• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 26, 2013

  DHAIRA NA MUDDE WAKWAMA GHANA WAKIREJEA KUTOKA LIBERIA, KUIKOSA KAGERA SUGAR LEO KAITABA

  Abbel Dhaira; Tatizo nini?

  Na Mahmoud Zubeiry
  WACHEZAJI wawili wa Simba SC, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde hawatashiriki mechi ya kesho ya klabu yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kutokana na kukwama nchini Ghana.
  Wawili hao, walikuwa Liberia mwishoni mwa wiki na timu ya taifa ya Uganda, The Cranes iliyokwenda kumenyana na wenyeji wao hao katika mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.
  Hata hivyo, wakiwa njiani kurejea nchini kujiunga na klabu yao, imeelezwa kwamba wamekwama Ghana.
  “Wamekwama Ghana,”alisema Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga alipozungumza na BIN ZUBEIRY jioni hii, ingawa hakuwa tayari kueleza kwa undani juu ya kilichowakwamisha wachezaji hao.
  Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea kesho kwa mechi mbili, mabingwa watetezi Simba wakiwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
  Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 3,000 unatarajiwa kushuhudia mechi yenye ushindani mkali kutokana na uwezo wa wachezaji wa pande zote mbili.
  Mechi nyingine itapigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam kati ya wenyeji Azam na Tanzania Prisons kutoka Mbeya.
  Tayari wachezaji wa Simba SC waliokuwa na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliyomenyana na Morocco mjini Dar es Salaam Jumapili na kushinda 3-1 wapo Bukoba kwa ajili ya mchezo huo.
  Hao ni kipa na Nahodha, Juma Kaseja, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Shomary Kapombe na viungo Mrisho Ngassa na Amri Kiemba.
  Kiungo mwingine wa Simba SC aliyekuwa na Taifa Stars Jumapili, Mwinyi Kazimoto yeye hajaenda Bukoba kwa sababu hayumo kwenye mipango ya kocha Mfaransa, Patrick Liewig kwa sasa.
  Simba SC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa kwa pointi zake 34, ikiwa nyuma ya Azam yenye pointi 37, wakati Yanga SC yenye pointi 48 inaongoza ligi hiyo.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: DHAIRA NA MUDDE WAKWAMA GHANA WAKIREJEA KUTOKA LIBERIA, KUIKOSA KAGERA SUGAR LEO KAITABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top