• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 30, 2013

  MRISHO NGASSA NA CRISTIANO RONALDO...

  KARIBUNI sana katika safu hii mpya iitwayo Ordem e Progresso. Hii ni safu mpya katika blogu hii ya rafiki yangu Mahmoud Zubeiry. Hii ni zawadi yangu kwa ajili ya blogu yake hii na mafanikio iliyoyapata, lakini pia ni shukrani yangu kwake kwa sababu wengi hawafahamu kuwa huyu bwana ni miongoni mwa watu walionipokea wakati nikianza kazi ya uandishi wa habari.

  Nimeazima maneno haya- Ordem e Progresso kutoka katika bendera ya Brazil. Maana yake kwa lugha ya Kiswahili (tafsiri isiyo rasmi ni Maendeleo kwa Utaratibu). Kwamba lazima haya mambo mawili yaende kwa pamoja.
  Utashangaa kwamba Wabrazil nao waliiga maneno haya kutoka kwa Mwanafalsafa wa Kifaransa, Auguste Comte, aliyetamka maneno haya zamani sana kwa lugha ya Kifaransa -"L’amour pour principe et l’ordre pour base; le progrès pour but" ("Love as a principle and order as the basis; progress as the goal").
  Kwa tafsiri (kwa mara nyingine, isiyo rasmi), Comte anasema kwamba Mapenzi yakiwa kama kanuni, Utaratibu ukiwa pa kuanzia…Maendeleo Yatakuwa Lengo.
  Lengo la safu hii ni kujaribu kujadiliana namna ya kufika tunapotaka kwenda. Ila, badala ya kulaumu kila kukicha, ninachokitaka ni kuchochea kupendana, kisha tuweke utaratibu ili tufikie malengo.
  Hutaona lawama zikizidi katika safu hii. Hutaona mtu au taasisi ikikashifiwa katika safu hii. Utaona mapenzi ya kweli kuelekea kwenye maendeleo. Karibuni katika Ordem e Progresso


