• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 21, 2013

  RAIS JK AMTUPIA KIJEMBE MWANAWE RIDHIWANI NA YANGA YAKE NA WAPINZANI WAO WA JADI SIMBA SC PIA, WAMEBAKI BARAKA YA MASHABIKI TU, AZAM NDIO MPANGO MZIMA

  Rias JK akikata utepe mChamazi leo

  Na Zaituni Kibwana
  RIDHIWANI Kikwete alikuwa anatambulishwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uendelezaji wa Jengo dogo la klabu ya Yanga SC, liliopo wa Mafia mchana wa leo, makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam wakati huo baba yake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa anazindua mradi wa ujenzi wa Uwanja mpya wa kisasa wa klabu ya Azam, huko Chamazi, nje kidogo ya Jiji.
  Katika uzinduzi wa mradi huo, Rais Kikwete ni kama alimtupia kijembe mwanawe Ridhiwani na Yanga yake na wapinzani wao wa jadi, Simba SC kwamba, wamebakia na Baraka ya mashabiki wengi, lakini wamedumaa kimaendeleo.  
  Kikwete, maarufu kama JK kwa ujumla ameziponda Simba na Yanga kwa kushindwa kuwekeza katika michezo na badala yake kuendekeza ushirikina.
  Akizungumza wakati akiweka jiwe la msingi katika Uwanja wa Chamanzi, Kikwete rais kipenzi cha Watanzania wengi aliitaka klabu ya Azam kutokuwa kivuli cha klabu yoyote nchini kama wanataka kufika mbali.
  “Mkikubali tu kuwa kivuli na kuruhusu kufanya kama zinavyofanya klabu kongwe, basi mtakuwa mmepotea, waacheni wafanye wenyewe, nyinyi chezeni mpira,”alisema.
  Ridhiwani akiwa na Hati ya jengo la
  Mafia baada ya kutambulishwa Mwenyekiti wa Kamati
  ya uendelzajki wa jengo hilo leo
  Kikwete aliisifu Azam imevunja ukiritimba wa Simba na Yanga katika soka ya Tanzania.
  “Klabu kubwa zimebaki na baraka ya kuwa mashabiki wengi tu, ila hawana kitu, maana baada ya kuwekeza kiufundi wao wanawekeza kwenye kamati ya ufundi, matokeo yake wanashinda mechi za hapa hapa Tanzania tu,”alisema.
  Rais huyo aliyeongozana na Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meckysadick na viongozi wengine mbalimbali wa Serikali, pia aliipongeza klabu hiyo inayomilikiwa na mfanyabiasha maarufu nchini na familia yake, Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa kwa kuiwakilisha vyema Tanzania kwenye michuano ya Afrika.
  “Simba na Yanga ni wa hapa hapa tu, huku wengine wanasajili kwa kukomoana, ila Azam mmeleta mfano kwa Watanzania,”alisema.
  Kikwete aliifananisha Azam na klabu ya Barcelona ya Hispania kwa kuwekeza vijana na baadaye kuwanunua kwa gharama kubwa.
  “Azam inaweza kuwa kama Barcelona kwa kuwazalisha wakina Messi, kwani wana mtindo wa Ulaya, kwa kuwa hawaendeshi timu kwa kutumia wanachama,”alisema.
  Kikwete aliyehaidi kuongea na wahusika wanaokata kodi ndani ya klabu hiyo ili kuwafanyie ahueni katika mradi huo, alisema kuwa kama soka inachezwa kwa uchawi basi Afrika ingechukua Kombe la dunia mashindano hayo yanapowadia.
  Azam FC ilianzishwa na kikundi cha wafanyakazi wa kampuni ya Mzizima Flour Mill, kampuni tanzu ya Bakhresa, makao yake makuu yakiwa Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam, lengo la wafanyakazi hao wa kampuni inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa, awali ilikuwa ni kucheza kwa ajili ya kujiburudisha, baada ya kazi.
  Lakini baada ya kuona wana timu nzuri, Oktoba 16, mwaka 2004, wafanyakazi hao waliisajili rasmi kwa ajili ya kushiriki Ligi Daraja la Nne, wakitumia jina la Mzizima FC.
  Ilikuwa wanapokwenda kucheza mechi, wanapitisha michango kiwandani kwa wafanyakazi na mabosi, wanakwenda kucheza.
  Baada ya Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya S.S. Bakhresa, Abubakar Bakhresa, aliona ni vyema timu hiyo ihusishe wafanyakazi wa kampuni zote za Bakhresa, na kutumia jina la moja ya bidhaa zao kubwa, Azam.
  Kampuni nyingine za Bakhresa ni Food Products Ltd, Azam Bakeries Ltd, Omar Packaging Industries Ltd na kadhalika. 
  Wazo lake lilikubaliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndipo timu hiyo ikaanza kuitwa Azam SC, badala ya Mzizima. Lakini baadaye Juni 11, mwaka 2007, ilibadilishwa jina tena na kuwa Azam FC. 
  Azam ilikwenda kwa kasi nzuri kuanzia Daraja la Nne na hadi mwaka 2008, ilifanikiwa kucheza Ligi Kuu, ikipandishwa na makocha King, aliyekuwa akisaidiwa na Habib Kondo. Baada ya kupanda, Azam ilimuajiri kocha wa zamani wa Simba SC, Mbrazil Neider dos Santos, aliyekuwa akisaidiwa na Sylvester Marsh na Juma Pondamali upande wa kuwanoa makipa.
  Baadaye ilimuongeza kocha wa viungo, Itamar Amorin kutoka Brazil pia, ambaye awali ya hapo alikuwa msaidizi wa Marcio Maximo katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
  Amorin baaaye akawa kocha Mkuu Azam FC baada ya kufukuzwa Marcus Tinocco. Amorin naye aliondoka ndipo akaja kocha wa sasa, Muingereza Stewart Hall. Hall alifukuzwa Agosti mwaka jana akaajiriwa Mserbia, Boris Bunjak ambaye alifukuzwa Oktoba mwaka jana na kurejeshwa Hall.
  Hadi sasa Azam ina mataji matatu katika kabati lake, mawili ya Kombe la Mapinduzi na moja la Kombe la Hisani walilotwaa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwishoni mwa mwaka jana.
  Ikiwa inashiriki michuano ya Afrika kwa mara ya kwanza mwaka huu, Azam FC imeonyesha dalili za kufika mbali kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kufika Raundi ya Pili na kuanza vyema katika mchezo wa kwanza, ikishinda ugenini 2-1 dhidi ya Barack Young Controllers II nchini Liberia.
  Katika Raundi ya Kwanza, Azam FC iliitoa Al Nasr Juba ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1, ikiifunga 3-1 Dar es Salaam na 5-0 Sudan Kusini.
  Azam sasa inahitaji sare katika mchezo wa marudiano na B.Y.C. wiki ijayo ili kusonga mbele. Simba na Yanga zipo tangu miaka ya 1930, lakini zaidi ya majengo yake waliyojenga kwa msaada wa rais wa zamani wa Zanzibar, Hayati Abeid Amaan Karume na kutawala soka ya Tanzania, hazina cha kujivunia- sana baraka ya mashabiki kama alivyosema rais JK leo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: RAIS JK AMTUPIA KIJEMBE MWANAWE RIDHIWANI NA YANGA YAKE NA WAPINZANI WAO WA JADI SIMBA SC PIA, WAMEBAKI BARAKA YA MASHABIKI TU, AZAM NDIO MPANGO MZIMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top