• HABARI MPYA

  Tuesday, January 13, 2015

  GORAN KOPUNOVIC ATAIPIKU REKODI YA PHIRI LEO?

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  MSERBIA Goran Kopunovic ataiongoza Simba SC katika mechi ya tano leo ikimenyana na Mtibwa Sugar Fainali ya Kombe la Mapinduzi, Uwanja wa Amaan, Zanzibar akiwa ameshinda zote nne za awali.
  Iwapo atafanikiwa kuiwezesha Simba SC kushinda mchezo huo, Goran atakuwa ameipiku rekodi ya kocha aliyemtangulia, Mzambia Patrick Phiri aliyeshinda mechi nne mfululizo za awali.
  Phiri aliyeanza kazi Agosti mwaka jana Simba SC akimpokea Mcroatia, Zdravko Logarusic alishinda mechi nne mfululizo za kirafiki mwanzoni, kabla ya kufungwa mechi ya tano na tangu hapo, timu ikawa inasuasua hadi akafukuzwa kazi Desemba mwishoni.
  Kocha Goran Kopunovic (kushoto) akiwa na Msaidizi wake Suleman Matola (kulia) katika mazoezi ya jana Uwanja wa Chukwani

  REKODI YA GORAN KOPUNOVIC SIMBA SC; 

  Simba SC 1-0 Mafunzo (Kombe la Mapinduzi)
  Simba SC 1-0 JKU (Kombe la Mapinduzi)
  Simba SC 4-0 Taifa Jang’ombe (Robo Fainali Kombe la Mapinduzi)
  Simba SC 1-0  Polisi (Nusu Fainali Kombe la Mapinduzi)
  Phiri alishinda 2-1 dhidi ya Kilimani City, 2-0 dhidi ya Mafunzo na 5-0 dhidi ya KMKM, zote za kirafiki Uwanja wa Amaan, Zanziabr na baadaye 3-0 dhidi ya Gor Mahia kirafiki pia, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Hata hivyo, katika mchezo wa tano ambao ulikuwa wa kirafiki pia, Phiri alifungwa 1-0 na URA Dar es Salaam na huo ukawa mwisho wa rekodi yake ya wimbi la ushindi wa mechi nne.
  Goran aliyeanza kazi Janauri, pia mechi za mwanzo amecheza Zanzibar na hadi sasa ameshinda nne mfululizo dhidi ya Mafunzo 1-0, JKU 1-0, Taifa Jang’ombe 4-0 na Polisi 1-0 pia, zote za Kombe la Mapinduzi.
  Simba SC ilipoteza mechi ya kwanza ya mashindano kwa kufungwa 1-0 na Mtibwa Sugar, lakini wakati huo Kopunovic alikuwa hajaanza kazi na timu ilikuwa chini ya kocha Msaidizi, Suleiman Matola. 
  Ikumbukwe, Phiri hakuweza kuvunja rekodi ya Logarusic, aliyeshinda mechi tano mfululizo tangu arithi mikoba ya Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ Desemba mwaka juzi.
  Kopunovic akiwaandaa vijana kwa ajili ya kushinda mechi ya tano leo

  Loga alizifunga KMKM 3-1 kirafiki, Yanga SC 3-1 pia Nani Mtani Jembe, KMKM tena 1-0 Kombe la Mapinduzi, Chuoni 2-0, URA 2-0 kabla ya kukwama kwa KCC katika Fainali Kombe la Mapinduzi akifungwa 1-0.
  Hata hivyo, kwa miaka ya karibuni, chini ya makocha tofauti, Simba SC imekuwa tishio katika mashindano ya vikombe vidogo vidogo, lakini inapowadia Ligi Kuu makali yao hupotea.
  Maana yake, hata kama Goran atafanikiwa kubeba Kombe la Mapinduzi, bado mtihani wake mkubwa ni kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Ataanza Ligi Kuu kwa kuiongoza Simba SC katika mchezo wa ugenini dhidi ya Ndanda FC Janauri 17, Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
  Baada ya hapo ataifuata Mgambo Shooting mjini Tanga katikati ya wiki na mwishoni mwa wiki,  Januari 24 atakutana na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Simba SC kabla ya kumalizia kiporo katikati ya wiki na Mbeya City Dar es Salaam.
  Wazi mechi hizo nne ndiyo zitatoa taswira ya mustakabali wa Mserbia huyo Msimbazi, ambaye amepewa Mkataba wa awali wa majaribio wa miezi sita.
  Simba SC imekubaliana na Kopunovic, iwapo atafanya vizuri katika sehemu iliyobaki ya msimu, ataongezewa Mkataba wa miaka miwili, lakini akichemsha ataonyeshwa mlango waliotokea Mserbia mwenzake Milovan Cirkovic, Mfaransa Patrick Liewig, mzalendo Kibadeni, Logarusic na Phiri ndani ya miaka miwili iliyopita.
  Phiri aliondoka Simba SC baada ya kuiongoza katika mechi nane za Ligi Kuu, akishinda moja, kufungwa moja na sare sita, hivyo kukusanya pointi tisa, ikizidiwa pointi saba na Mtibwa Sugar walio kileleni. 

  REKODI YA PATRICK PHIRI SIMBA SC

  Simba SC 2-1 Kilimani City (Kirafiki Zanzibar)
  Simba SC 2-0 Mafunzo (Kirafiki Zanzibar)
  Simba SC 5-0 KMKM (Kirafiki, Zanzibar)
  Simba SC 3-0 Gor Mahia (Kirafiki, Dar es Salaam)
  Simba SC 0-1 URA (Kirafiki, Dar es Salaam)
  Simba SC 0-0 Ndanda (Kirafiki Mtwara)
  Simba SC 2-2 Coastal Union (Ligi Kuu)
  Simba SC 1-1 Polisi Moro (Ligi Kuu)
  Simba SC 1-1 Stand United (Ligi Kuu)
  Simba SC 0-0 Orlando Pirates (Kirafiki, Afrika Kusini) 
  Simba SC 2-4 Bidvest Wits (Kirafiki, Afrika Kusini) 
  Simba SC 0-2 Jomo Cosmos (Kirafiki, Afrika Kusini) 
  Simba SC 0-0 Yanga SC (Ligi Kuu)
  Simba SC 1-1 Prisons (Ligi Kuu)
  Simba SC 1-1 Mtibwa Sugar (Ligi Kuu)
  Simba SC 1-0 Ruvu Shooting (Ligi Kuu)
  Simba SC 0-0 Express (Kirafiki, Taifa)
  Simba SC 2-4 Mtibwa Sugar (Kirafiki, Chamazi)
  Simba SC 2-0 Yanga SC (Nani Mtani Jembe)
  Simba SC 3-1 Mwaduni United (Kirafiki, Taifa)
  Simba SC 3-1 Taifa Jang’ombe (Kirafiki, Zanzibar)
  Simba SC 0-1 Kagera Sugar (Ligi Kuu Bara)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: GORAN KOPUNOVIC ATAIPIKU REKODI YA PHIRI LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top