• HABARI MPYA

    Thursday, November 14, 2013

    VIGOGO YANGA WAVAMIA STARS KUSAKA WACHEZAJI WA KUSAJILI

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    VIONGOZI wawili maarufu wa Yanga kwa masuala ya usajili, Seif Ahmed ‘Magari’ na Abdallah Ahmed Bin Kleb jana walitokea katika mechi ya kirafiki baina ya timu ya pili ya taifa, Future Young Taifa Stars dhidi ya timu ya kwanza, Taifa Stars Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
    Alianza kufika Seif Magari na muda mfupi baadaye akaibuka Bin Kleb na wote watatuliza akili zao kutazama mechi hiyo.
    Wazi wawili hawa waliofanikisha kumsajili kipa mkongwe Juma Kaseja wiki iliyopita, walikuwa wanatafuta wachezaji wengine wa kusajili. 
    Bin Kleb akiwasili Karume jana

    Anashuka...
    Mdogo mdogo

    Anatazama vijana
    Bin Kleb, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, tayari amesema kwamba watasajili wachezaji watatu zaidi baada ya kipa Juma Kaseja na lengo lao ni kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa mwakani.
    Alisema baada ya kufanikisha usajili wa kipa Juma Kaseja, sasa wanahamia katika nafasi nyingine kuboresha timu yao.
    Alisema watasajili beki mmoja wa kati, kiungo mkabaji na mshambuliaji mmoja ambao hata hivyo alisema bado mchakato wa kuwatafuta unaendelea.
    “Tunataka kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa mwakani, tunahitaji kuandaa timu vizuri pamoja na kusajili. Tatizo kubwa ni kalenda hii imekaa vibaya, kiasi kwamba tunakosa muda wa kuiandaa timu vizuri,”.
    Seif Magari anawasili


    “Mwezi huu wachezaji wetu wengi watakwenda Kenya na timu ya taifa kwenye michuano ya Challenge, wakirudi tu kuna mechi dhidi ya Simba ya Ngao ya Hisani Mwanza ambayo imeandaliwa na wadhami TBL,”
    “Kwa hivyo unakuta muda wa mwalimu kutekeleza programu yake vizuri unakosekana, ila tutapambana na hali hiyo kwa vyovyote ili kutimiza malengo yetu,”alisema.
    Future Young Taifa Stars jana ilionyesha ina wachezaji wengi wazuri, baada ya kuifunga Taifa Stars 1-0, bao pekee la mshambuliaji wa Ruvu Shooting ya Pwani, Elias Maguri aliyeunganisha krosi ya chipukizi wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Juma Luizio.
    Kabla ya kutia krosi, Luizio alimpokonya mpira beki mkongwe wa Yanga na mchezaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Kevin Yondan ambaye alianzishiwa na kipa wake, Ally Mustafa ‘Barthez’.
    Kwa ujumla Future waliihenyesha Stars inayoundwa na wachezaji nyota wa Tanzania wakiwemo Mrisho Ngassa, ambaye hii leo alishindwa kufurukuta.
    Kikosi cha Furure kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’ (Yanga)/Aishi Manula (Azam), Michael Pius (Ruvu Shooting)/John Kabanda (Mbeya City)/Kessy Hamisi (Mtibwa Sugar), Himid Mao (Azam FC)/Hassan Mwasapili (Mbeya City), Ismail Gamba ‘Kussi’ (Azam Akademi), Said Mourad (Azam FC), Jonas Mkude (Simba), Ramadhani Singano ‘Messi’ (Simba SC)/Joseph Kimwaga (Azam FC), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Elias Maguri (Ruvu Shooting)/Paul Nonga (Mbeya City), Juma Luizio (Mtibwa Sugar)/Farid Mussa (Azam FC) na Haroun Chanongo/(Simba B)Simon Msuva/(Yanga SC) na Hussein Javu (Yanga SC). 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VIGOGO YANGA WAVAMIA STARS KUSAKA WACHEZAJI WA KUSAJILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top