• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 29, 2013

  DHAIRA, MUDDE SASA PASUA KICHWA SIMBA SC, BABU MFARANSA KATIKA WAKATI MGUMU ZAIDI KESHO NA TOTO LA YANGA

  Kocha Liewig kulia akitoa maelekezo kwa Nahodha wa kikosi chake, Juma Kaseja

  Na Mahmoud Zubeiry
  WANASOKA wawili wa kimataifa wa Uganda, wanaochezea Simba SC, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde hawatakuwepo katika mchezo wa kesho wa timu yao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania dhidi ya wenyeji Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, BIN ZUBEIRY imeipata hiyo.
  Wawili hao, walitarajiwa kuwasili Mwanza leo kuungana na wenzao, lakini hawajafika na Ofisa Habari wa Wekundu hao wa Msimbazi, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba hawatawahi mchezo wa kesho.
  “Mudde na Dhaira hawatawahi mechi ya kesho,”alisema Ezekiel, maarufu Mr. Liverpool.
  Amri Kiemba; Ataiongoza Simba SC kesho

  REKODI YA LIEWIG SIMBA SC:
                           P W D L GF GA GD Pts
  Simba 19 7 5 7 23 22 1 26

  MECHI ZA SIMBA CHINI YA LIEWIG:
  Simba SC 4-2 Jamhuri             (Kombe la Mapinduzi)
  Simba SC 1-1 Tusker FC        (Kombe la Mapinduzi)
  Simba SC 1-1 Bandari             (Kombe la Mapinduzi)
  Simba SC 0-1 U23 Oman        (Kirafiki)
  Simba SC 1-3 Qaboos             (Kirafiki)
  Simba SC 2-1 Ahly Sidab         (Kirafiki)
  Simba SC 0-1 Black Leopard  (Kirafiki)
  Simba SC 3-1 African Lyon      (Ligi Kuu)
  Simba SC 1-1 JKT Ruvu           (Ligi Kuu)
  Simba SC 1-1 JKT Oljoro      (Ligi Kuu)
  Simba SC 0-1 Rec. de Libolo  (Ligi ya Mabingwa)
  Simba SC 1-0 Prisons              (Ligi Kuu)
  Simba SC 0-1 Mtibwa Sugar   (Ligi Kuu)
  Simba SC 0-4 Rec. de Libolo  (Ligi ya Mabingwa) 
  Simba SC 2-1 Coastal Union   (Ligi Kuu)
  Simba SC 1-0 CDA       (Ligi Kuu)
  Simba SC 4-0 Singida United  (Kirafiki)
  Simba SC 1-1 Rhino FC       (Kirafiki)
  Simba SC 0-1 Kagera Sugar    (Kirafiki)

  Waganda hao walikwama Ghana wakiwa njiani kurejea kutoka Liberia walipokwenda na timu yao ya taifa kwa ajili ya mechi dhidi ya wenyeji Liberia kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani.
  Kutokana na Uganda kuondoka kwa mafungu katika Uwanja wa Ndege Accra, walipotua kuunganisha ndege wakitokea Monrovia, ndiyo maana nyota hao wa Simba SC walichelewa na wakakosa mechi ya Jumamosi dhidi ya Kagera Sugar, ambayo Simba SC ilipigwa 1-0. 
  Kuchelewa kwa wawili hawa, zaidi kunazidi kumuweka katika wakati mgumu, kocha Mfaransa, Patrick Liewig, kwani tayari anakosa wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza kwa sababu tofauti.
  Liewig ameamua mwenyewe aliamua kuwaengua katika programu yake wachezaji kadhaa nyota wa kikosi cha kwanza kama Mwinyi Kazimoto, Amir Maftah, Paul Ngalema, Juma Nyosso, Abdallah Juma, Felix Sunzu, Komabil Keita na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kutokana na kutoridhishwa na nidhamu yao.
  Lakini wakati huo huo, kiungo Kiggi Makassy ni majeruhi na anatakiwa kwenda kufanyiwa upasuaji India.
  Kwa sasa, kikosi cha Simba kinasukwa zaidi na nyota waliopandishwa kutoka timu ya pili, Simba B ambao hata hivyo wameonyesha uwezo mkubwa siku za karibuni.
  Makinda hao wanaongezewa nguvu na wachezaji wachache waliobaki kutoka kikosi cha kwanza kama kipa Juma Kaseja, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Shomary Kapombe, viungo Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.
  Mwenendo wa Liweig anayesaidiwa kazi na beki wa zamani wa klabu hiyo, Jamhuri Kihwelo si mzuri Simba SC na zaidi inachangiwa na mazingira magumu anayofanyia kazi kwa sasa, ameikuta timu ipo ovyo na klabu inakabiliwa na mgogoro.
  Hata hivyo, wengi wanaridhiswa na kazi anayoifanya kocha huyo wa zamani wa akademi ya PSG ya Ufaransa na klabu ya ASEC Abidjan ya Ivory Coast.
  Hadi sasa, Liewig amekwishaiongoza Simba SC katika mechi 19, akiiwezesha kushinda mechi saba na kufungwa saba, sare tano tangu asaini mkataba Januari mwaka huu.
  Simba SC hivi sasa inaelekea kukosa ‘mwana hata maji ya moto’, kwani Yanga ipo katika nafasi nzuri ya ubingwa kwa pointi zake 48, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 40, wakati Wekundu hao wa Msimbazi wana pointi 34 sawa na Kagera Sugar.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: DHAIRA, MUDDE SASA PASUA KICHWA SIMBA SC, BABU MFARANSA KATIKA WAKATI MGUMU ZAIDI KESHO NA TOTO LA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top