• HABARI MPYA

  Tuesday, June 11, 2024

  WAZIRI JUNIOR AFUNGA TAIFA STARS YAWAPIGA ZAMBIA 1-0 PALE PALE NDOLA


  TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Zambia katika mchezo wa Kundi E kufuzu Kombe la Dunia 2026 uliofanyika Uwanja wa Levy Mwanawasa Jijini Ndola.
  Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee mshambuliaji wa KMC, Waziri Junior Shentembo dakika ya tano akimalizia pası ya kiungo wa Yanga SC, Mudathir Yahya Abbas.
  Kwa ushindi huo, Taifa Stars inafikisha pointi sita katika mchezo wa tatu na kusogea nafasi ya pili nyuma ya vinara, Morocco ‘Simba wa Atlasi’ ambao wamecheza mechi mbili, wakati Zambia inabaki na pointi zake tatu za mechi nne nafasi ya nne ikizidiwa tu wastani wa mabao na Niger iliyocheza mechi mbili - na Kongo inashika mkia ikiwa imecheza mechi moja na kufungwa.
  Wapinzani wengine katika Kundi E kufuzu Kombe la Dunia 2026 Eritrea walijitoa katika mbio za kuwania tiketi ya Fainali hizo zinazoandaliwa kwa pamoja na Canada, Mexico na Marekani.
  Mechi mbili za awali Taifa Stars ilifungwa 2-0 na Morocco nyumbani Novemba 21 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya Niger Novemba 18 mwaka jana Uwanja wa Marrakech nchini Morocco.
  Siku hiyo bao pekee la Taifa Stars lilifungwa na mshambuliaji mzaliwa wa DRC, Kokola Charles William M'Mombwa wa Macarthur FC ya Australia.
  Mechi zijazo Taifa Stars itacheza mwakani ikianzia nyumbani dhidi ya Kongo Machi 17, kabla ya kwenda ugenini kwa michezo miwili, dhidi ya Morocco Machi 24 na Kongo Septemba 1.
  Baada ya hapo Taifa Stars itarejea nyumbani kwa michezo miwili ya mwisho ya Kundi E dhidi ya Niger Septemba 8 na Zambia Oktoba 6 mwakani.
  Washindi wa kwanza tisa wa makundi A, B, C, D, E, F, G, H na I watafuzu moja kwa moja Kombe la Dunia 2026, wakati timu nne zitakazomaliza nafasi ya pili na wastani mzuri zitamenyana katika Mchuno kutafuta ya kwenda kwenye mchujo wa Mabara utakaohusisha pia timu za mabara yote kasoro UEFA na nyingine moja kutoka Bara wenyeji, CONCACAF.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAZIRI JUNIOR AFUNGA TAIFA STARS YAWAPIGA ZAMBIA 1-0 PALE PALE NDOLA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top