• HABARI MPYA

    Sunday, April 07, 2013

    KASEJA NA GIGI 2001, LEO...


    WAKATI Gianluigi ‘Gigi’ Buffon anatua Juventus ya Turin mwaka 2001 akitokea Parma aliyoichezea tangu mwaka 1995, ndipo Juma Kaseja alikuwa anasajiliwa katika klabu ya Ligi Kuu kwa mara ya kwanza akitokea sekondari ya Makongo, Dar es Salaam. 
    Kaseja alisajiliwa na Moro United baada ya klabu hiyo kuvutiwa na kipa huyo alipokuwa akiidakia timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys wakati ikifundishwa na makocha Mnigeria, Ernest Mokake na mzalendo Juma Matokeyo.

    Makocha hawa wote sasa ni marehemu, enzi hizo walifanya kazi kubwa na nzuri ya kuibua vipaji vingi vya wanasoka kabla na baada ya Kaseja, ambao baadaye walikuwa tegemeo la timu ya taifa, Taifa Stars.
    Kama Kaseja, ni Nahodha wa klabu yake, Simba SC aliyojiunga nayo mwaka 2003 na timu ya taifa, Gigi pia ni Nahodha wa Juve na The Azzuri, timu ya taifa ya Italia.
    Wataliano wanaridhika na kazi ya Gigi na wanamuamini, hata inapotokea amefanya vibaya wanachukulia ni hali ya kimchezo. Hali ni tofauti kwa Kaseja, kuanzia kwa klabu yake Simba SC hadi timu ya taifa.
    Simba SC kila siku wanatafuta kipa mbadala wa Kaseja, maana yake  wanampalilia safari ya kuondoka. Katika timu ya taifa nako, pamoja na Kaseja kufanya kazi nzuri langoni, lakini watu wanataka na makipa na wengine wapewe nafasi.
    Yaani maana yake wamemchoka Kaseja na ikitokea akafanya kosa kidogo, basi hiyo inakuwa ndiyo sababu. Hakuna makipa wengine? Hawazingatii uzoefu wa Kaseja kwamba ni silaha ya ziada anaposimama langoni, achilia mbali uwezo wake mkubwa.
    Lakini pamoja na changamoto zote hizo, bado Kaseja ameendelea kuwa kipa imara akilinda lango la klabu yake Simba SC na Taifa Stars pia. Makocha wanamkubali, ukiondoa Marcio Maximo pekee ambaye wakati akiwa hapa, hakumkubali kabisa kipa huyo, kisa alikuwa anakijua mwenyewe.
    Nchi za wenzetu wachezaji wanaheshimiwa, wanaenziwa kwa kazi wanayofanya kwa ajili ya nchi zao, lakini kwetu wachezaji wanadharauliwa. Wanalazimishwa kuondoka haraka uwanjani na wengine wameondoka mapema kweli.
    Kaseja asingekuwa kipa imara, mvumilivu na mwenye hekima, sasa hivi zamani amebaki historia katika soka ya Tanzania. Lakini unaweza ukajiuliza kwa nini kipa huyu haheshimiwi, hathaminiwi pamoja na mambo makubwa aliyoifanyia nchi hii na klabu yake, Simba SC?
    Ingawa hii inaonekana kuwa desturi ya muda mrefu katika soka ya Tanzania, maana mambo kama haya yaliwatokea hata akina Mwameja Mohamed pia enzi zao, lakini wakati umefika sasa watu wabadilike.
    Tujifunze kuwapenda wachezaji wetu na kutambua jukumu la kuwafanya wacheze muda mrefu ni letu ni sote. Mchezaji wa Tanzania anapambana na changamoto nyingi sana ambazo wachezaji wengine duniani hakika hawapitii.
    Na bado tunajiuliza, kwa nini nchi yetu haina wachezaji wa kucheza Ulaya kama nchi nyingine za Afrka wakiwemo majirani zetu Kenya na Uganda, lakini kwa mazingira yapi tunayomtengenezea mchezaji huyu kulinganisha na wenzetu?
    Kweli wachezaji wetu wana matatizo yao, ulimbukeni likiwa ni kubwa na hilo linachangiwa na makuzi yao holela, yasiyo ndani ya msingi maalum wa kitaalamu, lakini pia wapo baadhi ambao ni afadhili ya wengine, ila bado hawathaminiwi, kwa nini? 
    Tazama unafiki wa shabiki wa soka Tanzania, kuna wakati shabiki wa Simba alikuwa analia; “Emanuel Okwi anahujumu timu yetu, hatumuhitaji aondoke zake,”.. lakini leo Mganda huyo akiwa ameuzwa Etoile du Sahel ya Tunisia,  ndiye anatajwa kama mfano wa wachezaji bora kuwahi kutokea Simba SC.
    Okwi sasa anapumua Tunisia na sidhani kama ana hamu tena na soka ya Tanzania. Lakini desturi hii itaendelea hadi lini? Tubadilike, tuwaheshimu na kuwathamini wachezaji wetu kuanzia sasa. wAsAlAaM.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KASEJA NA GIGI 2001, LEO... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top