Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
WAKATI michuano ya Kombe la Mapinduzi inafikia tamati kesho, mshambuliaji wa Simba SC Ibrahim Salum Hajibu yupo katika nafasi nzuri ya kuwa mfungaji bora, huku Peter Manyika akiwania kuwa kipa bora.Kwa sasa, Hajibu anashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao katika mashindano haya ya takriban wiki mbili kwa mabao yake matatu aliyofunga katika mchezo mmoja dhidi ya Taifa Jang’ombe, Simba SC ikishinda 4-0 na kwenda Nusu Fainali.
Anayeongoza kwa mabao ni Simon Msuva aliyefunga mara nne, lakini kwa bahati mbaya, timu yake Yanga SC ilitolewa katika Robo Fainali na JKU.
Ibrahim Hajibu wa pili kulia baada ya Said Ndemla, anaweza kuibuka mfungaji bora wa Kombe la Mapinduzi mwaka huu iwapo atafunga kesho |
Mbrazil Andrey Coutinho wa Yanga SC pia, Mganda William Wadri wa KCCA na Amour Omar ‘Janja’ wa JKU nao wana mabao matatu kila mmoja sawa na Hajibu, lakini wote wamekwishaaga mashindano baada ya timu zao kutolewa.
Mchezaji mwenye nafasi ya kumpiku Hajibu, ni winga wa Simba SC, Ramadhani Singano ‘Messi’ mwenye mabao mawili sawa Mliberia Kpah Sherman wa Yanga SC.
Messi aliyefunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 katika Nusu Fainali Simba SC ikiifunga JKU, anatarajiwa kuanza kesho katika kikosi cha kwanza, wakati Hajibu anaweza kuendelea kutokea benchi.
Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanaonekana kumuibua tena Messi, ambaye siku za karibuni cheche zake ziliyeyuka.
Aidha, kipa mdogo Peter Manyika amejiweka katika mazingira mazuri ya kushinda tuzo ya mlinda mlango bora, baada ya kudaka mechi nne mfululizo bila kufungwa hata bao moja.
Peter Manyika anaweza kuwa kipa bora |
Mtoto huyo wa kipa wa zamani wa kimataifa Tanzania na klabu ya Yanga SC, alifungwa bao moja katika mchezo wa kwanza na Mtibwa Sugar Simba SC ikilala 1-0, lakini baadaye akadaka Wekundu wa Msimbazi wakishinda 1-0 mara tatu dhidi ya Mafunzo, JKU mara mbili mchezo wa Kundi C na Nusu Fainali na 4-0 dhidi ya Taifa.
Mpinzani wa Manyika katika tuzo ya kipa bora, ni Said Mohammed wa Mtibwa Sugar ambaye amefungwa bao moja na pia aliokoa penalti mara mbili katika Robo Faiali na Nusu Fainali, akiiwezesha timu yake kufika Fainali.
Kiungo Said Ndemla wa Simba SC, beki Salum Mbonde wa Mtibwa Sugar, wote wamecheza vizuri mechi zote za timu zao hadi sasa na haitakuwa ajabu mmoja kati yao, akitajwa mchezaji biora wa mashindano, iwapo atarudia kucheza vizuri kesho Uwanja wa Amaan usiku katika Fainali.
ORODHA YA MABINGWA KOMBE LA MAPINDUZI
Mwaka Bingwa Mshindi wa Pili
2007 Yanga SC Mtibwa Sugar
2008 Simba SC Mtibwa Sugar
2009 Miembeni KMKM
2010 Mtibwa Sugar Ocean View
2011 Simba SC Yanga SC
2012 Azam FC Simba SC
2013 Azam FC Tusker FC
2014 KCCA Simba SC
2015 ??????? ???????
0 comments:
Post a Comment