• HABARI MPYA

    Wednesday, March 20, 2013

    NONDA ALILOGWA NA MMACHINGA, KABLA YA TEGETE KUMLOGA KAVUMBANGU


    KIKOSI cha Yanga SC mwaka 1995, kilikuwa kinaundwa na idadi kubwa ya wachezaji waliopandishwa kutoka kikosi cha pili, Black Stars ambao waliandaliwa na aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye baadaye akapewa uraia wa Tanzania.
    Na Bin Zubeiry
    Tambwe ambaye kwa sasa ni marehemu, aliwasuka vijana hao na kupandishwa kikosi cha kwanza, baada ya klabu hiyo kufukuza idadi kubwa ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza waliomaliza msimu wa 1994 kwa tuhuma za kuhujumu timu ikafungwa 4-1 na mtani wake, Simba katika Ligi Daraja la Kwanza, sasa Ligi Kuu.
    Katika wachezaji wa Black Stars walikuwamo baadhi vijana wenye vipaji vya soka waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi na kuja Yanga kujiendeleza, miongoni mwa alikuwa Nonda Shabani ‘Papi’.
    Nonda alikuwa mshambuliaji mzuri ambaye cheche zake zilianza kuonekana mapema tu akiicheza Black Stars katika mechi mbalimbali za kirafiki, akishirikiana na akina Maalim Saleh ‘Romario’ pale mbele.
    Nonda alipata umaarufu mapema na kutokana na Black Stars kuanza vizuri msimu wa 1995, akapata jina kubwa. Baadaye kidogo, cheche za Nonda zikawa zimepungua na kilichotokea yakaibuka maneno ya chini chini, akidaiwa kumlalamikia mshambuliaji mkongwe Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ kwamba anamloga.
    Maneno yalizidi na siku moja wakiwa wanajiandaa kuanza mazoezi Uwanja wa Kaunda, Mmachinga akamtolea uvivu Nonda na kumuita. “Nilimuuliza, kwa nini wewe unanipakazia mimi nakuloga, nikuloge kwa sababu ipi?”aliniambia Mmachinga juzi, nilipomuuliza kumtaka anikumbushe sakata lake na Nonda.
    “Yeye mwenyewe alikuwa anafanya ngono sana, pale Mwananyamala alipokuwa anakaa, watu walikuwa wanamuona anaingiza wanawake hadi mchana, sasa akiingia uwanjani anaumia, anasema namloga. Mbaya zaidi alikuwa anakuja na viatu vyenye njumu ndefu. Mimi nikamuambia mambo mawili tu, acha ngono na acha kutumia hivi viatu vyenye njumu ndefu, tafuta vya njumu fupi uone kama utakuwa unaumia tena izo enka (vifundo vya mguu),”.
    “Bahati nzuri dogo (Nonda) akanisikiliza na baada ya hapo hakuumia tena, akawa anafanya vitu hadi akapata zali lake, akaenda Sauzi (Afrika Kusini), mara huyo Uswisi, Ufaransa sijui na Italia, England hadi Ubelgiji alipoachia mpira. Kawa tajiri kwa ushauri wangu. Lakini kama angekazania na ujinga analogwa, mpira ungemshinda mapema sana,”alisema Mmachinga.       
    Mmachinga hakujua kwa nini nilimtaka anikumbushe kile kisa- lakini akisoma makala haya, atajua. 
    Katika kikosi cha Yanga cha sasa kuna mshambuliaji anaitwa Didier Kavumbangu kutoka Burundi pia alikotokea Nonda. Huyu amesajiliwa msimu huu, baada ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame alipong’ara akiwa na klabu ya Atletico Olimpique.
    Aliyekuwa kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintefiet akavutiwa naye akaomba asajiliwe, na akasajiliwa. Kavumbangu alianza vyema Yanga akifunga mabao nane katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, baada ya hapo akatengeneza jina katika soka ya Tanzania.
