• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 19, 2013

  STARS NA SIMBA WA ATLASI BUKU TANO 'KAJAMBA NANI'

  Taifa Stars

  Na Dina Ismail
  KIINGILIO cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania, Taifa Stars na Morocco, Simba wa Atlas, itakayochezwa Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa ni Sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
  Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Idadi ya viti vya kijani katika Uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 ni 19,648. 
  Wambura amesema kwa upande wa viti vya rangi ya bluu, ambavyo viko 17,045 kiingilio kitakuwa ni Sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni Sh. 10,000.
  Amesema kwa upande wa viingilio vya daraja la juu, VIP C inayochukua watazamaji 4,060 itakuwa ni Sh. 15,000 wakati Sh. 20,000 kwa VIP B yenye watazamaji 4,160 na VIP A inayokusanya watazamaji 748 kiingilio chake kitakuwa ni Sh. 30,000.
  Amesema tiketi kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9:00 alasiri zitaanza kuuzwa siku mbili kabla ya mchezo huo, yaani Ijumaa katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, Mgahawa wa Steers ulioko makutano ya mitaa ya Ohio na Samora, Oil Com Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala.
  Ofisa Habari huyo, amesema katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu, ambayo pia yatafanya mauzo ya tiketi hizo uwanjani siku ya mechi. 
  “Vilevile tunapenda kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika, ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo,”alisema Wambura.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: STARS NA SIMBA WA ATLASI BUKU TANO 'KAJAMBA NANI' Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top