi zake zitachezewa jijini Dar es Salaam itaanza Januari 26 mwaka huu. Fainali itachezwa Februari Mosi mwaka huu.
  Vilevile Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF imemfungia kwa miaka miwili Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kwa kushindwa kuingiza timu yake uwanjani kwenye mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza dhidi ya Dodoma iliyokuwa ichezwe kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOMBE LA TAIFA YAINGIA RAUNDI YA PILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top