• HABARI MPYA

  Jumanne, Februari 26, 2013

  MRISHO NGASSA AFUNGUA YA MOYONI SIMBA SC, ASEMA...

  Mrisho Ngassa

  Na Mahmoud Zubeiry
  MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Mrisho Ngassa amesema kwamba wapo katika wakati mgumu kutokana na matokeo yasiyoridhisha ndani ya timu yao na hali kwa ujumla ndani ya klabu.
  “Tupo katika wakati mgumu, kwa ujumla kama wachezaji na hali halisi ndani ya klabu, tunajitolea sana, tunajituma. Wakati mwingine tunashinda, ila wakati mwingine inakuwa kama hivi,”alisema Ngassa juzi alipozungumza na BIN ZUBEIRY baada ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, ambayo Simba ililala 1-0.
  Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ngassa aliingia uwanjani dakika ya 58 akitokea benchi kwenda kuchukua nafasi ya Haruna Chanongo na kukaribia kufunga mara mbili.
  Kuhusu kuanzia benchi, Ngassa alisema; “Mimi sijui kwa nini kocha alinianzishia benchi, ila sina tatizo lolote, nafanya mazoezi, nipo kambini na sijafanya utovu wowote wa nidhamu, sijui mwenyewe,”alisema.
  Hata hivyo, Ngassa alisema kwamba hiyo haimuathiri hata kidogo na ataendelea kufuata maelekezo ya kocha huyo kadiri atakavyo. “Akisema naanza, nitaanza, akisema nasugua (kukaa benchi) poa, hata asiponipa jezi kabisa, nitaheshimu maamuzi yake,”alisema.
  Simba SC imeuweka rehani ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia kukubali kuachwa mbali na Yanga na Azam katika msimamo wa ligi hiyo.
  Yanga inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 39, baada ya kucheza mechi 17, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 36 baada ya kucheza mechi 18, wakati Simba SC iko nafasi ya tatu kwa pointi zake 31, baada ya kucheza mechi 18 pia.
  Katika Ligi ya Mabingwa Afrika pia, Simba SC iko mguu nje, mguu ndani, kufuatia kuanza vibaya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza, baada ya kufungwa nyumbani 1-0 na Recreativo de Libolo ya Angola wiki iliyopita.
  Simba SC sasa inakabiliwa na changamoto ya kushinda ugenini mabao 2-0 ili isonge mbele, wakati timu hizo zitakaporudiana mwishoni mwa wiki.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MRISHO NGASSA AFUNGUA YA MOYONI SIMBA SC, ASEMA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top