• HABARI MPYA

  Saturday, January 10, 2015

  SIMBA SC YAKABA KONA ZOTE KOMBE LA MAPINDUZI, KOCHA MPYA NI MJUZI KWELI

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC leo wana mtihani mgumu mbele ya Polisi ya Zanzibar watakapomenyana nayo katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, Uwanja wa Amaan mjini hapa.
  Mchezo huo utaanza Saa 2:15 usiku, baada ya kumalizika kwa Robo Fainali ya Kwanza, kati ya Mtibwa Sugar ya Morogoro dhidi ya JKU ya hapa pia, kwenye Uwanja huo huo, Amaan.
  Mtibwa Sugar, JKU na Simba SC zote zimetoka Kundi C, ambako zilikuwa pamoja na Mafunzo wakati Polisi imetoka Kundi A, ambako ilikuwa na Yanga SC, Taifa ya Jang’ombe na Shaba ya Pemba.
  Simba SC waliingia Nusu Fainali baada ya kuwafunga Taifa mabao 4-0, wakati Mtibwa Sugar waliitoa Azam FC kwa penalti 7-6 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, huku JKU ikiifunga Yanga SC 1-0 na Polisi iliwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, KCCA ya Uganda kwa penalti 5-4 baada ya sare 0-0.
  Polisi ilipita ‘kizali zali’ katika kundi lake na ilifungwa 4-0 na Yanga katika mchezo wa Kundi A, ila ikaja kuwastaajabisha wengi kwa kuwatoa mabingwa watetezi, KCCA.
  Kocha wa Simba SC, Goran Kopunovic akimfundisha kiungo Said Ndemla kupiga mipira ya adhabu
  Kopunivic akiwafundisha wachezaji wake kupiga penalti, hapa Abdallah Seseme anakwenda kupiga
  Dan Sserunkuma akimdhibiti kipa Peter Manyika, anatakiwa afanye hivi leo kwa kipa wa Polisi

  Na kuelekea mchezo na Simba SC leo hakuna anayeweza kuthubutu kutabiri matokeo kwa kuwa tayari Polisi imekwishaonyesha ni timu isiyotabirika- ilishindwa kuwafunga Taifa waliofungwa 4-0 na Yanga na Simba, lakini ikawang’oa KCCA.
  Kocha mpya wa Simba SC, Mserbia Goran Kopunovic jana amewafanyisha wachezaji wake mazoezi mara mbili, kwanza Uwanja wa Chukwani asubuhi na baadaye jioni Uwanja wa Amaan.
  Mazoezi ya asubuhi yalikuwa programu kamili kuanzia fiziki, kasi, maarifa na kuucheza mpira, lakini jioni walikwenda kufanyia kazi mambo kadhaa juu ya mbinu za kukabiliana na timu inayocheza mchezo wa kujihami.
  Kopunovic anahisi kabisa Polisi watarudia kucheza mchezo wa kujihami kama walivyofanya dhidi ya KCCA na jana aliwafundisha wachezaji wake maarifa ya kukabiliana na mchezo wa aina hiyo, maarufu kama ‘kupaki basi’.
  Pamoja na hayo, Kopunovic alionekana kumuandaa kiungo Said Hamisi Ndemla kwa ajili ya kupiga mipira yote ya adhabu, ikiwemo kona.
  Alikuwa akimuandaa mshambuliaji Dan Sserunkuma kumghasi kipa wa Polisi na mwisho akawapa wachezaji wote mafunzo ya upigaji penalti, zoezi ambalo lilikwenda vizuri.
  Kipa Manyika Peter alionyesha umahiri kwa kuokoa michomo kadhaa na wachezaji wengi wa Simba walionyesha ujuzi wa kupiga penalti.            
  Mwaka jana Simba SC ilifika Fainali na kufungwa na KCCA mabao 2-0 na leo itakuwa inawania kucheza mechi ya mwisho ya mashindano hayo kwa mara ya pili mfululizo na kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza tangu 2011 ilipowafunga mahasimu Yanga SC katika fainali 2-0, mabao ya Mussa Hassan Mgosi, sasa yupo Mtibwa Sugar na Shijja Mkina ambaye aliachwa mwishoni mwa mwaka huo.
  Wachezaji wote waliosajiliwa na Simba SC wapo Zanzibar kasoro Nahodha Joseph Owinio pekee aliye kwao Uganda, lakini kipa Ivo Mapunda na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi waliokuwa na udhuru tayari wapo kambini.
  Wawili hao, hawana nafasi ya kuwekwa hata benchi katika mchezo wa leo, lakini iwapo Simba SC itaingia Fainali wanaweza kushiriki mchezo huo Jumatatu.   
  Kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kuwa; Peter Manyika, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’, Said Ndemla, Elias Maguri, Dan Sserunkuma na Awadh Juma.
  Katika benchi wanatarajiwa kuwapo Ivo Mapunda, Shaaban Kisiga ‘Malone’, Said Nassor ‘Chollo’, Ibrahim Ajibu, Abdallah Seseme, Abdu Banda, Simon Sserunkuma, Twaha Ibrahim ‘Messi’ na wengineo.
  Polisi wao kikosi chao kinaweza kuwa; Nasir Suleiman, Mohammed Seif, Mwita Mohammed, Abdallah Mwalimu, Mohammed Ally, Daniel Justin, Steven Emmanuel, Ali Khalid, Said Bakari, Frank Temis na Mohamed Hassan.
  Baadhi ya wanaotarajiwa kuwapo kwenye benchi la Polisi ni pamoja na Samir Vincent na Abdallah Omar.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAKABA KONA ZOTE KOMBE LA MAPINDUZI, KOCHA MPYA NI MJUZI KWELI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top