• HABARI MPYA

  Saturday, June 22, 2024

  UHOLANZI NA UFARANSA ZATOSHANA NGUVU, AUSTRIA NA UKRAINE ZASHINDA


  TIMU za Uholanzi na Ufaransa jana zimegawana pointi baada ya sare ya bila mabao katika mchezo wa Kundi D Kombe la Mataifa ya Ulaya 'Euro 2024' Uwanja wa Leipzig Jijini Leipzig nchini Ujerumani.
  Safu ya ushambuliaji ya Ufaransa ilionekana kabisa kupoteza makali yake kutokana na kumkosa Nahodha wake, Kylian Mbappé Lottin aliyeumia pua kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Austria Uwanja wa Merkur Spiel-Arena Jijini Düsseldorf.
  Katika mchezo huo ambao Ufaransa ilishinda 1-0, Mbappe aliyejiunga na Real Madrid mwezi huu - aliumia pua baada ya kugongana na beki wa Lens ya Ufaransa, Kevin Danso na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na mshambuliaji wa AÇ Milan, Olivier Giroud dakika ya 90.
  Mechi nyingine ya Kundi D jana Austria iliibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Poland Uwanja wa  Olympia Jijini Berlin. 
  Sasa msimamo wa Kundi D ni Uholanzi na Ufaransa pointi nne kila moja, zikifuatiwa na Austria yenye pointi tatu na Poland inayoshika mkia ambayo haina pointi.
  Mabao ya Austria yalifungwa na Nahodha wake, beki wa  Feyenoord, Gernot Trauner dakika ya tisa, kiungo wa  RB Leipzig, Christoph Baumgartner dakika ya 66 na mshambuliaji wa Bologna, Marko Arnautović anayecheza kwa mkopo Inter Milan kwa penalti dakika ya 78, wakati bao pekee la Poland lilifungwa na mshambuliaji wa  İstanbul Başakşehir ya Uturuki, Krzysztof Piątek dakika ya 30.
  Mapema katika mchezo uliotangulia wa Kundi E, Ukraine iliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Slovakia Uwanja wa Düsseldorf Arena Jijini Düsseldorf.
  Mabao ya Ukraine yalifungwa na kiungo wa Dynamo Kyiv, Mykola Shaparenko dakika ya 54 na mshambuliaji wa Valencia, Roman Yaremchukon anayecheza kwa mkopo Club Brugge dakika ya 80, wakati bao pekee la Slovakia lilifungwa na mshambuliaji wa Slavia Prague, Ivan Schranz dakika ya 17.
  Romania na Ubelgiji zinakutana leo Saa 3:00 usiku katika mchezo mwingine wa Kundi E Uwanja wa RheinEnergie Jijini Cologne.
  Kwa sasa msimamo wa Kundi E ni Ukraine na Slovakia zote zina pointi tatu baada ya kucheza mechi mbili, sawa na Romania iliyocheza mechi moja wakati Ubelgiji inashika mkia haina pointi.
   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: UHOLANZI NA UFARANSA ZATOSHANA NGUVU, AUSTRIA NA UKRAINE ZASHINDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top