• HABARI MPYA

    Tuesday, March 19, 2013

    YANGA WAMBAINI MCHAWI 'ANAYEMLOGA' KAVUMBANGU

    Didier Kavumbangu hapa anapiga hewa badala ya mpira

    Na Mahmoud Zubeiry
    UONGOZI wa Yanga, umejiridhisha kushuka kwa kiwango cha mshambuliaji wake wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu kumetokana na mchezaji huyo kuendekeza anasa kupita kiasi.
    Kiongozi mmoja wa Yanga, aliyezungumza na BIN ZUBEIRY bila kutaka kutajwa jina lake, alisema kwamba Kavumbangu amelewa mafanikio aliyoanza nayo katika klabu hiyo na kuangukia kuwa ‘muumini’ wa anasa kiasi cha kushusha kiwango chake.
    “Kwa kweli hii hali inasikitisha sana, Kavumbangu amekuwa mtu wa anasa, ile nidhamu aliyokuwa nayo wakati anaingia hapa, haipo tena. Amekuwa mtu fulani kiburi kidogo,”.
    “Nadhani hii imetokana na mafanikio aliyoanza nayo hapa, alifanya vizuri mzunguko wa kwanza, lakini anasahau kwamba ile ilitokana na juhudi zake mazoezini, akawa fiti akawa anaweza kufanya vizuri.”alisema kiongozi huyo.
    Mzee wa Bata: Didier Kavumbangu
    Alipoulizwa kama wamejaribu kuzungumza naye mchezaji huyo, kiongozi huyo alisema; “Tunazungumza naye sana. Mimi leo hii (juzi) nimetoka kuzungumza naye, yeye anasema anasingiziwa, wakati watu wanamuona wanatupigia simu na tunakwenda kuthibitisha, amekuwa mtu wa dansi, pombe, wanawake hadi anaimbwa kwenye mabendi ya kikongo”.
    “Tazama alivyocheza mechi na Ruvu, yaani alikuwa hawezi hata kutuliza mpira, akiguswa kidogo anaanguka, sasa pale utasema analogwa? Mwili wake hauko vizuri na akili yake haipo uwanjani, atawezaje kufanya vizuri,”aliongeza.
    Alipoulizwa kuhusu mustakabali wa mshambuliaji huyo, kiongozi huyo alisema; “Inaumiza kichwa, ila kama hatabadilika kwa kipindi kilichobaki kuelekea kumaliza msimu, tutamuuza au tutamtoa kwa mkopo, ili tusajili mtu mwingine, maana kwa sasa hana msaada katika timu,”alisema.
    Kuhusu kufanya vibaya kwa washambuliaji wengine, kiongozi huyo alisema Said Bahanuzi anasumbuliwa na maumivu hajapona sawasawa, Hamisi Kiiza ameanza kufufua makali na Jerry Tegete anafanyia kazi kwa bidii mapungufu yake.
    “Kuna hali fulani ambayo inajitokeza kwenye timu ambayo hata sisi inatuchanganya, yaani tunatengeneza nafasi nyingi, lakini mwisho wa siku tunafunga bao moja. Hili mwalimu ameanza kulifanyia kazi, nadhani hali itabadilika,”alisema.
    Kavumbangu alimaliza mzunguko wa kwanza akiwa anaongoza kwa mabao yake nane katika Ligi Kuu, sawa na Kipre Tchetche wa Azam FC, lakini katika mzunguko wa pili amefunga bao moja tu, katika mechi saba, tena kwa penalti.
    Baada ya mzunguko wa kwanza, Kavumbangu alipata ofa ya kununuliwa na klabu moja Qatar, ambayo ilikuwa tayari kutoa dola za Kimarekani 200,000 hata hivyo kutokana na kushuka kwa kiwango chake, ‘zali’ hilo kama limeyeyuka hivi.
    Dalili mbaya kwa Kavumbangu zilianza pale alipotemwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Burundi kilichocheza Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge nchini Uganda mwishoni mwa mwaka jana.
    Juhudi za kumpata Kavumbangu mwenyewe kuzungumzia haya, hazikufanikiwa mapema, ingawa BIN ZUBEIRY inaendelea na jitihada za kumpata ili kusikia kutoka kwake.     
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WAMBAINI MCHAWI 'ANAYEMLOGA' KAVUMBANGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top