• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 24, 2013

  ZANZIBAR IANZISHE MFUKO WA SEKTA YA UTALII KUCHANGIA MICHEZO


  INASIKITISHA kuwa Zanzibar imepata uanachama shirikishi wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), lakini inashindwa kuitumia ipasavyo fursa hiyo adhimu.
  Tangu ilipopata uanachama huo mwishoni mwa mwaka 2004, Zanzibar imekuwa ikiwakilishwa na klabu zake kwenye mashindano ya klabu barani Afrika, yaani Ligi ya Mabingwa na ile ya Kombe la Shirikisho.
  Kwa miaka yote hiyo, klabu zinazobahatika kuchukua ubingwa na ushindi wa pili katika ligi kuu ya Zanzibar zimekuwa zikishiriki mashindano hayo, japokuwa si kwa mafanikio kwani mara zote zimekuwa zikiishia katika raundi ya kwanza.
  Lakini mwaka huu, kwa bahati mbaya sana, Zanzibar haikuweza kuwakilishwa kwenye Ligi uya Manbingwa, baada ya klabu iliyokuwa ishiriki ambayo ndiyo bingwa wa Zanzibar msimu huu unaomalizika Super Falcon, ilijiondoa kwa sababu za ukosefu wa fedha.
  Kutokana na kujitoa kwa timu hiyo, Jamhuri iliyokuwa ikshiriki Kombe la Shirikisho ikalazimika kuchukua nafasi ya Super Falcon, huku nafasi yake ikikosa timu ya kuibeba.
  Tayari Jamhuri imeshatolewa kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kupoteza mechi zote mbili za raundi ya kwanza dhidi ya St. George, mabingwa wa Ethiopia.
  Katika uchambuzi huu, ninakusudia kuelezea masikitiko yangu juu ya uwezo mdogo wa timu zetu, unaozifanya ama zishiriki mashindano ya kimataifa kwa kuombaomba, au kutokushiriki kabisa kama ilivyotokea mara hii.
  Sote tunajua kwamba klabu za michezo ya aina yote hapa Zanzibar ni masikini sana, na kamwe haziwezi kupata nguvu ya kushiriki mashindano ya kimataifa bila kushikwa mkono kwa kuchangiwa fedha kwa ajili ya kujiandaa na pia kuingia mashindanoni. 
  Linalotia uchungu zaidi, ni kuona Super Falcon ikitangaza mapema kwamba haina uwezo wa kushiriki mashindano ya mwaka huu barani Afrika, na kwa hivyo ikatangaza kujitoa, lakini hakuna hata taasisi moja iwe ya umma au binafsi, iliyopata hisia na kusema angalau isaidie malazi kwa timu ya wageni, seuze nauli ya kuwasafirisha wawakilishi wetu hao.
  Hii inaonesha taswira mbaya kwamba sasa, Wazanzibari hawana tena moyo wa kusaidia sekta ya michezo, bali wamekuwa watu wa kutaka mafanikio tu bila kuchangia senti hata moja pale timu zetu zinapokwazwa na uhitaji.
  Daima tumekuwa watu wa kulalamika kila timu zetu zinapofanya vibaya kwenye ngazi ya kimataifa, lakini kamwe hatuko tayari kujipinda kwa kutoa misaada hata midogo midogo kama chupa za maji pale timu zinapokuwa zikijiandaa.
  Uko wapi moyo na ari ya kuisaidia Zanzibar kimichezo uliokuwepo miaka ya nyuma ilipoanzishwa kamati ya ‘Saidia Zanzibar Ishinde’ (SAZI) ingawa ilikuwa kwa ajili ya timu ya taifa?
  Umoja na mshikamano kama ule ndio ambao ungepaswa kuonekana sasa, wakati Zanzibar inapeleka klabu mbili kwenye mashindano ya Afrika kila mwaka.
  Kwa muktadha huo basi, ninapenda kutumia nafasi hii kuiomba Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, ianzishe utaratibu wa kuwataka wawekezaji katika sekta ya utalii hapa nchini, wachangie maendeleo ya michezo.
  Kutokana na umasikini wa timu zetu, umefika wakati sasa kuwe na mfuko maalumu wa kusaidia maendeleo ya michezo, utakaochangiwa na wawekezaji wa miradi mbalimbali hasa utalii ambao kwa bahati unaangukia katika wizara moja na michezo.
  Kwa kuwa utalii una matawi mengi nyingi kuanzia hoteli, mikahawa, huduma za kutembeza watalii, michezo ya baharini na nyenginezo, itakuwa jambo la busara kama wizara kwa kushirikiana na Kamisheni ya Utalii zitatafuta njia ya kupata asilimia fulani ya mapato yatokanayo na sekta hiyo na kuyaingiza moja kwa moja kwenye mfuko huo utakaonzishwa.
  Kwa kiasi fulani, ninaamini mpango huu utasaidia sana kuzipa uwezo timu zetu hasa klabu zinapokabiliwa na mashindano ya kimataifa, ambapo huwa zinapeperusha bendera ya nchi na kuifanya Zanzibar itambulike katika medani ya michezo.
  Ili kuufanya mpango huo ulete ufanisi na kuwapa moyo wawekezaji na wachangiaji wengine, lazima kuwe na uwazi na uaminifu katika kuutunza mfuko huo, na kuutumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
  Ingawa mkazo hapa ni sekta ya utalii, lakini makampuni mengine yakiwemo ya simu, viwanda na mashirika mbalimbali, yanaweza kutakiwa kuchangia katika mfuko huo.
  Haitakuwa busara, tuanzishe mfuko kwa ajili ya kusaidia sekta ya michezo, halafu tuje kusikia fedha zimetolewa kwa kuazimwa kwa ajili ya shughuli nyengine, na ikawa kuazimwa huko hakuna uhakika wa kurejeshwa.
  Tukumbuke kuwa, kwa miaka mingi Zanzibar imekuwa ikililia kutambuliwa kimataifa katika sekta ya michezo, hivyo itakuwa aibu kushindwa kuzitumia fursa tunazopata kwa kupeleka timu zetu nje kwa kisingizio cha kutokuwa na fedha.
  Au kama tunashindwa kumudu gharama za kushiriki mashindano, ni vyema tuamue kujitoa kwa angalau miaka mitano, kwa sababu ya kuwa timu zetu hazifanyi vizuri ili tuzijenge.
  Pengine, hiyo itakuwa dawa mjarabu, kwanza ya kuziandaa timu zetu, na pia huenda kwa muda huo tutakuwa tumeutunisha mfuko huo tutakaouanzisha ili tukirudi tusiwe waombaji.
  Tujaribu kuanzisha mfuko kama huo, huku tukiziandaa timu zetu vizuri na kuzipatia nyenzo muhimu na mechi za kirafiki za kimataifa ili kuzijengea uzoefu, asaa kheri milango ya mafanikio itatufungukia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: ZANZIBAR IANZISHE MFUKO WA SEKTA YA UTALII KUCHANGIA MICHEZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top