• HABARI MPYA

  Monday, January 19, 2015

  ADUI MWINGINE WA BENDI ZETU NI HUYU HAPA

  Bado hadithi ya vurugu waliyofanyiwa wanamuziki wa Malaika Band pale New White House Kimara mwaka jana, haitaki kufutika kichwani mwangu.
  Nadhani wengi wetu tunafahamu kisa cha vurugu zile lakini kwa kukumbushana tu ni kwamba Malaika walinadi show yao wakisema Christian Bella atakuwepo huku wakijua wazi kuwa msanii huyo bado atakuwa nje ya nchi.
  Christian Bella hakuwepo, mashabiki wakachukia, wakachukua sheria mkononi, wakaanzisha vurugu za kuwashambulia wanamuziki wa Malaika pamoja na kuharibu vyombo vyao.

  Lakini hili la Bella si kwanza wala la pili kutokea. Siku moja Jahazi walifanya onyesho lao ndani ya Lugalo jeshini, vipeperushi na posters zao zilionyesha wazi kuwa Mzee Yussuf atakuwepo, lakini siku ya show hakuwepo.
  Unajua kilichotokea? Wanajeshi wakawachukua viongozi wa Jahazi na kuwaweka ‘rumande’ kwa muda, wakasema hapo hawatoki bila Mzee Yussuf kuja ukumbini.
  Ilikuwa ni zoezi gumu na refu kuwaelewesha maafande wale kuhusu kukosekana kwa Mzee Yussuf, mwisho wa siku somo likaeleweka lakini kwa onyo kali kuwa ‘msithubutu kufanya onyesho lingine hapa bila Mzee Yussuf’.  
  Mifano hiyo miwili inatufundisha nini? Inatufunza tuelewe kuwa pesa ni ngumu na ni vizuri kumpatia mtu huduma aliyotaraji kuipata kwa kadri ya vile vivutio vilivyotumika kunadi onyesho ili aone pesa yake imeenda kihalali.
  Kuna jambo moja ambalo bendi zetu huwa inalichukulia kwa uzito mwepesi. Promota anakodi show na kisha anatangaza kuwa bendi itasindikizwa na kundi fulani, msanii fulani au wasanii kadha wa kadha, lakini siku ya onyesho wasanii wote waliotajwa kama wasindikizaji hawaonekani ukumbini halafu bendi inachukulia poa tu.
  Ni ukweli usiopingika kuwa onyesho linapofana au kudorora basi sifa au lawama huenda kwa bendi na si promota …ni bendi itakayopigwa mawe, ni vyombo vya bendi vitakavyoharibiwa, ni gari la bendi litakapasuliwa vyoo …promota yuko salama salmin.
  Ifike wakati viongozi wa bendi lazima wawe mstari wa mbele kuhakikisha uongo wa promota hauna nafasi, kabla promota hajaanza kunadi show awajulishe muundo wa onyesho lake na kama ana wasanii waalikwa basi awapatie nakala ya mikataba ya wasanii hao, kinyume na hapo mtu huyo ni wa kuogopwa kama ebola … ‘rongo rongo za aina hii pia hupelekea bendi kupoteza mashabiki bila kujijua.
  Kingine ni kuheshimu viongozi wetu wa kitaifa, promota anapowataja kienyejienyeji tu kuwa waheshimiwa hao watakuwa wageni rasmi wa onyesho fulani halafu hawaonekani ukumbini na wala hakuna wawakilishi wao, ni kuwavunjia heshima. 
  Jana kuliwa na onyesho la Jahazi pale Travertine Hotel, tukatangaziwa kuwa atakuwepo Waziri wa Utamaduni pamoja na waheshimiwa wabunge lakini hadi mwisho wa onyesho hakuna Waziri wala Mbunge.
  Tukatangaziwa kuwa watakuwepo wasanii wa bongo movie akina Anti Ezekiel, Wema Sepetu, Ray na JB, lakini hakuna kati yao aliyekuwepo Travertine. Hata baadhi ya waaimbaji waalikwa nao hawakutokea. 
  Vipi kama mashabiki wangekuwa wakali na kutaka ‘andiko litimie’ kwamba wanahitaji kuwaona wote waliotajwa katika onyesho hilo, unadhani madhara yangekuwa kwa nani? Bendi au promota?
  Siku yakitokea maafa kutokana na ujanja ujanja kama huo, mtuhumiwa wa kwanza ni bendi, halafu ndiyo wanafuata wamiliki wa ukumbi na wengine na wengine na wengine. Rongo rongo (ubabaishaji) ni adui mwingine wa bendi zetu, iwe ni rongo rongo za promota, iwe ni za bendi jibu linabakia moja tu: RONGO RONGO NI ADUI.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ADUI MWINGINE WA BENDI ZETU NI HUYU HAPA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top