• HABARI MPYA

    Tuesday, February 26, 2013

    MILOVAN NDIYE MSINGI MKUU WA MATATIZO SIMBA SC


    Milovan akimuangalia Hamatre akiongoza mazoezi
    Na Mahmoud Zubeiry
    KATIKA sehemu moja tu ambayo Simba SC ilifeli zaidi msimu huu ni kwenye usajili na ndicho kitu ambacho kimekuwa kikiiumiza klabu hiyo kuanzia katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Profesa Milovan Cirkovick, ni kocha aliyemaliza msimu na Simba SC ikifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, kwa kikosi imara ambacho alikikuta, akianza kazi mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
    Simba iliyoanza mzunguko wa kwanza chini ya kocha Mganda, Moses Bassena ilimaliza mzunguko huo ikiwa kileleni mwa Ligi Kuu, lakini katika mastaajabu ya wengi, kocha huyo akafukuzwa na kuletwa Milovan.
    Mgogoro wa uongozi ndani ya wapinzani wao wakuu, Yanga SC, ulirahisisha kampeni ya Simba SC kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 62, dhidi ya 56 za Azam FC walioshika nafasi ya pili na 49 za Yanga.
    Simba ilimaliza msimu vizuri, hilo halina ubishi, lakini kuelekea msimu huu Milovan akiwa kocha Mkuu, alishindwa kurejesha timu kali kama aliyoikuta.
    Patrick Mafisango alifariki hata kabla dirisha la usajili halijafunguliwa, Kevin Yondan alihamia Yanga wakati Simba SC bado ina nafasi ya kusajili beki mwingine.
    Lakini tukumbuke, kila Simba ilipokuwa ikipoteza mechi, waliibuka watoa maoni juu ya uchezeshwaji wa pamoja wa Juma Nyosso na Yondan kama si sahihi, kwa sababu wote wana aina ya moja ya uchezaji.
    Hii maana yake, Simba ilihitaji kusajili beki, je Milovan alimsajili au alipendekeza nani asajiliwe? Mussa Mudde inaonekana ndiye mtu aliyesajiliwa kuziba pengo la Mafisango, lakini leo unaweza kujiridhisha ameshindwa na badala yake sasa, Amri Kiemba ndiye amefanya kazi hiyo.

    USAJILI MBOVU CHINI YA MILOVAN…
    Kimsingi baada ya kumalizika kwa msimu uliopita wa mashindano, Milovan alipaswa kuwa na orodha ya wachezaji anaotaka wasajiliwe ndani ya Simba SC, hakuna hakika kama alifanya hivyo.
    Wapinzani wake, Yanga na Azam walifanya usajili mzuri na matunda yake ni matokeo yao mazuri hivi sasa Ligi Kuu.
    Kilichokuwa kinaonekana ni Milovan kufanyiwa usajili na viongozi, maana yake yeye hakujishughulisha na zoezi hilo.
    Na alilundikiwa wachezaji wa akila aina, akina Kiggi Makassy, Salim Kinje, Kanu Mbivayanga, Lino Musombo, Patrick Ochieng, Daniel Akuffo na Danny Mrwanda.
    Bado huwezi kuona kiini cha kusajiliwa kwa fedha nyingi tu za klabu kwa wachezaji kama Mbivayanga, Musombo, Akuffo, Mrwanda na Ochieng kisha wakaachwa ndani ya siku chache.
    Lakini unachoweza kukiona kwa haraka ni udhaifu wa kocha mkuu katika usajili, kwa sababu kama baada ya msimu uliopita angekuwa na orodha yake ya wachezaji wa kusajiliwa, viongozi wasingekimbizana kusaka wachezaji.
    Na wachezaji wote ambao aliletewa Milovan, alipata muda mrefu wa kukaa nao kabla ya kukamilishwa kwa usajili wao, maana yake aliwakubali, baadaye ndio wakaonekana hawafai.
    Kumbuka wale akina Musombo na Mbivayanga, alifanya nao mazoezi kwa muda mrefu pale TCC Chang’ombe na wakasifiwa sana na vyombo vya habari nchini, akacheza nao mashindano ya Urafiki, baada ya hapo ndio wakaonekana magalasa wakatemwa.
    Akuffo na Ochieng, alikaa nao kwa mwezi mzima kambini Arusha, akawasifia ni wachezaji wazuri, wakasajiliwa, lakini baada ya muda mfupi wakaonekana ni magalasa wakatemwa. Hawakuondoka bure wote hao, waliitia hasara kubwa klabu.
    Kwanza walisajiliwa kwa fedha, na ili kuwaondoa ililazimu kuvunjwa mikataba yao kwa malipo ya fedha nyingi pia, hizi ni hasara ambazo klabu ikihisi maumivu yake, mtu wa kwanza kumnyooshea kidole ni Milovan.
    SILAHA ZA MILOVAN; Kutoka kushoto Paschal Ochieng, Kiggi Makassy na ABdallah Juma

