• HABARI MPYA

  Saturday, February 11, 2017

  SIMBA YATUMA SALAMU JANGWANI, YAIPIGA PRISONS 3-0 NA KUREJEA KILELENI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC leo imerudi kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodcom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 51 baada ya kucheza mechi 22, ikiwashushia nafasi ya pili mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 49 za mechi 21. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Alex Mahaggi wa Mwanza, aliyesaidiwa na Khalfan Sika na Abdallah Rashid wa Pwani, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
  Mabao yote hayo yalifungwa na washambuliaji wazalendo, Juma Luizio na Ibrahim Hajib na wote wakimalizia mipira kutoka pembezoni mwa Uwanja.
  Ibrahim Hajib (katikati) leo amefunga bao na kuseti lingine lililofungwa na Mavugo
  Juma Luizio akiifungia Simba bao la kwanza leo
  Said Ndemla akifumua shuti katikati ya wachezaji wa Prisons
  Laudit Mavugo akimiliki mpira pembeni ya mchezaji wa Prisons
  Ibrahim Hajib (kulia) akimiliki mpira mbele ya wachezaji wa Prisons

  Alianza Luizio anayecheza kwa mkopo Msimbazi kutoka Zesco United ya Zambia aliyefunga dakika ya 18 akimalizia krosi ya beki wa kulia, Janvier Besala Bokungu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kumchambua kipa Aaron Kalambo.
  Na Hajib naye akawainua vitini mashabiki wa Simba dakika ya 28 akimalizia pasi nzuri ya mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo.
  Simba ikajitahidi kupigania bao la tatu baada ya hapo, lakini bahati mbaya kwao Prisons walikuwa wamekwishatulia na kuanza kudhibiti hatari zote.
  Kipindi cha pili nyota ya Simba SC iliendelea kung’ara na wakafanikiwa kuunenepesha ushindi wao kwa bao la tatu lililofungwa na Laudit Mavugo.
  Mavugo aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC baada ya kusajiliwa kutoka Vital’O ya kwao, Burundi alifunga bao hilo dakika ya 67 kwa kichwa akimalizia krosi nzuri ya Ibrahim Hajib ambaye leo alikuwa katika kiwango kizuri.
  Winga Shizza Ramadhani Kichuya aliyetokea benchi kipindi cha pili alikaribia kufunga dakika ya 81 kama si shuti lake kugonga mwamba na mpira kurudi ndani na kumkuta Mavugo, ambaye alipopiga tena mpira ukaenda nje.
  Nafasi nzuri zaidi Prisons walipata katika mchezo huo ilikuwa ni dakika ya 12 baada ya Benjamin Asukile kuunganishia nje ya lango kwa kichwa krosi ya kiungo Mohammed Samatta.
  Baada ya mchezo wa leo, Simba wanakwenda kujichimbia kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu wao, Yanga Februari 25, Uwanja wa Taifa. 
  Kikosi cha Simba kilikuwa; Daniel Agyei, Janvier Bokongu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Method Mwanjali/Mwinyi Kazimoto dk62, James Kotei, Said Ndemla, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim Hajib/Pastory Athanas dk74 na Juma Luizio/Shizza Kichuya dk70.
  Prisons; Laurian Mpalile, Aaron Kalambo, Salum Kimenya, James Mwasote, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Lambert Sibiyanka, Kazungu Nchinjayi/Kassim Hamisi dk38, Victor Hangaya/Salum Bosco dk76, Mohammed Samatta na Benjamin Asukile/Meshack Suleiman dk56.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YATUMA SALAMU JANGWANI, YAIPIGA PRISONS 3-0 NA KUREJEA KILELENI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top