• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 26, 2013

  STARS WA SIMBA SC KUJIFUA MWANZA LEO WAKISUBIRI NDEGE

  Mrisho Ngassa

  Na Mahmoud Zubeiry
  WACHEZAJI watano kati ya sita wa Simba SC waliokuwa katika kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichocheza na Morocco juzi, leo wanafanya mazoezi peke yao mjini Mwanza walipokwama kutokana na matatizo ya usafiri wakiwa njiani kuelekea Bukoba kuungana na wenzao kwa ajili ya mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar.
  Wachezaji hao waliondoka jana asubuhi Dar es Salaam, lakini walipofika Mwanza tayari kuunganisha ndege kwenda Bukoba, wakaambiwa Uwanja wa Ndege wa mkoa wa Kagera umejaa maji kutokana na mvua mfululizo zinazoendelea nchini na ndege haziwezi kutua.
  Kwa sababu hiyo, wakalazimika kulala hadi mchana ndipo waunganishe ndege kwenda Bukoba kwenda kuongeza nguvu kwenye timu yao kwa ajili ya mechi hiyo ya kesho dhidi ya wenyeji Kagera Sugar.
  Wachezaji hao ni kipa Juma Kaseja, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Shomary Kapombe na viungo Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.
  Akizungumza jana usiku kwa simu kutoka Mwanza, Mrisho Khalfan Ngassa aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba leo asubuhi watafanya mazoezi peke yao kujiweka fiti, kwa sababu ratiba inawabana.
  “Tutafanya mazoezi wenyewe watano hapa kesho ili kujiweka fiti, kwa sababu ratiba yenyewe imekwishakuwa inatubana na bila kufanya hivyo, tutafika kule tupo ovyo na kushindwa kucheza vizuri,”alisema Ngassa.
  Ni mchezaji mmoja tu wa Simba SC, Mwinyi Kazimoto aliyekuwa kwenye kikosi cha Stars kilichoiadhibu Morocco 3-1 juzi, ambaye ameachwa kwa sababu hayumo kwenye mipango ya kocha Mfaransa, Patrick Liewig kwa sasa.
  Tayari wachezaji wa Simba SC ambao hawakuwamo Taifa Stars, wapo Bukoba tangu Jumamosi kwa ajili ya mchezo huo wa Ligi Kuu.
  Wachezaji wengine wawili wa Simba waliokuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uganda, The Cranes kilichomenyana na Liberia juzi, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde nao wataungana na akina Ngassa leo mjini Mwanza kuunganisha safari kwenda Bukoba.
  Simba ambayo ni kama imekwishavuliwa ubingwa wa Ligi Kuu, kutokana na kuzidiwa pointi 14 na wapinzani wao wa jadi, Yanga wanaoongoza kwa pointi zao 48, inapigana kuhakikisha japo inakuwa ya pili kwa kuipiku Azam iliyo katika nafasi hiyo kwa pointi zake 37. Simba ni ya tatu ikiwa na pointi 34.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: STARS WA SIMBA SC KUJIFUA MWANZA LEO WAKISUBIRI NDEGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top