• HABARI MPYA

    Wednesday, February 20, 2013

    YANGA WAJIFUA VIKALI BAGAMOYO

    Kocha Brandts akiwanoa vijana wake

    Na Baraka Kizuguto, Bagamoyo
    KIKOSI cha Yanga SC leo asubuhi kimeanza mazoezi kwenye Uwanja wa Mbegani, Bagamoyo kujiandaa na mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wapinzani wao wakuu katika mbio za ubingwa, Azam FC utakaofanyika Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga, ambayo iliingia kambini katika hoteli ya Kiromo mjini hapa jana mchana kujiandaa na mchezo huo, leo asubuhi imefanya mazoezi chini ya benchi lake zima la ufundi, likiongozwa na Kocha Mkuu, beki wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, Ernie Brandts, Kocha, beki wa zamani wa Yanga, Freddy Felix 'Minziro' na kocha wa makipa, Mkenya Razack Ssiwa.
    Kikosi cha Mholanzi Ernest Brandts, kwa ujumla kinaonekana kuwa kwenye hali nzuri na wachezaji wote wanaoekana kuwa kwenye ari ya mchezo huo wa Jumamosi, ambao ndio utakaotoa taswira ya bingwa wa msimu huu.
    Yanga ambayo katika mchezo wake wa mwisho wa ligi hiyo, iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya African Lyon, kwa sasa inaonekana safu yake ya ushambuliaji ina uchu wa mabao.
    Kocha Brandts amesema kikosi chake kipo katika hali nzuri, mazingira ya kambi ni mazuri, wachezaji wanapata fursa ya kukaa pamoja na kushiriki mazoezi kwa pamoja katika hali ya utulivu, hali ambayo anaamini inaongeza umakini katika kuelewa maelekezo yake.
    “Najua macho na masikio ya wapenzi wa soka nchini yansubiri kuona nini kitatokea siku ya Jumamosi, ukweli ni kwamba huo ni mchezo muhimu sana kwetu, ili kujiweka katika hali nzuri ya kuendelea kuongoza ligi, hivyo nachoweza kusema ni kwamba nimekiandaa kikosi changu ili kiweze kuibuka na ushindi katika mcheo huo siku ya Jumamosi,”alisema Brandts.
    Aidha, Brandts alisema anafarijika kuwa na wachezaji wake wote 26 kambini kujiandaa na mchezo huo wa Jumamosi. “Wachezaji wote wapo safi kiafya, kiakili na morali ya kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huo, hivyo ninashukuru nitapata fursa ya kumtumia yeyote kati yao,”alisema.
    Yanga kwa sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 36, baada ya kucheza michezo 16, ikiwa imeshinda 11, imetoka sare tatu na kupoteza miwili, huku ikiwa imefunga jumla ya mabao 33 na kufungwa mabao 12 tu.
    Nafasi ya pili inashikiliwa na Azam FC yenye pointi 33, baada ya kucheza mechi 16 pia, ina mabao 27 ya kufunga na 14 ya kufungwa. Azam inatarajiwa kucheza mechi ya 17 leo kwenye Uwanja wake wa Azam Complex, uliopo Chamanzi dhidi ya JKT Ruvu.
    Inaweza kuifikia Yanga kwa pointi ikishinda leo, lakini kupanda kileleni itategemea na idadi ya mabao itakayoshinda leo, kwani vinara hao wa Ligi Kuu wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WAJIFUA VIKALI BAGAMOYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top