    JINAMIZI LA MAFISANGO NA KUUZWA KWA OKWI…
    Simba ikifanya vibaya, mifano inayotolewa ni Mafisango na Emmanuel Okwi, lakini watu hawahoji juu ya kushuka kwa viwango vya wachezaji wengine wa timu hiyo kama Felix Sunzu na Haruna Moshi ‘Boban’, au wale makinda akina Ramadhan Sinagano ‘Messi’ na Edward Christopher.
    Okwi ameondoka katika wakati ambao Simba imempata Mrisho Ngassa na ameuzwa kwa bei nzuri tu, dola za Kimarekani 300,000 zaidi ya Sh Milioni 450 ambayo ni faida kubwa kwa klabu, akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa Simba aliyeuzwa kwa bei kubwa zaidi.
    Baada ya Simba SC kufungwa bao 1-0 na Recerativo de Libolo ya Angola katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, tathmini za wengi zilisema timu hiyo iliathiriwa na kukosa mshambuliaji.
    Ikumbukwe huyu Okwi alikuwa wa kuondoka Simba SC mapema tu kabla ya kuanza kwa msimu mpya, kama angefanikiwa katika majaribio yake Afrika Kusini, je Milovan alijiandaaje kumpoteza Mganda huyo, au ndiyo usajili wa Kinje?
    Mussa Mudde aliyesajiliwa kuziba pengo la Mafisango

    KUFUKUZWA KWA MILOVAN…
    Baada ya hasara zote alizoitia Simba SC, kufukuzwa ni kitu ambacho kilitarajiwa kwa Milovan, achilia mbali matokeo mabaya ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Simba ikimaliza katika nafasi ya tatu.
    Kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja aliofanya kazi tangu arejeshwe Simba SC, Milovan amedhihirisha kufeli. Aliikuta timu iko vizuri baada ya makocha wengine kufanya kazi ya kuitengeneza kuanzia Patrick Phiri na baadaye Basena, akatamba nayo mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita, baada ya hapo akashindwa kuendeleza makali yake.
    Ajabu, baada ya kufukuzwa Milovan anaanza kuibuka na kauli ambazo zinalenga kuleta chokochoko ndani ya Simba SC.
    Anadai alikuwa anaingiliwa katika upangaji wa timu, akisema alikuwa anaulizwa kwa nini amempanga fulani badala ya fulani na kutokana na msimamo wake wa kukataa kuingiliwa, watu wakamchukia wakamfukuza.
    Anawashika uchawi kundi la Friends Of Simba na Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ eti ni watu hatari katika timu.
    Kwa hali ilipofikia juu ya madudu aliyoyafanya Milovan katika usajili, dhahiri kiongozi yeyote makini anaweza kuanza kumtilia shaka na kuhoji kwa nini hakumpanga fulani badala ya fulani, ilikuwa sahihi kulingana na hali halisi ya kocha mwenyewe.
    Kocha kapewa wachezaji Akuffo na Ochieng, kakaa nao kambini Arusha mwezi mzima akapendekeza wasajiliwe, kumbe ni magalasa, kweli kesho utashindwa kuhoji upangaji wake wa timu?
    Nilikuwa nafuatilia sana mazoezi ya Milovan kuanzia kule Uwanja wa Kinesi hadi TCC, hakuwa mtendaji mzuri sana. Mara nyingi alikuwa anachelewa kufika mazoezini na alikwishaanza kugombana na uongozi kwa kuwapa wachezaji mazoezi hafifu.
    Milovan anaweza kufika amechelewa, akafikia nje kuvuta sigara baada ya hapo akiingia uwanjani ndani ya nusu saa anamaliza mazoezi. Haya yalikuwa yanatokea pale Kinesi na hata watu watakuwa wanakumbuka. 
    Kwa ilipofikia, mabadiliko katika benchi la ufundi la Simba SC yalitarajiwa na klabu haikukosea kumtupia virago Milovan.
    Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Hamatre Richard (mwenye kofia) akiwapa mawaidha wachezaji wa timu hiyo kabla ya mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam wakati wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu na chini ni Milovan akiwa nje ya Uwanja anavuta sigara yake. 

    Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovick akivuta sigara yake wakati Hamatre anazungumza na wachezaji

    HALI IKOJE BENCHI LA UFUNDI HIVI SASA?
    Yule babu Mfaransa, Patrick Liewig huwa anasimama muda mrefu peke yake akipigizana kelele na wachezaji wakati wa mechi. Anafika mapema mazoezini kila siku. Anaonekana ni mtu ambaye ana juhudi na kazi.
    Wasaidizi wake, Moses Basena, Jamhuri Kihwelo na James Kisaka wapo nyuma yake wakati wote na hawamuingilii zaidi ya kumshauri, naye anaonekana kusikilizana nao.
    Tatizo lipo kwenye timu aliyoirithi kutoka kwa Milovan, ina mapungufu makubwa. Kuna tatizo bado katika beki ya kati na kuna tatizo katika ushambuliaji. 
    Kuna tatizo la nidhamu- hizi ni changamoto ambazo anakabiliana nazo huyo Mfaransa na sidhani kama ana maisha marefu Simba SC, kutokana na desturi yetu ya kutoana ‘kafara’, iwapo matokeo mabaya yataendelea.
    Lakini kwa vyovyote, Milovan ndiye msingi wa matatizo yanayoisibu Simba SC uwanjani hivi sasa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MILOVAN NDIYE MSINGI MKUU WA MATATIZO SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top