• HABARI MPYA

    Thursday, March 28, 2013

    SIMBA SC YATUA MWANZA USIKU HUU KWA BASI IKITOKEA BUKOBA, MUDDE NA DHAIRA KUUNGANA NA TIMU KESHO

    Mussa Mudde aliyeruka, ataungana na timu kesho

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIKOSI cha Simba SC kimewasili mjini Mwanza usiku huu kwa basi kikitokea Bukoba mkoani Kagera, ambako jana kilichapwa 1-0 na wenyeji Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Simba SC imetua Mwanza ajili ya mchezo wake mwingine wa Ligi Kuu dhidi ya Toto Africans ya mjini humo Jumamosi.
    Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, watajifua kesho mjini humo kabla ya mchezo wao huo wa mwisho wa ligi Kanda ya Ziwa Jumamosi, wakiwa na dhamira ya kushinda.
    Simba SC wanakabiliwa na changamoto ya matokeo mabaya katika Ligi Kuu hivi karibuni, kiasi cha kupoteza matumaini ya kutetea ubingwa wao na tayari matumaini ya angalau kushika nafasi ya pili yameanza kufifia baada ya kulala 1-0 kwa Kagera jana.
    Hivi sasa Simba yenye pointi 34 sawa na Kagera Sugar, inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, wakati Azam FC yenye pointi 40 ni ya pili na Yanga yenye 48 ipo kileleni zikiwa zimebaki raundi sita ligi kugota ukingoni.
    Wakati huo huo; wachezaji wawili wa kimataifa wa Uganda wa Simba SC, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde wanatarajiwa kujiunga na timu hiyo mjini Mwanza kesho.
    Wawili hao walikwama Ghana wakiwa njiani kurejea kutoka Liberia walipokwenda na timu yao ya taifa kwa ajili ya mechi dhidi ya wenyeji Liberia kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani.
    Kutokana na Uganda kuondoka kwa mafungu katika Uwanja wa Ndege Accra, walipotua kuunganisha ndege wakitokea Monrovia, ndiyo maana nyota hao wa Simba SC walichelewa na wakakosa mechi ya jana. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC YATUA MWANZA USIKU HUU KWA BASI IKITOKEA BUKOBA, MUDDE NA DHAIRA KUUNGANA NA TIMU KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top