• HABARI MPYA

    Saturday, March 23, 2013

    RAGE APOKEWA KIFALME SIMBA SC AKITOKEA INDIA ALIPOKUWA ANATIBIWA

    Wanachama wakisukuma gari la Rage jana
    Na Princess Asia
    MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Alhaj Ismail Aden Rage amerejea jana jioni mjini Dar es Salaam akitokea India alikokuwa akitibiwa na kuzusha tafrani Uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam.
    Kuna makundi mawili ya wanachama wa Simba SC, yaliyofika uwanjani hapo kumpokea kiongozi wao huyo.
    Kundi la kwanza ni lile linalompinga na lingine linalomuunga mkono. Wanaompiga walifika na mabango ya kumtaka ajiuzulu, wakati wanaomuunga mkono walimpokea kwa shangwe na vigelegele.
    Hata hivyo, kundi la wanaompinga Rage lilizidiwa nguvu na wanaomuunga mkono na kuondoka katika eneo hilo.
    Wanachama walikuwa wengi waliojitokeza kumlaki Rage, walikuja na mabasi matatu aina ya Coaster, wagon moja, gari ndogo aina ya salon tatu na pikipiki mbili.   
    Walikuwa wamebeba mabango yaliyoandikwa ujumbe wenye kuashiria wana imani na kiongozi wao huyo na kwamba wanaompiga ni adui zake wanaokerwa na jinsi alivyodhibiti mali za klabu.
    Mara alipotokeza kutokea lango la ‘watu muhimu sana’, yaani VIP, Rage ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), alilakiwa na wanachama hao ambao walisukuma gari lake kuelekea makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam. Shughuli ilipendeza.
    Jumapili iliyopita wanachama 698 wa klabu ya Simba walifikia uamuzi wa kuuondoa madarakani uongozi wa klabu yao chini ya Rage na kuunda Kamati Maalum ya Muda, wakiwateua Zacharia Hans Poppe na Rahma Al Kharoos au Malkia wa Nyuki kwa jina la utani kuiongoza.
    Katika Mkutano uliofanyika kwenye ukumbi maarufu wa Star Light Cinema, Dar es Salaam, wanachama hao walifikia uamuzi wa pamoja kuuondoa madarakani uongozi huo, kutokana na kile kilichoelezwa kushindwa kutekeleza majukumu yao na kuifikisha timu pabaya.
    Kwa upande wake, Hans Poppe, kwanza alisema hana taarifa za Mkutano huo wala yaliyofikiwa.
    “Sina taarifa na wala siafiki, kwa sababu hakuna mtu aliyeshauriana na mimi kabla, na pia wamefanya mambo kinyume na Katiba,”alisema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
    “Lazima wanachama wawe na subira, wasubiri Mwenyekiti arudi aitishe mwenyewe Mkutano, yeye mwenyewe (Mwenyekiti) alikwishasema ataitisha Mkutano, sasa kitu gani kinachowafanya wao wanakosa subira,”.
    “Mbaya zaidi wamekwenda kufanya Mkutano wao na kufikia maamuzi yao, bila hata kunitafuta kuniuliza kwanza, sasa hii si ni dharau? Ina maana wao wanataka mimi nifanye wanavyotaka wao, mimi sitaki kuwa sehemu ya migogoro katika Simba,” alisema Hans Poppe. 
    Naye Malkia wa Nyuki, alisema kwamba hatambui uteuzi wake huo kwa sababu anafikiria zaidi vita ya kuinusuru timu katika wakati huu mgumu.
    Malkia ambaye alisema alikuwa safarini wakati mapinduzi hayo yanafanyika mwishoni mwa wiki, alisema haelewi nini dhamira ya kutajwa kwake katika mkutano ule uliotishwa kinyume cha Katiba ya Simba SC.
    “Hawa watu kama wangekuwa wana nia nzuri na Simba au mimi, wangenihusisha katika mambo yao, lakini hawakunihusisha na wanakwenda kutaja jina langu bila kuwasiliana na mimi. Kwa kweli sijapenda,”alisema.
    Hata hivyo, Malkia alisema hataki kuzungumzia zaidi mambo hayo kwa sasa, kwa kuwa kichwa chake kimetingwa na majukumu ya kuinusuru timu.
    “Hapa najipanga kwa mechi za Kanda ya Ziwa, nataka tuchukue pointi sita za Kanda ya Ziwa tujiweke sawa. Hata kama hatuwezi kupata ubingwa, lakini lazima tupate nafasi ya pili,”alisema.
    Aidha, Mama Al Kharoos amesistiza huu si wakati mwafaka kwake kuzungumzia siasa za klabu au migogoro, bali anataka asikie kuhusu kuiwezesha Simba kutetea ubingwa au kushika nafasi ya pili.
    Kwa ujumla, hamkani si shwari sasa ndani ya Simba SC, kufuatia viongozi wawili wa Kamati ya Utendaji, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Hans Poppe aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili  kujiuzulu wiki mbili zilizopita.
    Walijiuzulu wakati Rage yuko India kwa matibabu na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Joseph Itangare ‘Kinesi’ aliyeteuliwa kukaimu Umakamu Mwenyekiti, ndiye akawa anakaimu Uenyekiti wa klabu.
    Aidha, Baraza la Wazee kwa pamoja na Baraza la Wadhamini, waliunda Kamati Maalum ya kusimamia timu kuhakikisha inafanya vizuri katika wakati huu mgumu, chini ya Mwenyekiti, Malkia wa Nyuki.
    Malkia wa Nyuki alianza vyema baada ya kuiongoza Simba SC kuilaza 2-1 Coastal Union katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu na sasa anajiandaa kwenda kucheza mechi ya pili, dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba Jumatano ijayo.
    Rage akihutubia makao makuu ya klabu jana
    Simba SC ambao ni mabingwa watetezi, kwa sasa inazidiwa kwa pointi 14 na Yanga SC, inayoongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 48, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 37. Simba ya tatu.
    KUNRADHI: Kutokana na matatizo ya mtandao, tumeshindwa kuwaletea picha za matukio ya kuwasili kwa Rage jana. Aidha pia imesababisha kuchelewa kwa habari hii.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: RAGE APOKEWA KIFALME SIMBA SC AKITOKEA INDIA ALIPOKUWA ANATIBIWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top