Miraj Adam kulia akizungumza jana na kushoto ni Hussein Twaha |
Na Mahmoud Zubeiry
NAHODHA wa
timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, Miraj Adam
amesema kesho watapigana kwa nguvu zao zote, kuhakikisha wanawafunga Kongo
Brazzaville ili watimize ndoto zao za kucheza Fainali za Vijana chini ya umri
wa miaka 17 nchini Morocco mwakani.
Akizungumza
jana kwenye hoteli ya JB Belmonte, Dar es Salaam, Adam alisema kwamba hata kama
Kongo Brazzaville wamekuja na wachezaji waliovuka umri kwa mujibu wa kanuni za
mashindano hayo, lakini kesho watafungwa tu.
“Kongo
watakufa, watake wasitake, nasema Kongo watakufa,”alisema kwa hisia kali Adam anayechezea
Simba wakati wa hafla maalum ya chakula cha usiku kuichangia timu hiyo.
Kwa upande
wake, Msaidizi wake, Hussein Twaha ‘Messi’ alikumbushia maneno waliyoambiwa na
mwanasoka bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele katika ziara yake nchini hivi
karibuni na kusema yatakuwa kichocheo kwao kufanya vizuri na kukata tiketi ya Morocco.
“Pele
alituambia mpira unachezwa na watoto kutoka familia masikini, hata yeye alitoka
familia ya kimasikini, akajitahidi akafanikiwa na kufanya watoto wake waingie katika
mpira wakitokea familia ya kitajiri, hivyo na sisi tunatumia kauli hii kama
kichocheo cha kufanya vizuri ili tufuate nyayo zake,”alisema Twaha, anayechezea
Coastal Union.
Kocha Mkuu,
Mdenmark Jacob Michelsen alishukuru kwa sapoti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
katika maandalizi na akasema ana matumaini makubwa ya kuwatoa Kongo, kwani
amewaandaa vema vijana wake.
Kocha Msaidizi,
Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema kwamba wachezaji wanatakiwa kujituma ili
kushinda mechi hiyo na kujiwekea mazingira mazuri ya kufuzu.
Rais wa TFF,
Leodegar Tenga aliwaambia vijana kwamba amekuwa mchezaji, kocha, kiongozi, Mjumbe
wa bodi mbalimbali na Mwenyekiti wa Bodi, lakini katika maisha yake ya soka
hakuna kitu anachojivunia kama kuwa Nahodha wa timu ya taifa, hivyo akawataka
vijana wakapigane kesho kwenda kuweka historia.
Juzi Michelsen
alisema kwamba ana wasiwasi wapinzani wake, Kongo Brazzaville wana wachezaji
waliozidi umri, baada ya kuichunguza vizuri Kongo na sasa anaifahahamu vema.
Michelsen
alisema kwamba alikwenda kushuhudia mchezo wa kwanza wa raundi iliyopita, baina
ya Kongo na Zimbabwe waliotolewa na wapinzani wao hao na kujionea makali ya
wapinzani wao.
Pamoja na
kukiri kwamba Kongo ni timu bora na ilicheza Fainali zilizopita za Kombe la
Dunia nchini Mexico mwaka jana na kutolewa raundi ya pili, Michelsen alisema
bado ana wasiwasi timu hiyo ina ‘vijeba’.
“Nilipokwenda
kuwaangalia wakicheza na Zimbabwe, nilikuta kikosini mwao kuna wachezaji sita
wa kikosi kilichokwenda Mexico kwenye Kombe la Dunia, inanitia shaka kwa sababu
hakuna mchezaji anayeweza kucheza michuano mikubwa kama ile akiwa ana umri wa
miaka 15.
Mimi ni
kocha wa vijana na ninajua, haiwezekani. Ucheze fainali za Kombe la Dunia za
U17 una miaka 15, hakuna,”alisema Michelsen, ambaye aliwataja baadhi ya
wachezaji anaowatilia shaka wamezidi umri ni Hady Binguila na Charvely Mabiat.
Amesema
wamecheza mechi za kujipima nguvu 15 zikiwemo dhidi ya timu za Ligi Kuu na
hawajafungwa hata moja, kitu ambacho anaamini ni kipimo cha ubora wa timu yake.
Serengeti jana ilihamia katika hoteli ya JB Belmonte, kutoka hoteli ya Itumbi, ili kuwaweka vizuri kisaikolojia vijana, hizo zikiwa ni jitihada za Kamati maalum iliyoundwa kuisaidia timu hiyo.
Serengeti
imefanikiwa kufuzu hadi Raundi ya Tatu bila jasho, baada ya wapinzani wake wa
awali katika Raundi ya Kwanza na ya Pili, Kenya na Misri kujitoa. Iwapo timu
hii itafuzu, hii itakuwa mara ya pili kwa Serengeti kukata tiketi ya kucheza
fainali hizo, baada ya mwaka 2005.
Hata hivyo,
pamoja na kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe, Serengeti haikwenda Gambia mwaka
huo kutokana na kuondolewa kwenye michuano hiyo na Shirikisho la Soka Afrika
(CAF), baada ya kubainika walitumia kijana aliyezidi umri, Nurdin Bakari.