• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 29, 2013

  KIGGI MAKASY AUMIA VIBAYA GOTI, ITABIDI AKAPIGWE KISU INDIA

  Kiggi; Kisu kinamsubiri India

  Na Mahmoud Zubeiry
  KIUNGO wa Simba SC, Kiggi Makassy atahitaji kufanyiwa upasuaji wa goti nchini India kutokana na kuumia katika mchezo wa kirafiki dhidi ya CDA mjini Dodoma wiki iliyopita. 
  Daktari wa Simba SC, Cossmas Kapinga ameaimbia BIN ZUBEIRY leo kwamba, kiungo huyo mwenye mashuti makali, alichanika nyama za katikati ya goti ambazo suluhisho lake ni upasuaji tu.
  “Ameumia meniscus tear ya goti la kulia, yaani kwenye goti, kuna mfupa wa juu na chini, sasa katikati kuna nyama, ndiyo hizo za Kiggi zimechanika na sasa kuna utaratibu unafanywa aende kufanyiwa upasuaji India,”alisema Kapinga.
  Kuumia kwa Kiggi ni pigo kwa Simba S katika kipindi hiki ambacho inakabiliwa na changamoto ya japo kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu.
  Aidha, kwa Kiggi pia ni mwendelezo wa mwanzo wake mbaya katika klabu hiyo aliyojiunga nayo msimu huu akitokea kwa mahasimu, Yanga SC.
  Kikosi cha cha Simba SC kiliwasili mjini Mwanza usiku jana kwa basi kikitokea Bukoba mkoani Kagera, ambako juzi kilichapwa 1-0 na wenyeji Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Simba SC ilitua Mwanza ajili ya mchezo wake mwingine wa Ligi Kuu dhidi ya Toto Africans ya mjini humo kesho.
  Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, watajifua leo mjini humo kabla ya mchezo wao huo wa mwisho wa ligi Kanda ya Ziwa Jumamosi, wakiwa na dhamira ya kushinda.
  Simba SC wanakabiliwa na changamoto ya matokeo mabaya katika Ligi Kuu hivi karibuni, kiasi cha kupoteza matumaini ya kutetea ubingwa wao na tayari matumaini ya angalau kushika nafasi ya pili yameanza kufifia baada ya kulala 1-0 kwa Kagera juzi.
  Hivi sasa Simba yenye pointi 34 sawa na Kagera Sugar, inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, wakati Azam FC yenye pointi 40 ni ya pili na Yanga yenye 48 ipo kileleni zikiwa zimebaki raundi sita ligi kugota ukingoni.
  Wakati huo huo; wachezaji wawili wa kimataifa wa Uganda wa Simba SC, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde wanatarajiwa kujiunga na timu hiyo mjini Mwanza leo.
  Wawili hao walikwama Ghana wakiwa njiani kurejea kutoka Liberia walipokwenda na timu yao ya taifa kwa ajili ya mechi dhidi ya wenyeji Liberia kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani.
  Kutokana na Uganda kuondoka kwa mafungu katika Uwanja wa Ndege Accra, walipotua kuunganisha ndege wakitokea Monrovia, ndiyo maana nyota hao wa Simba SC walichelewa na wakakosa mechi ya juzi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KIGGI MAKASY AUMIA VIBAYA GOTI, ITABIDI AKAPIGWE KISU INDIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top