• HABARI MPYA

  Thursday, January 08, 2015

  ELIAS MAGURI: SIMBA KWANZA, MIMI BAADAYE

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Elias Maguri amesema kwamba anapokuwa uwanjani anafikiria zaidi kuiwezesha timu kushinda kuliko yeye kufunga.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana baada ya kuiongoza Simba SC kushinda 4-0 dhidi ya Taifa ya Jang’ombe, Maguri amesema kwamba anafurahi sana timu yake hiyo inaposhinda.
  “Nimefurahi sana tumeshinda na tumetinga Nusu Fainali, lengo letu ni kushinda pia hadi kufika Fainali na tunaamini tunaweza, tunaomba sapoti ya mashabiki wetu tuweze kufanya vizuri,”amesema.
  Elias Maguri amefunga mabao matano katika mechi 22 alizocheza Simba SC, lakini mchango wake ni mkubwa katika timu

  Alipoulizwa kwa nini hakuweza kufunga bao hata moja akiwa mshambuliaji mkuu jana, Maguri alijibu; “Ninapoingia uwanjani, kwanza ninafikiria namna ya kuisaidia timu kushinda. Siwezi kuthubutu kuchezea nafasi ya timu kushinda kupitia kwangu, kwa sababu tu nataka nifunge mimi,”amesema.
  Maguri amesema kwamba anapenda mno kucheza kwa manufaa ya timu kuliko kibinafsi na ndiyo maana imekuwa rahisi kwake kuzoeana na wenzake Simba SC ingawa amejiunga na timu hiyo msimu huu.
  “Sisi wachezaji, wengi wetu tunapoingia kwenye timu tunapenda kujionyesha sisi uwezo wetu bila kufikiria kuisaidia timu, sasa mimi ni tofauti sana. Makocha hawaangaalii umefunga mabao mangapi, wanaangalia unaisaidia vipi timu kushinda,”. 
  “Unaweza kufunga halafu timu ikapoteza mechi, inakuwa haina maana. Lakini unapocheza bila kufunga ukifikiria zaidi kuiwezesha timu kushinda ni bora zaidi,”amesema.
  Tangu amejiunga na Simba SC msimu huu akitokea Ruvu Shooting ya Pwani, Maguri amefunga mabao matano tu katika mechi 22, lakini hakuna ubishi mchango wake katika timu ni mkubwa.
  Bao muhimu zaidi alifunga katika ushindi wa 2-0 dhidi ya mahasimu Yanga SC, Desemba 13 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya Nani Mtani Jembe.
  Maguri ni kati ya washambuliaji chipukizi wanaoinukia vizuri katika soka ya Tanzania kwa sasa, ambao wanatarajiwa kuwa tegemeo la timu ya taifa, Taifa Stars muda si mrefu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ELIAS MAGURI: SIMBA KWANZA, MIMI BAADAYE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top