• HABARI MPYA

    Thursday, June 13, 2013

    KIUNGO WA ARSENAL ATISHIA NAFASI YA NIYONZIMA KIKOSINI RWANDA

    Anataka namba ya Niyonzima; Alfred Martins Mugabo ameitwa Amavubi
    Na Bonnie Mugabe, Kigali, IMEWEKWA JUNI 13, 2013 SAA 6:30 MCHANA
    PENGO la Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima katika kikosi cha Rwanda, Amavubi litazibwa na kiungo wa kikosi cha wachezaji wa akiba cha Arsenal, Alfred Martins Mugabo kuelekea mchezo wa Kund H kuwania tiketi ya kucheza Kombe la Dunia Jumapili dhidi ya Algeria kwenye Uwanja wa Amahoro, Kigali.
    Kiungo huyo wa ‘timu ya rizevu’ ya Arsenal, Alfred Martins Mugabo amesema anafurahia kuitwa katika kikosi cha Nyigu wa Rwanda, lakini kocha Eric Nshimiyimana amemuambia mchezaji huyo aliyezaliwa miaka 18 iliyopita kwamba lazima aonyeshe uwezo mazoezini ndio ampange.
    Niyonzima anayechezea Yanga SC ya Dar es Salaam, ambaye pia ndiye Nahodha wa Amavubi anaweza kujikuta anapoteza namba moja kwa moja Rwanda iwapo kinda huyo wa Arsenal atafanya kazi nzuri Jumapili. 
    “Najisikia vizuri, ni mara yangu ya kwanza kuwa nchini baada ya muda mrefu. Ni vizuri kurejea Rwanda na natarajia kuwawakilisha wananchi katika mchezo wa mwishoni mwa wiki,”alisema Mugabo ambaye amefurahia kuona nchi yake ilivyopiga hatua tangu mwaka 1994 baada ya vita ya Wahutu na Watutsi.”
    Benchi linamuita Amavubi? Haruna Niyonzima anakabiliwa na upinzani wa namba na kiungo wa Arsenal

    “Kitu cha kwanza baada ya kusikia nimeitwa timu ya wakubwa ya Amavubi, nilishitushwa sana, kwa sababu mimi ni mdogo, sikutarajia kuitwa, lakini naipokea nafasi hii na nafikiri ni nafasi nzuri kuonyesha nini naweza kuifanyia nchi yangu na ni matumaini yangu nitapewa nafasi.”
    Mugabo alisema; “Nimekuwa Arsenal kwa miaka mitano na nimesaini mkataba mpya. Ninaendelea vizuri na makocha ni wazuri. Nimepandishwa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 21, ambacho ni wachezaji wa akiba na natarajia kupiga hatua zaidi katika msimu mpya.”

    Amesema anawavutia wachezaji wengi Arsenal na ni marafiki wazuri ambao wanawapa matumaini wachezaji chipukizi kupiga hatua waje kuwa wachezaji bora.”
    Anaweza; Mugabo kulia akiichezea Arsenal

    “Jack Wilshere ni mfano mzuri sana wa kuigwa, ananifundisha mengi sana na ni rafiki mzuri,”alisema Mugabo.
    Kiungo huyo wa kimataifa wa England, anayetabiriwa kutikisa ulimwengu wa soka, alidhihirisha kumsapoti kwake Mugabo katika ukurasa wake wa Twitter miezi kadhaa iliyopita.
    Uzoefu utambeba? Haruna Niyonzima ni mzoefu wa michuano mikubwa japokuwa anacheza Afrika
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIUNGO WA ARSENAL ATISHIA NAFASI YA NIYONZIMA KIKOSINI RWANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top