  MRISHO NGASSA NA CRISTIANO RONALDO...
  NAFIKIRI sihitaji kumtambulisha Mrisho Ngassa kwa yeyote anayesoma makala hii kwa sasa. Katika kipindi cha miaka takribani sita au saba sasa, amekuwa miongoni mwa wachezaji bora hapa nchini.
  Lakini ni muhimu nikaweka baadhi ya takwimu wazi ili niweze kuelekeza mjadala huu kule ninakotaka uende. Kama alivyowahi kusema Comte niliyemtaja kwenye utangulizi wa makala hii, mjadala ule mzuri ni ule unaoendeshwa na takwimu au data zinazofahamika tayari.
  Mpaka kufikia hatua hii ya Ligi Kuu ya Tanzania, Ngassa ametoa pasi saba za magoli (assist) katika mechi alizocheza. Ukifanya mlinganisho na Ligi kubwa za Ulaya, amezidiwa kwa pointi tatu na kinara wa pasi hizo katika Ligi Kuu ya England, Juan Mata, aliye na pasi 10.
  Hata hivyo, idadi hiyo ni takribani nusu ya pasi 15 alizotoa David Silva msimu uliopita katika klabu ya Man City. Ni nusu pia ya pasi 14 alizotoa Nani wa Man United misimu miwili iliyopita.
  Niseme kitu kingine. Idadi hiyo ya pasi ni sawa na pasi zote alizotoa Robin Van Persie katika msimu mzima wa Ligi Kuu ya England msimu uliopita.
  Kwa idadi hiyo ya pasi za magoli ya Ngassa, hivi sasa ana wastani mzuri zaidi kuliko walionao akina Xavi Hernandez (ana pasi tano hadi sasa), Cristiano Ronaldo, Angel Di Maria, Luis Suarez, Steven Pienaar na wengineo.
  Hapa sitaki kusema kwamba Ngassa ni bora kuliko hao niliowataja. Pointi yangu hapa ni kwamba, si rahisi kutoa pasi saba za magoli katika msimu mmoja wa ligi. Tena ligi yenyewe ikiwa na timu 14. Sisi tuna mechi za ligi 26 msimu mzima, wenzetu wana mechi 38. Mechi 12 pungufu !
  Halafu angalia rekodi ya nidhamu ya mchezaji huyu. Kama kumbukumbu zangu ziko sahihi, hajawahi kupewa kadi nyekundu wala ya njano tangu aanze kuchezea klabu ya Simba msimu huu.
  Ninaamini, katika miaka yake nane ya kucheza Ligi Kuu ya Tanzania, Ngassa hawezi kuwa amefikisha kadi tano za njano. Sijawahi pia kumuona akigombana na mtu uwanjani au nje ya uwanja.
  Amewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Tanzania miaka mitatu au minne iliyopita. Sidhani kama kuna mchezaji hapa nchini ambaye ana uwezo mkubwa wa kufunga na kusababisha mabao hapa nchini sawa sawa na Mrisho.
  Wachezaji wenzake wanamheshimu sana na ndiyo maana wanamuita Anko. 
  Hata hivyo, Ngassa anapita katika kipindi kigumu cha uchezaji wake hivi sasa. Tuhuma, lawama na kila kitu kinaelekezwa kwake. Kumbuka, huyu ni mchezaji ambaye mwanzoni mwa msimu huu alikuwa na ndoto za kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu.
  Mwishoni mwa mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwaka huu, Cristiano Ronaldo, alielezwa kutokuwa na raha wakati akichezea Real Madrid. Inadaiwa, alikuwa hapewi heshima inayostahili na washabiki wa klabu yake hiyo ya Los Merengues.
  Kwamba pamoja na kuibeba Real, bado uongozi na washabiki ulikuwa haumpi heshima kama waliyokuwa wakipewa akina Iker Casillas, Sergio Ramos na Raul Gonzalez. 
  Baada ya mechi baina ya Real na Man United, Ronaldo hakuonekana mwenye furaha. Goli lake ndilo lililoitoa United. Alipofunga hakushangilia hilo bao.
  Hata hivyo, kwa sasa yeye ndiye mchezaji muhimu zaidi wa Real. Washabiki wa Real walielewa huzuni yake kwa vile ameeleza wazi mapenzi yake kwa Man United. Kila mtu anajua.
  Ila, kitu watu wasichojua ni kwamba Real ndiyo timu ambayo Ronaldo alikuwa akiishabikia kuliko United. Alikwenda England kutafuta maisha na ndiyo maana Real walipomtaka alikwenda.
  Hata hivyo, mapenzi waliyomuonyesha Man United yamemfanya aiweke pia moyoni mwake. Kuna uwezekano akarudi England siku moja. Hii maana yake ni kwamba unaweza kuipenda timu ambayo hukuishabikia utotoni.
  Jamie Carragher alikuwa shabiki mzuri wa Everton utotoni lakini sasa anaitwa Mr. Liverpool. 
  Kuna madai kwamba Ngassa ana mapenzi na Yanga. Inaweza kuwa kweli au si kweli. Hata hivyo, anaweza kuwa na mapenzi na Simba kama tu watu watamwonyesha mapenzi na mshikamano.
  Anaweza pia kuwa shabiki wa Simba, kama baadhi yetu tunavyofahamu. Hata hivyo, anaweza kuipenda Yanga kutokana na namna wapenzi, washabiki, viongozi na wachezaji walivyoishi naye.
  Wanaisaikolojia ya michezo wamebaini kwamba mchezaji anaweza kubadili mapenzi yake kutoka timu moja kwenda nyingine kutoka na mapenzi anayoonyeshwa na timu anayochezea.
  Maana yake ni kwamba, Ngassa inawezekana kabisa akawa anaipenda Yanga lakini angeweza kuipenda Simba au Azam baadaye kutokana na namna atakavyotendewa huko.
  Au, inawezekana Ngassa akawa shabiki wa Simba lakini akaipenda Yanga kutokana na mapenzi na namna anavyotendewa na washabiki wa timu hiyo. Ronaldo alipiga makofi upande wa washabiki wa Man United waliokuwa wakimshangilia, Ngassa anaweza kupiga makofi upande wowote wa washabiki wanaomshangilia. Ni shukrani. Ni Fair Play.
  Mchezo wa mpira una dhana nyingi sana. Niliwahi kushuhudia Emmanuel Okwi akitaka kupigwa na washabiki wa Simba kwa madai kwamba ni shabiki wa Yanga na huwa hafungi kwa makusudi.
  Ni mashabiki haohao ambao sasa wanalalamika kwanini aliuzwa na uongozi kwenda Tunisia. Nakumbuka Kelvin Yondani alivyoishi kwa taabu baada ya kupitwa na Ngassa na kusababisha Simba ifungwe.
  Kwenye mechi nyingine, krosi ya Rashid Gumbo wa Yanga ilitua kwenye kichwa cha Kenneth Asamoah aliyekuwa amebanwa na Yondani na kuandika bao.
  Kelvin aliandamwa na tuhuma kwamba huwa anauza mechi. Ilifika wakati, ikifika mechi ya Simba anajiuliza acheze au vipi. Leo hii, Yondani pengine ndiye mlinzi bora zaidi wa kati hapa nchini na wale wale waliokuwa wakimpa wakati mgumu Simba, ndiyo wanaolalamika aliachwa vipi aende Yanga?
  Ujumbe wangu mkubwa leo kwenye safu hii ni upendo kwa wachezaji. Hata kama Ngassa ataamua kwenda Yanga au popote kule mwisho wa msimu, tumpe fursa ya kuitumikia Simba kwa moyo wake wote, nguvu zake zote na akili zake zote.
  Lengo ni kwamba akumbuke nyakati zile nzuri alipokuwa na Simba. Lengo ni kwamba, wachezaji wajue ya kuwa wakichezea klabu fulani, wataishi vizuri kwa muda wao wote.
  Anachohitaji Ngassa, na wanachohitaji wachezaji wote wa mchezo wowote ni kuhisi kwamba wachezaji wenzao, washabiki wao na viongozi wao wanawapenda na kuwajali muda wote.
  Wakiwa wazima au wagonjwa, wakiwa kwenye fomu au wakiwa chini ya kiwango. Wakiwa washabiki wa timu wanayochezea au wa timu pinzani. 
  Mapenzi ndiyo msingi, utaratibu ndiyo kanuni na lengo litafikiwa. Ordem e Progresso.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MRISHO NGASSA NA CRISTIANO RONALDO... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top