• HABARI MPYA

    Wednesday, March 27, 2013

    SAFARI BADO NDEFU, TOFAUTI NA TUNAVYOFIKIRIA


    TIMU ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania Jumamosi iliibwaga Morocco mabao 3-1 katika mchezo wa Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.
    Na Bin Zubeiry
    Shukrani kwao, washambuliaji wawili wanaochezea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbwana Ally Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu waliofunga mabao hayo leo.
    Samatta alifunga mawili na Ulimwengu aliyetokea benchi dakika ya 46 kuchukua nafasi ya Mwinyi Kazimoto Mwitula alifunga moja.
    Kwa matokeo hayo, Stars inaendelea kushika nafasi ya pili katika Kundi C kwa pointi zake sita, nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kwa pointi zake saba, baada ya jana kushinda 3-0 dhidi ya Gambia.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa kutoka Angola Helder Martins aliyesaidiwa na ndugu zake, Inacio Manuel na Ricardi Daniel washika vibendera, hadi mapumziko hakukuwa na bao.
    Kipindi cha pili, Stars walianza na mabadiliko, kocha Mdenmark Kim Poulsen akimtoa Kazimoto na kumuingiza Ulimwengu aliyekwenda kubadilisha kabisa mchezo.
    Katika dakika ya 46, mpira wa kwanza kuugusa Thomas Ulimwengu ambao alirushiwa na beki Erasto Nyoni aliunganisha nyavuni na kuipatia Stars bao la kwanza.
    Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo kwa upande wa Stars na katika dakika ya 67, Samatta alifunga bao la pili akimchambua kipa Nadir Lamyaghri baada ya kupokea pasi nzuri ya Ulimwengu ambaye naye alipasiwa na Athumani Iddi ‘Chuji’ aliyetokea benchi pia.
    Morocco walionekana kuchanganyikiwa baada ya bao la pili na kuruhusu Stars kutawala zaidi mchezo.
    Zilikuwa zinapigwa pasi zisizo na idadi, ili mradi burudani kwa mashabiki wa soka wa Tanzania waliyokuwa wakipatiwa na wachezaji wa timu yao.
    Lakini katika mtindo huo huo, Stars ilikuwa inatengeneza mashambulizi ya kushitukiza yaliyosababisha kosakosa kadhaa langoni mwa Morocco.
    Hata hivyo, kazi nzuri ya Ulimwengu aliyepambana na beki wa Morocco na kumzidi nguvu hatimaye kufanikiwa kupiga krosi, liliipatia Stars bao la tatu lililounganishwa kimiani na Samatta dakika ya 80.
    Beki Abderrahim Achchakir alipewa kadi nyekundu kwa kumtolea kauli chafu refa baada ya Stars kufunga bao la tatu. Beki huyo alikuwa kama analalamika kuchezewa rafu na Uli wakati akipiga krosi ya bao.
    Burudani iliongezeka baada ya bao hilo, Stars wakigonga pasi nyingi- hata hivyo kosa kidogo la safu ya ulinzi liliipa nafasi Morocco kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Yousef Elarabi aliyetokea benchi. 
    Baada ya mchezo huo, kocha wa Tanzania, Mdenmark Kim Poulsen alisema kwamba amefurahia matokeo na anawapongeza vijana, lakini bado ana kazi ngumu katika mechi tatu zijazo dhidi ya Morocco na Gambia ugenini na Ivory Coast nyumbani. 
    Mapema tu kocha Kim Poulsen alisema lengo lake ni kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2015 na kuelekea Brazil anashindana tu ili kuijengea timu uwezo wa kupigania tiketi za michuano ya bara hili.
    Lakini kulingana na mwenendo wa timu hivi sasa, yote yanawezekana hata kwenda Brazil. Stars ni ya pili nyuma ya Ivory Coast, ikizidiwa pointi moja. Stars imefungwa mechi moja tu na Ivory Coast ugenini. Tembo watakuja hapa kumenyana na sisi Juni, ina maana tukijipanga vyema tukashinda, na kama matokeo yetu na Morocco katika mchezo wa marudiano yatakuwa mazuri ugenini, tunaweza kuwapiku.
    Nafasi ya kwenda Brazil tunayo. Huo ndio ukweli. Kitu kimoja tu ambacho wengi hawaelewi ni kwamba, tukifanikiwa kuongoza kundi C, si maana yake tumekata tiketi ya Brazil, bali tutakuwa tumeingia hatua ya mwisho ya mchujo kuelekea fainali hizo.
    Kwani baada ya hatua ya makundi, vinara wa makundi yote 10 Afrika watapangiwa mechi baina yao, nyumbani na ugenini na timu tano zitakazopata matokeo mazuri kwa ujumla, ndizo zitakwenda Brazil.
    Tulikua hatuiamini timu yetu tangu mwanzo na kwa kiasi kikubwa tulijihesabu washiriki tu ila sasa wengi wetu ikiwemo Serikali inaamini tunashindana. Hivyo, basi ipo haja ya Watanzania kushikamana kuipa sapoti timu yetu iweze kutimiza ndoto zetu.
    Kimzaha mzaha, Angola walicheza Kombe la Dunia mwaka 2006 Ujerumani- basi nasi kama kweli kwa pamoja, TFF, Serikali, Vyombo vya Habari, Klabu na wananchi tutaipa sapoti timu yetu, inaweza kwenda Brazil. Ila ukweli ni huo, safari bado ndefu, tukaze buti. Wasalam.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SAFARI BADO NDEFU, TOFAUTI NA TUNAVYOFIKIRIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top