    Baada ya mzunguko wa kwanza, zikaibuka habari za mshambuliaji huyo kutakiwa na klabu moja ya Qatar kwa dau la dola za Kimarekani 200,000. Uongozi wa Yanga haukubabakia ofa hiyo, ukiamini utamuuza kwa bei nzuri zaidi mshambuliaji wake huyo.
    Alikuwa hatari, ana kasi, nguvu, mwepesi, hatua, uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kugombea mipira, kupiga vichwa. Alikuwa mshambuliaji anayeweza kuivutia hata timu ya Ulaya.
    Ajabu, kuanza kwa mzunguko wa pili cheche za mshambuliaji huyo zimeyeyuka na amepoteza sifa nyingi kati ya hizo alizokuwa nazo. Katika mechi saba za mzunguko wa pili alizocheza, Kavumbangu amefunga bao moja tu, tena kwa penalti na katika mechi dhidi ya timu dhaifu, African Lyon. Imefikia hadi penalti anakosa. 
    Mwezi uliopita ziliibuka habari, Kavumbangu amegombana na mshambuliaji aliyemkuta Yanga, Jerry Tegete akimtuhumu anamloga. Wakati watu bado wakiumiza kichwa juu ya ugomvi wa wawili hao, zinaibuka habari juu ya mabadiliko ya mfumo wa maisha ya Kavumbangu baada ya kuwa nyota.
    Kwa ufupi, anadaiwa amekuwa mtu wa anasa sana, na kwamba hilo ndilo linalomuathiri kisoka hivi sasa. Viongozi wa Yanga wamejiridhisha, mshambuliaji huyo amekuwa muumini wa starehe na amesahau kilichomleta Yanga. Kwa kifupi amepoteza malengo na uongozi umempa muda wa kujirekebisha kwa kipindi kilichobaki kuelekea mwishoni mwa msimu, vinginevyo atauzwa au kutolewa kwa mkopo.
    Sijawahi kukutana na Kavumbangu katika anga za maisha yake binafsi, lakini kwa ninavyomuona uchezaji wake wa sasa anaathiriwa na kile kitu ambacho unaweza kukiita kutokuwa fiti. Kwa nini hayuko fiti na anafanya mazoezi karibu kila siku?
    Hapo sasa ndipo mtu unapoweza kushawishika kuamini yanayozungumzwa juu yake, kwamba anasa zinammaliza. Kweli tuna tatizo la jumla la ubutu wa safu ya ushambuliaji wa Yanga kwa sasa, lakini kwa Kavumbangu unaweza kuona ana tatizo la ziada.
    Wenzake wanakosa mabao mfano Tegete, lakini unaweza kuona uchezaji wao, tatizo ni kushindwa kufunga tu, ila bado ni washambuliaji imara.
    Ipo haja kwa Kavumbangu kuachana na dhana kwamba eti analogwa na kujitazama mara mbili, wakati anaingia Yanga alikuwa anaishije na sasa anaishije. Bado kijana mdogo na kwa kuwa ana kipaji, kama kweli tuhuma anazozungumziwa ndizo zinazomdhoofisha, akijirekebisha atakuwa tishio tena.
    Nakumbuka tangu siku ya kwanza anakuja Yanga, anatambulishwa hadi anasaini mkataba. Kavumbangu alikuwa mchezaji aliyetokea kwenye maisha magumu na mwonekano wake ulidhihirisha hayo kuanzia mavazi.
    Kavumbangu wa leo anaonekana ni mtu ambaye yuko njema kidogo, anapata fedha Yanga, ambazo alipokuwa Burundi alikuwa hazipati. Lakini Kavumbangu anatakiwa kujua Yanga hakuna fedha, fedha zipo kule alipocheza Nonda, ambaye sasa baada ya kustaafu kwa kuwa alizichanga vyema karata zake ni tajiri.
    Nilikwenda DRC mwaka jana na nilijionea vitegauchumi na rasilimali za Nonda pale DRC. Soka imemnufaisha. Lakini kama anavyosema Mmachinga, iwapo Nonda asingejitambua mapema na kujirekebisha akakazania imani za kulogwa, dhahiri mpira ungemshinda mapema. Ni juu yake Didier, kusuka au kunyoa. Wasalam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NONDA ALILOGWA NA MMACHINGA, KABLA YA TEGETE KUMLOGA KAVUMBANGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top