• HABARI MPYA

  Jumatano, Machi 20, 2013

  KWA HILI ZFA IMEIPA SERIKALI KISU IICHINJE


  YAONEKANA hakuna dawa mjarabu itakayokifanya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kitawalike.
  Kwa miaka mingi sasa, jitihada za serikali kuona soka la Zanzibar linapiga hatua na kutambulika kimataifa, zimekuwa zikirudishwa nyuma kutokana na migogoro isiyokwisha ndani ya ZFA.
  Awali, kelele za wadau zilikuwa zikielekezwa kwa viongozi wa chama hicho, wakidaiwa kuwa hawana dhamira ya dhati kuiletea Zanzibar maendeleo katika mchezo wa mpira wa miguu.
  Kelele hizo zilimfanya Ali Ferej Tamim aliyekuwa Rais wa chama hicho kwa zaidi ya miongo miwili, aamue kukaa pembeni na kuruhusu kufanyika uchaguzi mdogo ili kupata Rais mwengine, ambaye alitarajiwa kushusha presha za wadau waliokuwa wakililia mabadiliko.
  Hatimaye, Juni 30, mwaka jana, ZFA ikaitisha uchaguzi mdogo uliomuweka madarakani Amani Ibrahim Makungu kuwa Rais kwa kipindi kilichobakia kabla ya uchaguzi mkuu wa Disemba 2014.
  Yalikuwa matumaini ya wengi, hata viongozi wakuu wa Serikali ya Zanzibar ambao hawakusita kuelezea kuchoshwa kwao na migogoro ya ZFA kila walipopata nafasi, kwamba sasa mpira utakwenda mbele.
  Matumaini hayo pia yalitokana na hatua ya Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad kuamua kwa makusudi kukutana na uongozi mzima wa ZFA na wadau wa soka, wakati huo kabla kujiuzulu kwa Ali Ferej, na kujadili kwa kina kinacholeta mivutano na kusaka muarubaini wa tatizo hilo.
  Wakati Wazanzibari wakianza kupata faraja na kuamini kuwa sasa ni maendeleo tu na migogoro basi, ndani ya kipindi cha miezi saba tu ya uongozi wa Amani Makungu, yameibuka makubwa na kumfanya Rais huyo aamue kuomba kujiuzulu.
  Ikitambua kwamba, kumkubalia Rais huyo aondoke, wengi wataelewa kuwa huenda tatizo la ZFA liko ndani ya kamati zake tendaji Unguja na Pemba, na pia katiba yake ambayo huko nyuma tuliambiwa eti imefanyiwa marekebisho, ZFA ilichukua muda kumbembeleza Makungu afute uamuzi wake huo.
  Baada ya kuona maji yamezidi unga, na kwamba kila mmoja sasa amefahamu kuwa chama hicho ni sawa na gunia la misumari lisiloweza kubebeka, kwa shingo upande ZFA, ikiendelea kuvunja katiba kwa kufanya kikao cha wajumbe wa kamati tendaji ya Unguja peke yao, iliridhia Makungu aondoke.
  Ni jambo lililozoeleka kwa chama hicho kimekuwa kikifanya maamuzi mengi na mazito yanayokiuka katiba, ndivyo pia kilivyofanya mara hii kwa kutoa baraka kwa Makungu kuachia ngazi, kwa kujikusanya kikundi tu cha wajumbe wa Unguja na kuwasemea wenzao wa kisiwa cha Pemba katika jambo zito kama hilo linalogusa maslahi ya taifa kimpira.
  Hapa tu panatosha kuipa nguvu serikali kuchukua maamuzi magumu ya kuivunja ZFA ambayo imeonesha wazi kuwa inashindwa kuendesha mambo kwa mujibu wa katiba yake iliyoiunda yenyewe.
  Kama mtu mwengine yeyote aliyechoshwa na jambo, Makungu alikuwa na  haki ya kuomba kujiuzulu na hakukuwa na haja ya kumlazimisha abakie.
  Lakini pamoja na haki hiyo, je, ZFA huku ikiongozwa na mwanasheria wake inayemtegemea, haikubaini kwamba kuamua bila kuwashirikisha wenzao wa Pemba na kukubali ombi la Rais huyo, lilikuwa kosa?
  Hapa ndipo panapoibuka dhana kwamba kamati tendaji ya ZFA Unguja, inawatenga wenzao wa upande wa pili kwani mara nyingi imekuwa ikifanya maamuzi makubwa peke yake.
  Yawezekana kwamba huko Pemba nako wako wajumbe wanaoafiki Makungu kuachia ngazi, lakini si kwa namna hii ilivyofanyika, ilipasa wote washirikishwe katika kutoa uamuzi.
  Je, madudu haya yaliyofanywa na ZFA ambayo si mwanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hayatoshi kuionesha serikali kwamba sasa umefika wakati wa kufanya maamuzi magumu na kukivunja chama hicho ili kuandaa mustakbali mzuri wa baadae?       
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KWA HILI ZFA IMEIPA SERIKALI KISU IICHINJE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top