• HABARI MPYA

  Monday, March 25, 2013

  AZAM WAINGIA KAMBINI LEO KUIWEKEA AKILI SAWA PRISONS

  Kocha Stewart Hall akiwaongoza vijana wake mazoezini (Picha ya Maktaba).

  Na Mahmoud Zubeiry
  AZAM FC inaingia kambini leo kwenye hosteli zake za Azam Complex, zilizopo Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Jumatano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Prisons ya Mbeya keshokutwa.
  Kocha Mkuu wa Azam, Muingereza Stewart Hall ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba anashukuru kwa sasa hana majeruhi hata mmoja kikosini baada ya kupona kwa beki Sammih Hajji Nuhu.
  Hall amesema kwamba wachezaji wote wakiwemo wale waliokuwa na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa kilichocheza na Morocco jana wataingia kambini leo.
  Amesema anatarajia mchezo huo utakuwa mgumu, lakini wanajiandaa vizuri kuhakikisha wanashinda na kujiweka vizuri katika mbio za ubingwa.  
  Hall amesema kwamba mechi mbili za Ligi Kuu watakazocheza keshokutwa na mwishoni mwa wiki dhidi ya Ruvu Shooting zitawasaidia kabla ya kurudiana na Barrack Young Controller II ya Liberia katika Kombe la Shirikisho.
  Amesema wapinzani wao wote wawili ni wazuri na anaamini changamoto watakayoipata hapo, itawasaidia mno kabla ya kurudiana na B.Y.C. Aprili 6, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Azam ambayo inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu kwa pointi zake 37, nyuma ya Yanga yenye pointi 48, iliifunga B.Y.C. mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza ugenini wiki iliyopita.
  Sasa inahitaji hata sare katika mchezo wa marudiano nyumbani ili kusonga mbele. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: AZAM WAINGIA KAMBINI LEO KUIWEKEA AKILI SAWA PRISONS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top