• HABARI MPYA

  Sunday, February 05, 2017

  OMOG AWAAMBIA SIMBA; TULIENI UBINGWA UNAKUJA

  Na Mwandishi Wetu, SONGEA
  KOCHA wa Simba SC, Mcameroon Joseph Marius Omog alikuwa mwenye furaha jana baada ya kushinda 3-0 dhidi ya Maji Maji na akasema wakati anaelekea kwenye gari; “Tulieni ubingwa unakuja”.
  Simba jana ilijirudisha jirani kabisa na mahasimu wao, Yanga SC katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya wenyeji Maji Maji, Uwanja wa Maji Maji Songea mkoani Ruvuma.
  Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 48 baada ya kucheza mechi 21, sasa wakizidiwa pointi moja na mabingwa watetezi, Yanga. 
  Ukiwa ni ushindi wa kwanza kwa Simba mwaka huu katika Ligi Kuu, umepokewa kwa furaha na kila mmoja katika klabu hiyo hadi viongozi.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe aliyekuwapo Uwanja wa Maji Maji akishuhudia kazi nzuri ya vijana aliowasajili msimu huu, alisema; “Haya ndiyo mambo tunayotaka,”.
  Poppe, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alisema kwamba ushindi huo unawafanya wakae sawa katika mbio za ubingwa na sasa wanaelekeza nguvu zao katika mchezo ujao.
  Baada ya ushindi wa Jumamosi, Simba inakwenda mafichoni na itaibuka tena Februari 25 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na mahasimu Yanga.  
  Huo utakuwa mchezo wa kutoa taswira ya ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, kwani atakayefungwa ayamuachia mwenzake usukani.
  Katika mchezo wa juzi uliochezeshwa na refa Ahmed Kikumbo wa Doodma, mabao ya Simba SC yalifungwa na Ibrahim Hajib, Said Ndemla na Laudit Mavugo.
  Hajib alifunga dakika ya 19 akiunganisha vizuri kwa kichwa krosi ya winga Shiza Ramadhani Kichuya, Ndemla alifunga dakika ya 63 kwa shuti baada ya kona chini chini ya kiungo Mghana, James Kotei aliyetokea benchi kipindi cha pili na Mrundi Mavugo akafunga dakika ya 88 akimvisha kanzu beki baada ya pasi ya kichwa ya kiungo Mwinyi Kazimoto aliyetokea benchi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OMOG AWAAMBIA SIMBA; TULIENI UBINGWA UNAKUJA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top