• HABARI MPYA

    Sunday, May 14, 2017

    SPORTPESA WAIVURUGA SIMBA, MO DEWJI ADAI 'MAHELA' YAKE, HANS POPPE ABWAGA MANYANGA MSIMBAZI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    MFANYABIASHARA Mohammed Dewji anayetaka kununua hisa Simba, amesikitishwa na uongozi wa klabu hiyo kwa kuingia mkataba wa udhamini na kampuni ya SportPesa bila kumshirikisha.
    Na habari ambazo hazijathibitishwa na upande wowote, zinasema Mo Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini ameuandikia barua uongozi wa klabu hiyo chini ya Rais wake, Evans Aveva kudai alipwe fedha zake, Sh Bilioni 1.4 alizokuwa anaikopesha Simba kwa kulipa mishahara ya wachezaji na benchi la Ufundi, Sh Milioni 80 kila mwezi.
    Imedaiwa Mo Dewji alikuwa anatoa fedha hizo kwa makubaliano zitalipwa wakati mpango wake wa kununua hisa za klabu utakapokamilika. Mo alikubaliana na uongozi wa Simba kununua asilimia 51 ya hisa kwa Sh. Bilioni 20 mara baada ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba utakapokamilika.
    Zacharia Hans Poppe (kulia) amejiuzulu Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba 
    Lakini zoezi hilo linaelekea kuingia doa baada ya Mo Dewji kuandika katika ukurasa wake wa Twitter akilalamikia uongozi wa klabu kuingia mkataba na SportPesa bila kumshirikisha.   
    Na upande mwingine, uongozi wa Simba na umemeguka baada ya Mjumbe wa kuteuliwa wa Kamati ya Utendaji, Zacharia Hans Poppe kuandika barua ya kujiuzulu, naye pia akilalamikia kutoshirikishwa katika mkataba wa SportPesa.
    Hans Poppe aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Kamati za Usajili na mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Bunju Complex, amezungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo na kuthibitisha kujiuzulu kwake, lakini hakutaka kuzama ndani zaidi juu ya sakata hilo.
    Ijumaa SportPesa Tanzania ilitangza rasmi udhamini wake wa miaka mitano kwa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, wenye thamani ya Sh. Bilioni 4.96.
    Mkurugezi wa Utawala wa SportPesa, Tarimba Abbas alisema kwamba wameingia mkataba huko kwa dhumuni la kuendeleza soka nchini na kuisaidia klabu ya Simba kufikia malengo yake.
    Akifafanua, Tarimba ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa mahasimu wa Simba, Yanga alisema kwamba, katika mkataba wao kwa mwaka wa kwanza wadhamini hao watatoa Sh. Milioni 888 na miaka itakayofuata wataongeza asilimia 5 na miaka miwili ya mwisho watatoa Sh. Bilioni 1 na kwamba fedha hizo zitatolewa kwa awamu nne kwa mwaka.
    Tarimba alisema kwamba Simba watapaswa kuyathibitisha matumizi ya fedha hizo kwamba yalifanyika kwa maendeleo ya soka.
    Alisema licha ya mkataba huo, pia kutakuwa na motisha klabu hiyo ikishinda mataji, mfano kwa ubingwa wa Ligi Kuu watapewa zawadi ya Sh. Milioni 100.
    “Pia ikishinda michuano kama (Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati) Kombe la Kagame pia watapewa zawadi na wakifanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika watapata zawadi ya Milioni. 250,”alisema Tarimba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SPORTPESA WAIVURUGA SIMBA, MO DEWJI ADAI 'MAHELA' YAKE, HANS POPPE ABWAGA MANYANGA MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top