• HABARI MPYA

    Sunday, June 01, 2014

    STARS NA ZIMBABWE NI KUFA NA KUOPONA LEO HARARE

    Na Mahmoud Zubeiry, HARARE
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inashuka dimbani leo Uwanja wa Taifa wa Harare mjini hapa kumenyana na wenyeji Zimbabwe katika mchezo wa marudiano hatua ya kwanza ya mchujo ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2015.
    Tanzania iliyoshinda 1-0 bao la John Bocco wa Azam FC katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo itahitaji sare yoyote kusonga mbele katika hatua ya mwisho ya mchujo, ambako ikifuzu itapangwa kwenye Kundi kuwania tiketi ya Morocco 2015.
    Kikosi cha Taifa Stars
    Stars iliyofikia katika hoteli ya Best City Lodge mjini hapa, pamoja na misukosuko waliyoipata juzi mjini hapa ya kufungiwa vyumba vya hoteli kwa saa mbili, wachezaji wake wanaonekana kuwa katika morali ya hali ya juu kuelekea mchezo huo.
    Kocha Mart Nooij raia wa Uholanzi bado ni mwenye kujiamini kuelekea mchezo huo licha ya matokeo ya ushindi mwembamba Dar es Salaam na amesema watacheza kwa kujiamini leo.
    Zimbabwe imekiongezea nguvu kikosi chake kwa wachezaji waliokosa mchezo wa kwanza ambao wanacheza soka ya kulipwa Afrika Kusini na nchi nyingine.
    Kwa ujumla, Zimbabwe imeweka nguvu nyingi katika mchezo huo kuhakikisha inapindua matokeo na kuitoa Tanzania.
    Lakini Tanzania ina kumbukumbu nzuri katika mechi zake za miaka ya karibuni nchini hapa kwa ngazi ya klabu na kimataifa.
    Mwaka 2001 klabu ya Yanga baada ya sare ya 2-2 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Highlanders katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilifanikiwa kuifunga timu hiyo 2-1 mjini Bulawayo na kusonga mbele.
    Lakini mchezo haukumalizika baada ya Yanga kupata penalti ikiwa inaongoza 2-1 ambayo wenyeji waliigomea na kuanzisha vurugu, zilizosababisha mchezo kuvunjika.
    Yanga ilisonga mbele na kwenda kutolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
    Mwaka 2005, timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 17 ilianza kwa ushindi wa 2-0 Dar es Salaam na katika mchezo wa marudiano mjini  Bulawayo ikashinda pia na kuitoa Zimbabwe.
    Hata hivyo, pamoja na Serengeti Boys kufuzu fainali za U17 Afrika zilizopigwa Gambia, lakini ilienguliwa kwa tuhuma za kumtumia Nurdin Bakari akiwa amezidi umri, wakati huo akichezea Simba SC.
    Kikosi cha Tanzania leo hakitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa kutoka kile kilichocheza mechi ya kwanza na kushinda 1-0 Dar es Salaam bao pekee la John Bocco ‘Adebayor’.
    Bila shaka Nooij ataawaanzisha tena pamoja washambuliaji watatu, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu wote wa TP Mazembe ya DRC na Bocco, wakati katika safu ya kiungo Mwinyi Kazimoto wa Markhiya ya Qatar na Frank Domayo wa Azam watapewa majukumu.
    Mrisho Ngassa wa Yanga SC atacheza pembeni akiwa na jukumu la kutengeneza mashambulizi na kusaidia safu ya kiungo.
    Shomary Kapombe atacheza tena beki ya kulia, wakati kushoto kuna uwezakano Erasto Nyoni, wote wa Azam FC akaanza badala ya Oscar Joshua na mabeki wa kati bila shaka watapangwa tena Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan, wakimlinda kipa Deo Munishi ‘Dida’, wote wa Yanga.
    Bado Stars itakuwa na hazina nzuri katika benchi ya wachezaji hodari kama Simon Msuva, Ramadhani Singano ‘Messi’, Haroun Chanongo na wengineo.
    Ikumbukwe huu utakuwa mchezo wa pili wa mashindano kwa Nooij tangu arithi mikoba ya Mdenmark Kim Poulsen baada ya wa awali na Zimbabwe Dar es Salaam.
    Aidha utakuwa mchezo wa nne kwa ujumla tangu aanze kazi Taifa Stars akitokea St George ya Ethiopia, mechi nyingine mbili zikiwa dhidi ya Malawi, moja akitoa sare ya bila kufungana Mbeya na nyingine akishinda 1-0 Dar es Salaam.               
    Mungu ibariki Tanzania, ibariki Taifa Stars. Amin
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS NA ZIMBABWE NI KUFA NA KUOPONA LEO HARARE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top