• HABARI MPYA

    Monday, March 09, 2015

    MANJI AMKWIDA KIGOGO SIMBA SC, AMFUNGULIA KESI POLISI YA KUJERUHI MTOTO WAKE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIGOGO wa Friends of Simba na mmoja wa wafadhili wa muda mrefu wa Simba SC, Musley Al Ruweh, ameshitakiwa na Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji.
    Kisa? Manji anadai Musley amemjeruhi mwanawe, Mehbub Ally Manji jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya mchezo baina ya timu hizo.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY usiku huu, Musley amesema kwamba amepigiwa simu na Polisi wa kituo cha kati, Dar es Salaam akitakiwa kwenda kutoa maelezo ya kumjeruhi mtoto wa Manji. “Nitakwenda kesho, leo nilishindwa kwenda kwa sababu nilikuwa mbali,”amesema Musley. 
    Musley kulia akiwa na Zacharia Hans Poppe 
    Yussuf Manji kulia amemfungulia mashitaka Musley Polisi

    Alipoulizwa chanzo cha matatizo yao, Musley ambaye amerithi mapenzi ya Simba SC kutoka kwa baba yake, aliyekuwa mfadhili wa klabu hiyo miaka ya 1970, amesema kwamba mtafaruku ulitokea kwenye lifti.
    “Baada ya mechi mimi nilikwenda kwenye lifti kupanda nishuke chini niende kwenye vyumba vya wachezaji. Nilipofika kwenye lifti watu walikuwa wengi, ikabidi nijichomeke nijibane,”.
    “Kwa bahati mbaya lifti ikawa haiendi kwa sababu ilikuwa imejaa. likatolewa wazo watu wapungue, sasa katika watu waliokuwa mbele mmojawao alikuwa huyo mtoto wa Manji, mimi simjui. Yule mtoto akashuka mwenyewe,”.
    “Aliposhuka, Manji kumbe alikuwa nyuma yangu, akanivaa akaanza kunishambulia kwa maneno kwamba mimi nimemsukuma mwanawe, wakati si kweli. Yule mtoto alishuka mwenyewe,”.
    “Kwa kweli mimi sikutaka kupigana naye, na watu wakasema nimuache kwa sababu ana hasira za kufungwa (Yanga ilifungwa 1-0 jana). Alinikunja hadi akanivua kitambulisho changu. Lifti ilipofika chini, mimi nikaenda kwenye chumba cha wachezaji,”.
    Karatasi ya hospitali inayoonyesha mtoto wa Manji alivyojeruhiwa 
    Karatasi ya Polisi, Musley atajibu kesho

    Nasikia Manji alikuja hadi kule ananitafuta, lakini sikumfuatilia. Mimi nikaondoka zangu. Sasa leo nimepigiwa simu naitwa Polisi. Nitakwenda kesho. Ila baada ya pale tulifanya jitihada za kuyamaliza haya, lakini Manji amekataa,”amesema Musley.
    Jitihada za kumpata Manji usiku huu kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa, lakini BIN ZUBEIRY imefanikiwa kupata vielelezo vya taarifa za hospitali kwamba mtoto alijeruhiwa, ambavyo vimeambatanishwa katika jarida alilofunguliwa Musley.      
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI AMKWIDA KIGOGO SIMBA SC, AMFUNGULIA KESI POLISI YA KUJERUHI MTOTO WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top