• HABARI MPYA

    Friday, October 18, 2013

    ACHENI KIBADENI AITWE KING WA SIMBA NA YANGA

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zinatarajiwa kuwaka moto Jumapilii (Oktoba 20, 2013) kwa mpambano wa watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. BIN ZUBEIRY inaendelea kukuletea mfululizo wa makala za kuelekea pambano hilo linalobeba picha halisi ya soka ya Tanzania na leo tunahamia kwa mchezaji aliyefanya mambo makubwa zaidi na ya kukumbukwa daima katika michezo iliyowahi kuwakutanisha wapinzani hao wa jadi. Endelea.
    Acheni aitwe King; Kibadeni ndiye pekee aliyefunga hat trick mechi za watani

    SASA ni miaka 36, tangu mmoja wa washambuliaji hodari kabisa kuwahi kutokea ardhi ya Tanzania, Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’, aweke rekodi ya kufunga mabao matatu katika mechi moja, kwenye mapambano ya watani wa jadi, Simba na Yanga.
    Wengi wamejaribu kutaka kuvunja rekodi hiyo na wa mwisho alikuwa ni Mganda, Emmanuel Okwi aliyeishia kwenye mabao mawili katika ushindi 5-0 Oktoba 3, mwaka jana.
    Ilishindikana mtu kuvunja rekodi hiyo mbele ya ‘Yanga Mdondo’, Mei 6, mwaka jana na je itawezekana kweli Jumapili, kila timu ikionekana kupania na iko vizuri? Labda!  
    Kucheza Simba au Yanga ni fahari kwa mchezaji wa Tanzania. Lakini ni fahari zaidi iwapo atakuwa mchezaji ambaye atashiriki mechi baina ya timu hizo.
    Inakuwa fahari zaidi iwapo mchezaji atafunga bao au mabao katika mechi ya watani wa jadi, kwani huwafanya maelfu ya mashabiki wa timu yake walitaje jina lake na kushangilia kwa raha zao. Wengine, hupewa zawadi kutokana na kufunga kwenye mechi hizo za watani.
    Wapo waliolewa sifa na kupotea kwenye ramani ya soka haraka, kwa sababu tu ya kuvimba kichwa baada ya kufunga mabao mfululizo kwenye mechi za watani.
    Said Sued 'Scud', alifunga bao pekee la ushindi kwenye mechi ya watani wa jadi, akiwa anaichezea Yanga alitikisa nyavu za Simba dakika ya saba katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, sasa Ligi Kuu Mei 18, mwaka 1991.
    Kibadeni kulia baada ya kupewa tuzo ya mchezaji bora daima kuwahi kutokea Simba SC. Aliyepeana naye mikono ni Katibu wa zamani wa klabu hiyo, Kassim Dewji, waanaofuatia ni wanachama maarufu wa klabu hiyo, Mohamed Nassor 'Muddy Kigoma' na Musley Ruwey.

    Huo ukiwa msimu wake wa kwanza kwenye klabu hiyo, hakika ilikuwa furaha kubwa kwake, kwani tangu hapo aliaminika na kuwa mchezaji wa kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.
    Chipukizi huyo wa wakati huo, alipata ngekewa ya kuifunga tena Simba katika mchezo uliofuata wa marudiano wa ligi baina ya watani wa jadi, likiwa pia bao pekee la ushindi Agosti 31, mwaka huo huo 1991, jambo ambalo lilimfanya awe maarufu zaidi.
    Lakini katika mastaajabu ya wengi, Scud hakurejea kwenye kikosi cha Yanga cha mwaka 2002 na huo ukawa mwisho wa umaarufu wake kwenye soka ya Tanzania.
    Kama wapo wanaodhani Scud alifanya kubwa sana katika historia ya watani wa jadi, watakuwa wapo mbali kabisa na ukweli, kwani Kibadeni, maarufu kama Chifu Mputa ama King, au Ndululu kama walivyokuwa wakimuita Wakenya, anaweza kusimama na kusema ana kubwa la kujivunia katika historia ya mechi baina ya Simba na Yanga ambalo hadi kitabu hiki kinaingia sokoni lilikuwa halijavunjwa.
    Kibadeni wa tatu kutoka kushoto katika kikosi cha Simba SC mwaka 1978
    Abdallah Kibadeni ndiye mchezaji pekee hadi sasa aliyeweza kufunga mabao matatu peke yake katika mchezo mmoja kwenye mechi za watani wa jadi katika Ligi.

    Hiyo ilikuwa ni Julai 19, mwaka 1977 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, sasa Uwanja wa Uhuru, wakati Yanga ilipotandikwa 6-0 na Simba.
    Siku hiyo, Kibadeni alitikisa nyavu za Yanga katika dakika za 10, 42 na 89, wakati mabao mengine ya Wekundu wa Msimbazi, yalitiwa kimiani na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika ya 60 na 73 na jingine Selemani Sanga wa Yanga alijifunga mwenyewe dakika ya 20 katika harakati za kuokoa krosi ya Ezekiel Greyson 'Jujuman'.
    Hivyo siku hiyo mbali na Simba kushangilia kulipa kisasi cha kulala 5-0 kwa Yanga, Juni Mosi mwaka 1968, Kibadeni alikuwa ana sherehe binafsi za kutumbukiza tatu peke yake kwenye mechi baina ya watani hao, jambo ambalo liliwashinda wengi kabla yake kati ya waliowahi kuvaa jezi za Simba au Yanga.
    Hakuna cha Sunday Manara 'Computer' wala Maulid Dilunga 'Mexico' aliyewahi kufanya hivyo zaidi ya King Kibadeni pekee ambaye Jumapili ataiongoza timu yake ya zamani kama kocha dhidi ya watani. Sasa baada ya miaka 36 tangu Kibadeni awaokoteshe Yanga mipira nyavuni mara tatu, miamba hiyo inakutana tena Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, je rekodi hiyo itavunjwa? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ACHENI KIBADENI AITWE KING WA SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top