• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 28, 2013

  KIM POULSEN; ‘LESO’ INAYOFUTA MACHOZI YA WATANZANIA

  Wakati wa furaha; Wachezaji wa Stars wakishangilia dhidi ya Morocco

  Na Mahmoud Zubeiry
  MWISHONI mwa wiki, timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilipata ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Morocco katika mchezo wa Kundi C, kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.
  Ushindi huo umeleta faraja kubwa kwa Watazania na kwa mara ya kwanza, baada ya muda mrefu, kurasa za michezo za magazeti ya Tanzania zinapambwa na habari njema kuhusu Taifa Stars.
  Kim; Amewafuta machozi Watanzania  REKODI YA KIM POULSEN STARS
                    P W D L GF GA  GD Pts
  Tanzania 10 5 3 2 13 10 3 18

  MECHI ZA STARS CHINI YA KIM POULSEN:
  Mei 26, 2012
  Tanzania 0 – 0 Malawi (Kirafiki)
  Juni 2, 2012
  Ivory Coast 2 – 0 Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
  Juni 10, 2012
  Tanzania 2 – 1 Gambia (Kufuzu Kombe la Dunia)
  Juni 17, 2012
  Msumbiji 1 – 1 Tanzania  (Tanzania ilitolewa kwa 
  penalti kufuzu Mataifa ya Afrika)
  Agosti 15, 2012
  Botswana 3 – 3 Tanzania (Kirafiki)
  Novemba 14, 2012
  Tanzania 1-0 Kenya (Kirafiki)
  Desemba 22, 2012
  Tanzania 1-0 Zambia (Kirafiki)
  Januari 11, 2013
  Tanzania 1-2 Ethiopia (Kirafiki)
  Februari 6, 2013
  Tanzania 1-0 Cameroon (Kirafiki)
  Machi 22, 2013
  Tanzania 3-1 Morocco (Kufuzu Kombe la Dunia)

  Ni mageuzi makubwa, kutoka Stars kichwa cha mwendawazimu, Stars fungu la kukosa na Stars ovyo kabisa- hadi Stars lulu.
  Nani anastahili pongezi hizi?   
  Si mwingine zaidi ya Kocha Mdenmark, Kim Poulsen aliyezaliwa Machi 22, mwaka 1959 nchini Denmark.
  Kim, alianza kazi Taifa Stars Mei mwaka jana akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.
  Hadi sasa, Kim amekwishaiongoza Taifa Stars katika mechi 10 na kati ya hizo ameshinda tano, sare tatu na kufungwa mbili, akiiwezesha timu hiyo kufunga mabao 13 katika mechi hizo, na kufungwa 10 tu. 
  Yaani amekusanya wastani wa pointi 18 katika mechi zote hizo, hivyo kusaidia mno kuipandisha katika viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hadi sasa nafasi ya 119 kutoka 127 wakati anaanza kazi. 
  Mafanikio haya hayakuja hivi yametokana na kazi nzuri yenye kuonekana anayoifanya Kim katika kutengeneza timu.
  Uwajibikaji wa uhakika, sera na falsafa nzuri ya ufundishaji, mafunzo bora na kusimamia nidhamu haswa ndiyo siri ya mafanikio ya Kim. 
  Kabla ya kuja Tanzania, timu maarufu aliyoifundisha Kim ilikuwa ni Viborg FF ambayo aliiwezesha kutwaa Kombe la Denmark mwaka 2000.
  Poulsen hakucheza soka kwa kiwango cha juu sana, kwani aliishia kuwa mchezaji wa ridhaa tu.
  Lakini akiwa kocha, ameata heshima ya kitaifa na kimataifa, kwani awali aliiongoza Aarhus Fremad kupanda Ligi Kuu. 
  Aliifundisha pia AC Horsens kutoka 1996 hadi 1997 kabla ya kurejea Aarhus Fremad mwaka 1998. 
  Aliifundisha AC Horsens tena mwaka 1999, kabla hajatimkia Viborg FF mwaka huo huo. Chini ya Poulsen, Viborg FF iligeuka kuwa klabu kamili ya kulipwa na kutwaa Kombe la Denmark mwaka 2000 pamoja na Super Cup ya Denmark. 
  Oktoba mwaka 2001, Poulsen alifukuzwa, akahamia Randers FC na Deaemba mwaka 2002, Poulsen akatimkia Singapore, ambako alipewa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa 18, The Young Lions, yaani Simba Watoto na baadaye klabu ya jeshi la nchini hiyo, Singapore Armed Forces FC. 
  Alirejea Denmark kujiunga na klabu ya Vejle Boldklub mwezi Januari mwaka 2006 kwa mkataba wa miaka mitatu, kabla ya kutupiwa virago Aprili mwaka 2007, kisha akaenda kujiunga na Naetved BK Julai mwaka 2007.
  Juni mwaka 2010 alitajwa kuwa Kocha wa FC Hjorring, ambayo aliachana nayo Aprili mwaka 2011 na kuingia mkataba na Tanzania kwa ajili ya kufundisha timu za vijana, kabla ya Mei mwaka jana kupandishwa timu ya wakubwa.
  Kim sasa ni kipenzi cha wapenzi wa soka Tanzania kwa kazi nzuri aliyowafanyia ndani ya muda mfupi.
  Timu inacheza soka ya kuvutia na ya ushindani, si ya waoga woga, kujihami zaidi kama ilivyokuwa enzi za makocha wengine. Stars ya sasa inacheza soka hadi wapinzani wanapoteana uwanjani.
  Stars inatia matumaini. Mwenyewe amekwishasema, nia yake haswa ni kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2015, lakini kwa mwenendo wa timu katika Kundi C kwenye kinyang’anyiro cha tiketi ya Kombe la Dunia hivi sasa, yote yanawezekana. Asante Kim. Wewe yeye ndiye ‘leso’ ya kufuta machozi ya Watanzania.  
  Kim kushoto akizungumza na Waandishi wa Habari. Kulia ni Nahodha Juma Kaseja

  WASIFU WAKE:
  JINA: Kim Poulsen
  KUZALIWA: Machi 22, 1959 (Miaka 53)
  ALIPOZALIWA: Denmark
  KAZI: Tanzania (Taifa Stars)
  NAFASI: Kocha Mkuu
  MUDA: Tangu Mei 2012
  TIMU ZA AWALI:
  Mwaka Timu
  1987-1995 Aarhus Fremad
  1996-1997 AC Horsens
  1998         Aarhus Fremad
  1999         AC Horsens
  1999-2001 Viborg FF
  2002         Randers FC
  2003        Singapore U-18
  2004        Young Lions (Singapore U-23)
  2005         Singapore Armed Forces FC
  2006-2007 Vejle Boldklub
  2007-2010 Naetved Boldklub
  2010-2011 FC Hjorring
  2011-2012 Tanzania u-21
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KIM POULSEN; ‘LESO’ INAYOFUTA MACHOZI YA WATANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top