• HABARI MPYA

    Wednesday, March 27, 2013

    IKULU YAONYA; JK ASILISHWE MANENO KUHUSU UZINDUZI WA AZAM COMPLEX KUHUSU SIMBA NA YANGA

    Rais JK akizindua Azam Complex

    "RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alitembelea na kuzindua rasmi Uwanja wa Michezo wa Azam Complex ulioko Chamazi, Temeke, Dar es Salaam unaomilikiwa na Kampuni ya Said Salim Bakhressa Group Alhamisi iliyopita, Machi 21, 2013.
    Rais Kikwete alizindua Uwanja huo wa Azam Complex unaotumiwa na Klabu ya Soka ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ya Azam FC ikiwa ni tukio la mwisho la ziara yake yenye mafanikio makubwa ya siku nne katika Mkoa wa Dar Es salaam.
    Wakati wa hotuba yake ya uzinduzi wa Uwanja huo, Mheshimiwa Rais Kikwete aliipongeza Klabu ya Azam kwa kuwa dira na mfano nzuri wa  kuendeleza soka nchini na kuwekeza katika  maendeleo ya mchezo huo unaopendwa na wenye washabiki wengi nchini kwa njia za kisasa.
    Tokea siku hiyo ya Alhamisi, Vyombo mbali mbali vya habari nchini yakiwemo magazeti vimetangaza na kuandika habari nyingi na wachambuzi wa michezo wameandika maoni na uchambuzi wao wa kila aina kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Rais Kikwete kwenye hafla hiyo.
    Wengine wameandika vizuri kwa mujibu wa ujumbe wa Rais Kikwete kwa wanamichezo wa Tanzania na taasisi za michezo katika nchi yetu. Lakini kwa bahati mbaya, wapo wachache ambao wamepindisha ujumbe huo, wengi wao wakimlisha maneno ambayo hakuyatamka Mheshimiwa Rais. 
    Aidha, wengine wamejaribu kutumia kauli ya Rais Kikwete kuwashambulia wapinzani ama washindani wao katika soka. Katika ari ya kila mtu kuzusha jambo lake chini ya kivuli cha kauli ya Rais Kikwete, wengine hata wametumia michoro ya katuni kwenye magazeti ili “kufafanua” kile alichokisema Mheshimiwa Rais.
    Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kutoa ufafanuzi wa baadhi ya kauli hizo za vyombo vya habari kama ifuatavyo:

    (a)               Kwamba nia ya Mheshimiwa Rais Kikwete kwenye hotuba yake ilikuwa kupongeza jitihada za Klabu ya Azam na Kampuni mama ya klabu hiyo Bakhressa Group kwa kuchukua njia sahihi na za kisayansi kuendeleza mchezo wa soka nchini.

    (b)               Kwamba haikuwa nia ya Mheshimiwa Rais kuzikemea ama kuzisema taasisi nyingine za soka katika Tanzania ambazo nazo kwa namna yake zinachangia maendeleo ya soka katika nchi yetu.

    (c)                Kwamba, Mheshimiwa Kikwete,  kama mpenzi wa soka na michezo maisha yake yote anatambua na kuheshimu mchango wa Klabu za Soka za Simba na Yanga na changamoto ambazo zinazikabili klabu hizo katika kuinua kiwango cha michezo nchini. Hivyo, ni jambo lisilowezekana kuwa yeye anaweza kuzikejeli kwa namna yoyote hizo klabu hizo kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari vimejaribu kuelezea tokea alipozindua Azam Complex.

    Hakuna shaka kuwa Rais Kikwete anajua fika na anaamini kuwa waandishi wa michezo nchini wanafanya kazi kubwa na nzuri na wakati mwingine katika mazingira magumu ya kuwahabarisha, kuwaelimisha na kuwaburudisha wananchi kuhusu michezo na maendeleo yake nchini. Ushauri wake ni kwamba waendelee kufanya jitihada zaidi za kuongozwa na misingi ya taaluma, weledi na ukweli zaidi katika kuifanya kazi yao,"
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: IKULU YAONYA; JK ASILISHWE MANENO KUHUSU UZINDUZI WA AZAM COMPLEX KUHUSU SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top